The House of Favourite Newspapers

Miaka Minne Ndani ya Mapango ya Amboni – 39

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
“Sasa ni kwa nini afanye hivyo?” Mtu mwingine aliuliza kwa mshangao.
Faiza akabetua mabega yake.
“Sababu yake siijui. Anachosema yeye ni kuwa amenitunuka.”
Wakati tunaendelea kuzungumza na Faiza tukauona tena ule mwanga ambao ulimweka mbele yetu.
Nilishtuka sana.

SASA ENDELEA…
Ghafla tukamuona yule jini ameibuka mbele yetu. Uso wake uliokuwa na ndevu ndefu nyeupe, ulikuwa mwekundu kwa ghadhabu. Macho yake yenye mboni za rangi ya bluu yalikuwa yakimeta kama kaa la moto.

“Mtakufa nyote!” alituambia kwa hasira kabla ya kumdaka polisi mmoja.
“Jamani jini mwenyewe ndiye huyo!” nikapiga kelele kuwaambia wenzangu.
Faiza alining’ang’ania kiasi kwamba nilishindwa kukimbia.
“Faiza niache!” Nikamwambia Faiza huku nikiichomoa mikono yake iliyokuwa imenishika.

“Niachie, tutakufa sote hapa hapa,” nikaendelea kumwambia.
Wenzetu walikuwa wametawanyika ovyo kwa kutaharuki. Polisi aliyekuwa amebaki alimuelekezea bunduki Kaikush akampiga risasi mbili. Alikuwa kama anapiga mti.

Kaikush hakushtuka wala kutambua kuwa alikuwa amepigwa risasi yule polisi aliendelea kuishikilia bunduki yake akamfyatulia risasi ingine. Niliona kama imempata kifuani lakini mara baada ya kuingia lile tundu lilijiziba wakati uleule ikawa kama vile hapakutobolewa.

Hali hiyo ilinitisha sana naye kwa kuwa bunduki zao za kivita SMG hubeba risasi nyingi kwenye kihifadhi risasi yaani magazini alikoki tena bunduki yake na kumfyatulia risasi kama kumi hivi sehemu mbalimbali za mwili wake lakini alikuwa anatoboka mwili lakini baada ya sekunde tano, pale palipotobolewa panaziba na wala alikuwa hatoki hata tone kidogo la damu.

Baadaye aliamua kuweka ‘basti’ kwenye bunduki na zikamiminika risasi nyingi ambazo zilimuingia Kaikush na zikafanya tundu kubwa kifuani lakini kama ilivyo ada baada ya sekunde chache tundu lile liliziba naye akawa anatabasamu, yaani zile risasi zilikuwa kama vile zilikuwa zikimtekenya.

Aliendelea kumshikilia yule polisi aliyemdaka ambaye naye alikuwa akiminyana ili aachiwe.

“Faiza niachie tukimbie,” nilimwambia Faiza.
Faiza akauacha mwili wangu na kunishika mkono. Sisi ndiyo tulikuwa wa kwanza kukimbia.

Wale wenzetu walipoona tunakimbia na pia walipoona risasi mbili alizopigwa Kaikush hazikumuathiri, nao wakatimua mbio.
Huku nyuma yule polisi aliyeshikwa alikuwa ameshatiwa meno akifyonzwa damu.
Tuliisikia sauti yake ikilalamika.

“Jamani nakufa!”
Baada ya hapo hatukumsikia tena. Tukaendelea kukimbia, mimi na Faiza tukiwa mbele ya wenzetu.

“Kumbe jini mwenyewe ndiye yule!” Tulimsikia yule polisi aliyebaki akisema nyuma yetu.
“Ndiye yule. Ni katili na muuaji na anafyonza damu na kula ubongo,” nilimjibu mimi.
“Nilimpiga risasi mbili lakini hakuathirika hata kidogo.”
“Yule ni jini, risasi haziwezi kumuingia,” nikamwambia.

“Mimi nilikuwa siamini lakini sasa nimeamini,” akasema mtu mwingine.
“Jamani tukimbieni tuache kuzungumza linaweza kutufuata tena.” Ilikuwa sauti ya mmoja wa wenzetu waliokuwa nyuma.

“Kwani bado ni mbali sana?” Faiza akauliza.
“Bado tuna mwendo mrefu,” mtu mmoja aliye nyuma yetu akamjibu.
“Kama ni hivyo basi tutakwisha. Hapa nilipo nimekwishachoka.”
“Nitakubeba kama mwanzo,” nikamwambia.

Tulikuwa tumepunguza mwendo, wenzetu wakatupita. Tukasimama.
“Jamani tusubirini nimbebe Faiza.”
Wenzetu wakasimama.

Nikambeba Faiza na kumuweka kwenye bega langu. Kusema kweli sikuona uzito wake. Sikujua ni kwa sababu alikuwa mwanamke au mwenyewe tu hakuwa na uzito mkubwa.
Nikaanza kukimbia naye.

Mwendo haukuwa wa kasi kama wa mwanzo na tulikuwa tuko nyuma ya wenzetu. Jambo hilo lilinikera. Hofu yangu ni kuwa tukiwa nyuma Kaikush akitokea kwa nyuma atatushika sisi.

Nilitamani nijitahidi niwe mbele lakini nilishindwa.
Kukimbia huku umebeba mtu haikuwa sawa na kukimbia ukiwa peke yako.
Hatimaye na mimi nilianza kuchoka. Nikawa nahema kama chura.

“Jamani tupumzikeni kidogo,” nikawaambia wenzangu. Nilirudia kuwaambia hivyo mara mbili ndipo wenzangu waliposimama.
Nikamshusha Faiza.

“Sasa tembea kwa miguu yako,” nikamwambia.
“Hatuwezi kupumzika kidogo,” Faiza akauliza alipoona nilivyokuwa nikitweta.
“Hapapumzikiki dada’ngu. Bora tujitahidi hivyo hivyo,” mtu mmoja akamwambia Faiza.
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye gazeti hilihili Jumanne ijayo.

Comments are closed.