Michuano ya Mapinduzi Inapoteza Mvuto Wake

MICHUANO ya Mapinduzi inaelekea ukingoni wikiendi hii. Ni mashindano ya muda mfupi ambayo katika miaka ya nyuma ilikuwa na mvuto mkubwa na ushindani wa klabu za Bara na Visiwani.

 

Kutokana na maendeleo ya teknolojia katika miaka ya hivi karibuni michuano hiyo ilianza kuhusisha timu alikwa kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

 

Lengo lilikuwa ni kujaribu kuongeza mvuto na msisimko zaidi pamoja na kuziandaa klabu zetu kwa michuano ya kimataifa. Lakini kadri siku zinavyokwenda mashindano hayo ya mapinduzi yameonekana kupoteza mvuto na uhalisia wake.

 

Imefika hatua timu mahiri za Zanzibar zinashindwa kushiriki na hata zikishiriki ushiriki wake unakuwa wa kawaida sana tofauti na siku za nyuma. Kikubwa kinachotajwa ni hali mbaya ya kiuchumi miongoni mwa timu hizo kiasi cha kushindwa kuwa katika utimamu unaostahili.

Lakini si hizo tu hata Simba na Yanga ambazo zilikuwa zikiongeza ushindani kwenye michuano hiyo na zenyewe zimeipuuzia.

 

Zinakwenda tu kutimiza wajibu na kuogopa kugombana na mamlaka. Lakini tunadhani kwamba kuna haja ya waandaaji kuacha kuandaa mashindano hayo kisiasa au kutimiza wajibu. Wakae chini na wadau mbalimbali waangalie jinsi ya kuiboresha michuano hiyo na kuongeza msisimko.

 

Hiyo inaweza kufanyika kwa kushirikisha wadau mbalimbali nakujua ni nini mahitaji ya wakati huu kwa klabu na wadau na ni utaratibu gani mzuri zaidi wa uendeshaji ambao unaweza kutumika ukaongeza mvuto zaidi na hata klabu zikashiriki.

 

Waandaaji wakifanya tu kwa lengo la kutimiza wajibu itafika sehemu hata huu mvuto wa mbali uliopo kwa sasa hautakuwepo kabisa, kuna haja ya kukaa chini na kuumiza vichwa kupata njia nzuri ya kuchangamsha hayo mashindano.

 

Waandaaji wasikariri mifumo ya kizamani, gharama za uendeshaji kwenye klabu hizi kwasasa imekuwa juu sana lazima waangalie namna nzuri ya kuzihamasisha timu zenyewe zipate mzuka mkubwa wa kushiriki lakini vilevile hata wahusika ambao ni wachezaji na wenyewe wahamasike.

 

Zawadi lazima ziboreshwe kwenye nafasi zote ili kuongeza morali kwa timu, zawadi zikiwa kubwa hata kama ni mashindano ya wiki moja yatakuwa na mvuto mkubwa zaidi ya ilivyo sasa.

 

Na vilevile wanaweza kukubaliana wakabadili mfumo wa uendeshaji yakawa yanachezwa Bara na Visiwani, fainali zikachezwa Visiwani. Ni namna mbalimbali tu ambazo zinaweza kufanya mashindano yakawa na mvuto zaidi na haya yote yanawezekana kama wadau wakikaa pamoja na kujadiliana juu ya maboresho yake.

 

Tunaamini kwamba mashindano hayo ni makongwe na muhimu sana kwa maendeleo ya soka na muungano wa pande zote mbili, hivyo yanahitaji kuendeshwa kwa namna bora zaidi kuanzia mwakani.

 

Lazima ifike mahali tukubaliane kwamba hakuna kizuri bila gharama,ni muhimu waandaaji kuongeza fedha ili kufanya kitu kizuri chenye mvuto wa kimapinduzi.

 

Kwa hili ambalo limejitokeza mwaka huu ni somo kwa waandaaji hasa kutokana na ukweli kwamba kuna timu ambazo hazikushiriki kabisa licha ya kualikwa. Sababu kubwa ilikuwa ni mpangilio wa ratiba hivyo kuna umuhimu ya kutazama upya namna ya kuweza kupanga ratiba mapema.

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment