The House of Favourite Newspapers

MJAMZITO AWALAANI MADAKTARI AKIKATA ROHO!

DAR ES SALAAM: Binadamu anapofariki dunia akiwa na kinyongo na mtu huku akimwachia maneno yamtakiayo mabaya, wahenga waliita hali hiyo kuwa ni marehemu kuacha laana.

Huwenda ikawa hivyo kwa Grace Kalinga mjamzito ambaye mashuda wa tukio la kifo chake waliliambia Amani kuwa alikata roho akiwalaumu vilivyo madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Palestina iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam kwa kile alichodai ni kuzembea kumhudumia.

Ijumaa Juni 8, Grace alifikishwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kujifungua, lakini haikuwa hivyo alichotaraji hakukipata bali mapenzi ya Mungu yalitimia kwake na kichanga chake kufia tumboni.

 

HIVI NDIVYO ILIVYOANZA

Akizungumza na Amani kwa masikitiko makubwa huku akilia kwa uchungu, mdogo wa marehemu, Aneth Kalinga alisema kuwa dada yake alifariki katika mazingira tatanishi.

“Siku ya Ijumaa nilikuwa kazini, Aunty akanipigia simu akaniambia niende nyumbani dada anaumwa,nikaenda pale nikamkuta kweli anaumwa uchungu.

“Akaniambia kuna kitu kimembana kifuani halafu kiuno kinamuuma, basi nikamuandalia nguo nikamwambia twende Hospitali ya Palestina,” alisema mdogo wa marehemu.

 

AENDELEA

Hakuishia hapo Amani liliendelea kumpa nafasi mdogo huyo kueleza hali ilivyokuwa ambapo aliendelea hivi:

“Tulipofika hospitali tukaenda mapokezi wakaniambia mimi nisubiri pale mgonjwa aingie na akishapimwa njia kama imefunguka atakuja kuniambia.

“Tulikaa kuanzia saa tatu usiku hadi saa nne ndio mgonjwa akashuka akatuambia ameambiwa abaki njia imeshafunguka, basi sisi tukaondoka.”

 

NINI KILIFUATA?

Inaonekana kama stori imeishia hapo lakini ukweli si hivyo kwa sababu hata ndugu walipoondoka Amani lilipata chanzo kingine ambacho kilisimulia kuwa hali ya Grace kwa usiku mzima ilikuwa ya matumaini.

“Mgonjwa alilala vizuri alikuwa anaongea na alionekana hana tatizo lolote,” chanzo kutoka ndani ya hospitali kililiambia Amani kwa masharti ya kutotajwa jina.

 

ANETH AMERUDI TENA

“Tuliporudi asubuhi ya Jumamosi tulimkuta na hali ileile, tukaondoka ilipofika mchana mgonjwa alinipigia simu akaniambia kuna dawa inahitajika na yeye hakuwa na pesa.“Nikampa mdogo wangu mwingine anayeitwa Luth elfu ishirini, dawa ikanunuliwa, lakini dawa zote pamoja na dripu hakuwekewa kwa sababu wauguzi walisema mpaka awekewe kidonge cha uchungu.”

Aliongeza kuwa kwa siku ya kwanza na hiyo ya pili walindelea kuwa na imani na madaktari lakini walishangazwa zaidi waliporejea asubuhi ya Jumapili na kuambiwa kuwa Grace alikuwa amefariki.

 

USIKU WA JUMAMOSI ULIKUWAJE?

Mjamzito mmoja aliyekuwa amelala kitanda cha karibu na marehemu Grace aliliambia Amani kuwa hali ya mgonjwa ilibadilika baada ya manesi kumuwekea kidonge cha kuchachua uchungu.

“Alipomuwekea kile kidonge ndiyo hali ikabadilika akaanza kulalamika uchungu na kuna wakati aliomba huduma za usaidizi lakini si unajua manesi wetu nao hawakuonesha kujali sana,“Ulipofika usiku alizidi kulalamika, wengi tukawa tunamuonea huruma lakini kwa kuwa kila mtu alikuwepo hospitali kwa majanga yake tukashindwa cha kumsaidia.

 

GRACE APIGANIA UHAI WAKE

Shuhuda huyo alisema kuwa Grace alipoona hali inazidi kuwa mbaya alianza kulalamika akisema madaktati wanamuacha afe na mtoto wake.

“Mimi sikujua kuwa alikuwa anakufa nilidhani ni hali ya kuwewesekea uchungu tu, kumbe haikuwa hivyo.“Kuna wakati alikuwa akishika simu yake sijui alitaka kumpigia nani lakini alishindwa, akawa anasema mnaniacha nife, Mungu anawaona.

“Karibu dakika ishirini alikuwa anasema maneno ya kuwalaumu madaktari na manesi na wauguzi, wakati mwingine alikuwa akimwita mama yake na mdogo wake.“Basi taratibu sauti ikawa inapungua, mara nikaona anakoroma nikajua anakufa kweli, niliogopa sana.”chanzo kilisema.

 

MUME WA GRACE AMWAGA CHOZI

Siku ya Jumapili haikuwa njema kwa mume wa Grace ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini kwa kile alichodai kuwa ni masharti ya kazi yake (hakuitaja pia) hasa mara baada ya kuambiwa kuwa mkewe amefariki.

“Madaktari waliniambia kuwa mke wangu ana presha ya kushuka, ila njia ya uzazi ilikuwa imefunguka. “Baadaye waliniambia inahitajika dawa ambayo walisema inauzwa shilingi elfu arobaini, nikatoa hiyo ilikuwa jana Jumamosi.

“Nakuja leo naambiwa mke wangu amefariki, siambiwi kilitochotokea, naumia sana, naumia sana kwa kweli,” alisema mume wa marehemu Grace huku akimwaga chozi.

 

MJAMZITO ATOROKA PALESTINA

Chanzo chetu ambacho kilikuwa karibu na kitanda cha Grace alirejea na tukio jipya baada ya kuliambia Amani kuwa mara baada ya mjamzito mwenzake huyo kufariki, aliamua kuondoka hospitalini hapo.

“Nilikumbuka tulivyokuwa tunaongea naye alipokuwa hai, alivyoniambia jinsi huduma mbovu zinavyosababisha wajawazito kufariki, halafu kweli ikatokea niliogopa sana. “Nilimpigia simu mume wangu nikamweleza kuhusu hilo tukio, nikamwambia siwezi kuendelea kuwepo Palestina tena.

“Ikabidi tutoroke hospitalini hapo tukaenda hospitali ya (anaitaja jina) kwa ajili ya kupata huduma, kusema kweli pale kuna uzembe ambao ni lazima ufanyiwe kazi vinginevyo wajawazito wataendelea kupoteza maisha.”

 

AMANI LATINGA PALESTINA

Mara baada ya kukusanya tuhuma hizo za uzembe wa huduma, Amani lilifunga safari kuwatafuta viongozi wa Palestina lau waseme kitu cha ufafanuzi, ambapo lilimpata Mganga Mkuu Dr. Chrispin Kayola ambapo baada ya kuelezwa mengi kuhusu kifo cha Grace alisema:

“Siwezi kuzungumzia chochote kuhusu swali lako utaratibu wetu hauruhusu, nenda kwa mkurungezi wa manispaa ya Ubungo akiniruhusu nitakuambia kilichotokea.”

 

AMANI LAFIKA UBUNGO

Siku ya pili, Amani lilifika ndani ya Manispaa ya Ubungo na kukuta mkurugenzi yupo likizo ambapo mmoja kati ya watumishi wa manispaa hiyo alielekeza atafutwe mganga mkuu wa wilaya. Baada ya maelekezo hayo Amani lilifanikiwa kuonana na Daktari wa Wilaya, Dk. Mariamu Maliwa ambapo alikiri kupokea malalamiko hayo lakini akaongeza haya:

“Ni kwamba kifo cha mjamzito yeyote kikitokea na kikawa na utata huwa tunaunda timu ambayo itachunguza na kuweza kugundua tatizo. “Tunafanya hivi kwa sababu ya kuchukua hatua zinazostahili ili matukio hayo yasijirudie na wakati mwingine kuwatendea haki walalamikaji na wanaolalamikiwa.”

 

TURUDI KWA SHANGAZI WA GRACE

Aidha, shangazi wa Grace alisema: “Yamefanyika mambo ya ajabu sana kwa mgonjwa wetu, alikuwa hasikilizwi wala kupewa huduma za msingi. “We fikiria hata nyaraka za matibabu na kifo cha Grace nazo ni kama za kufoji, nimekataa kuzisaini, wanifukuza.

“Lakini nitasaini vipi nyaraka ambazo naona hazina mihuri na kuna mambo yameandikwa ndivyo sivyo, mimi naomba tena namuomba sana Mkuu wa Mkoa Paul Makonda atusaidie sisi wanafamilia kupata haki. “Hata mwili wa marehemu tulipoufikisha Mwananyamala Hospitali kuna nyaraka walizikataa, kazi ya kutenganisha mwili wa mama na mtoto nayo imefanyika lakini kwa vikwazo vingi,” alisema shangazi huyo ambaye naye hakutaka jina lake liandikwe.

 

Mbali na kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar, Makonda ambaye wamesema wamamwamini kwa utendaji wake, ndugu wa Grace wamesema wako tayari kulifikisha suala lao ngazi za juu zaidi.

Mwili wa marehemu Grace na kichanga chake uliagwa katika Hospitali ya Mwananyamala, Juni 11 na kusafirishwa kuelekea Mufindi mkoani Iringa.

Waandishi: Neema Adrian na Shamuma Awadhi.

Comments are closed.