The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu- -37

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Mara simu ikaita tena.
“Ni Inspekta tena…Haloo!”
“Sasa wako wawili, mmoja tumpeleke ya serikali na huyu wenu tumpeleke huko Malamulo Hospitali?” alihoji.

“Hapana, wote tuwapeleke Hospitali ya Malamulo, tusifanye ubaguzi ni dhambi kwa Mungu,” akajibu Bwana Makang’ako.
Je, nini kitaendelea?
SONGA NAYO…

“Sawa,” alisikika Kamanda Inspekta Ben Mtwanga.

Msafara wetu ulikwenda moja kwa moja katika Hospitali ya Misheni ya Malamulo.
Mara baada ya kufika katika hospitali hiyo, haraka sana manesi walilizunguka gari la polisi huku wakiwa na vitanda vyenye magurudumu vya wagonjwa.
“Wabebeni walazeni kitandani,” aliamuru inspekta.

Haraka haraka walianza kumbeba kaka yangu Edgar na wakamaliza kumbeba yule mwanaume mwingine. Nesi mmoja alitaka kumshusha yule mwanamke aliyemfanya kaka yangu zezeta akidhani naye ni mgonjwa.
“Hapana, huyo siyo mgonjwa,” alisema kamanda.

“Hee, mbona kama mgonjwa,” akadakia nesi.
“Ni mtuhumiwa huyo,” akasema Kamanda Ben. Nilichogundua ni kwamba askari msemaji wao popote pale huwa ni kiongozi wao, wengine huzungumza wakiambiwa wafanye hivyo na kamanda wao ndiyo maana hata katika msafara huu yeye Kamanda Ben Mtwanga ndiye anayezungumza, wengine hujibu au kusema jambo akiwauliza.
“Umesema huyu mtuhumiwa, kafanya nini?”

“Wewe nesi mbona una maswali mengi kama mwandishi wa habari? Pokea wagonjwa hao wawili, huyu nimekuambia ni mtuhumiwa. Unataka kujua kafanya nini ili iweje?” alifoka kamanda. Kuona hivyo yule nesi aliachana na yule mwanamke mkatili na kwenda kwa wagonjwa waliokuwa wakipelekwa ndani ya hospitali.

Wagonjwa walifikishwa mapokezi na nesi aliyekuwa pale akaanza kunihoji mimi kwa kuwa nilikuwa mstari wa mbele.

“Huyu mgonjwa anaitwa nani?” alihoji akiwa karibu na kitanda alicholala kaka yangu. Mwenyewe alikuwa hajui kinachoendelea kutokana na kufanywa zezeta na yule mwanamke aliyekuwa akiishi naye tuliyemuacha kwenye gari la polisi akiwa chini ya ulinzi.

“Huyu anaitwa Edgar Ugonile.” Akaandika kwenye kadi.
“Ni Mmalawi?”
“Hapana ni Mtanzania.”
“Ana miaka mingapi?”

“Miaka arobaini na sita,” alikuwa akihoji na kuandika.
Maswali hayo aliniuliza pia kwa mgonjwa mwingine nami nilimjulisha nesi yule kuwa jina lake silifahamu kwa kuwa tulikuwakuta wote kwenye chumba kimoja wakiwa katika hali hiyo.

“Nani anaweza kujua jina lake kwa sababu hatuwezi kumpeleka kwa daktari bila jina kujulikana.”

Baada ya kusikia hivyo askari aliyekuwa pamoja nami alisema anatoka nje kwenda kumuuliza jina la huyo mgonjwa yule mwanamke aliyekuwa chini ya ulinzi garini.
Hakuchukua muda mrefu alirudi.

“Anaitwa Banda Babali,” akamuandikia kadi lake, kisha nesi mwingine akaburuza kitanda cha kaka na mwingine akasukuma kitanda cha Banda hadi kwa daktari.

Tulipoingia tu chumbani daktari alishtuka na kuuliza wagonjwa hao wamepatwa na nini hasa baada ya kumuona kaka Edgar akiwa anatokwa udenda mfululizo na wakiwa hawana akili, wamekuwa mazezeta.

“Wanasumbuliwa na nini?”
“Ni mazezeta, wamefanywa mazezeta.”
“Ilikuwaje?
“Hatujui.”

Daktari alikwenda kwenye kabati lake na kutoa glovu mbili, akavaa kila mkono kisha kuwarudia wagonjwa.
Alianza kumchunguza kaka kwa kumfunua kinywani, sikujua anaangalia nini. Wakati anafanya uchunguzi huo mkono mmoja alikuwa ameshika tochi ndogo iliyokuwa ikiwaka.

Baadaye alichukua ‘kipima mapigo ya moyo’ akampima kaka.
Aliulizwa maswali mengi ambayo sikusita kumjibu japokuwa mengine yalikuwa siyo majibu sahihi kwa kuwa yalikuwa maswali ambayo yalipaswa kujibiwa na yeye mwenyewe kaka.

Maswali kama alianza lini kutokwa na udenga au ilikuwaje hali ikawa hivyo, hakukuwa na mtu aliyejua na baada ya kumfahamisha daktari nini kilitokea alifahamu kuwa tatizo hilo ni zito na hakuwa tena na haja ya kunihojihoji.

Baadaye alimgeukia mgonjwa mwingine, yaani Banda, hata hivyo, hakuchukua muda mrefu kumchunguza kwani alijua kuwa matatizo yake ni sawasawa na ya kaka yangu.
“Huyu ana nafuu, lakini huyu mwingine ana hali mbaya. Hawa ni ndugu zako?” aliniuliza.

“Huyu mmoja ambaye nimejibu maswali yake mengi ndiye ndugu yangu wa damu. Ni kaka yangu, tumezaliwa baba mmoja na mama mmoja. Huyu mwingine simjui kabisa.”
“Lakini nesi aliniambia kuwa wote hawa wanalipiwa na mtu mmoja, nikadhani ni wewe.”

“Hapana. Tuna ndugu yetu hapo nje, anaitwa Bwana Makang’ako ndiye atakayelipa bili za wote wawili.”

“Ahaa, Bwana Makang’ako namjua, si yule Mtanzania anayependa kufuga ndevu?”
“Ndiyo. Ndiye aliyeshauri wagonjwa hawa tuwalete hapa Hospitali ya Malamulo kwa madai kuwa kuna madaktari makini.”
“Hajasema kuwa kuna daktari anayemfahamu?”
“Hajaniambia.”

ata kabla hatujamaliza mazungumzo tulishtukia Bwana Makang’ako akiingia katika chumba cha daktari.

“Dokta Pius Namahonga, Habari za siku nyingi?”
“Nzuri Bwana Makang’ako, hatuonani na tupo mji mmoja?”
“Bwana pilikapilika ni nyingi. Hawa ni wagonjwa wangu, nimewaleta hapa kutokana na kufahamu umahiri wako. Nilikuwa hapo nje nikiuliza kama upo au la, nikaambiwa na nesi mmoja kwamba upo na unawashughulikia wagonjwa wangu.”

“Si ungenipigia simu kujua hayo hata kabla hamjafika?”
“Simu yangu laini yake ni mpya, simu ya mwanzo niliibiwa na laini yake, kwa hiyo namba za simu za watu wangu wengi muhimu ukiwemo na wewe zilipotea.”
“Dah pole sana.”

“Huyu mgonjwa mmoja ni kaka wa huyu aliyeingia naye, anaitwa Jerome, tumefanya mengi mpaka kufikia hapa ofisini kwako, huyu mwingine simfahamu lakini nimeamua atibiwe hapahapa kwa gharama zangu, ndiyo ubinadamu.

Jerome, huyu ni Dokta Pius Namahonga ni mwenyeji wa nyumbani Tanzania isipokuwa alichukuliwa na hospitali hii ya misheni baada ya kusifiwa sana kule nyumbani.
Usikose kusoma muendelezo wa simulizi hii wiki ijayo.

Comments are closed.