The House of Favourite Newspapers

Mjeda, Kibinti Wanaswa Wakifanya Mchezo Hatari Usiku

HII ni aibu kubwa! Joseph Mbega ambaye amedaiwa kujifanya ni mwanajeshi (mjeda) pamoja na mrembo aliyefahamika kwa jina la Rebeca Arcadi wamejikuta wakipata aibu kubwa baada ya kunaswa wakifanya mchezo hatari wa utapeli.

Tukio hilo lililonaswa na makachero wa Oparesheni Fichua Maovu (OFM) lilitokea hivi karibuni majira ya usiku, maeneo ya Sinza Mori jijini Dar. Shuhuda wa tukio alimpigia simu kamanda wa OFM ambaye aliwasha bodaboda fasta na kufika eneo la tukio.

“Njooni hapa Sinza-Mori, kuna dada mmoja alikuwa anataka kufanya tukio la hatari sana la kutapeli kwa njia ya mtandao sasa amedakwa alipokuwa anataka kutoweka,” shuhuda wa tukio hilo alimueleza kachero wa OFM.

 

KWA NINI NI HATARI?

Shuhuda huyo alimueleza kachero wetu kuwa, kitendo cha dada huyo kufanya tukio hilo ni cha hatari kwa sababu tayari wenzake wengine wameshafanya matukio hayo na kujikuta wakichezea kichapo na kupata aibu.

“We juzijuzi tu hapa kuna dada alifanya mchezo huu, akapigwa kweli na kudhalilishwa. Leo hii pia kuna dada mwingine hapa karibu na Lachaz Pub, naye alijifanya anatuma shilingi laki tano, akaombwa akawa hana na akadakwa. Bahati nzuri yeye aliishia kuzomewa tu lakini pengine angeweza kupigwa na hata kuuawa,” alisema shuhuda huyo.

 

ENEO LA TUKIO

Ndani ya dakika sifuri, makachero wawili wa OFM walifika eneo hilo na kulizingira duka ambalo Rebeca alikuwa akijaribu kufanya mchezo huo wa hatari ambao ungeweza kugharimu hata maisha yake.

OFM WAGAWANA MAJUKUMU

Wakati kachero mmoja wa OFM akiendelea kuchukua picha za tukio hilo, mwingine alikuwa akimhoji mmoja wa mashuhuda ambaye alilielezea mwanzo mwisho.

“Iko hivi blaza, huyu dada alikuja hapa katika hiki kibanda cha kutumia fedha za mitandao, akawa anazuga kuwa anataka kutuma shilingi laki saba kwa mtu. “Akamtajia namba, mhudumu akawa anaziweka zile namba katika simu yake wakati yeye akiwa bize kama vile mtu anayetoa fedha katika pochi yake.

 

“Kweli mhudumu akatuma zile fedha katika ile namba. Sasa alipoombwa fedha akawa kama anazugazuga kwa kuongea na simu nyingine.

“Mhudumu wa kibanda cha kutumia fedha akawa makini naye. Alipoona tu kama anataka kukimbia ndipo alipoomba msaada kwa watu kwa ajili ya kumtaiti,” alidai shuhuda huyo.

 

NAMBA HAIPATIKANI

Shuhuda huyo aliendelea kuwashibisha OFM ubuyu kuwa, mara tu baada ya dada huyo kushtukiwa, ile namba aliyoitaja ili iwekwe fedha ikawa haipatikani.

HUDUMA KWA WATEJA HOLA

Kama hiyo haitoshi, mhudumu wa kibanda hicho alipojaribu kupiga simu huduma kwa wateja, alijibiwa kuwa fedha hiyo tayari imeshatolewa ndani ‘dakika sifuri’ tangu itumwe.

“Yani hii michezo wanaicheza haraka sana, ile inatumwa tu kule katika ile namba aliyoitaja, fasta inatolewa hivyo hata ukipiga huduma kwa wateja ili uweze kuzuia, unaambiwa ishatolewa,” alidai shuhuda huyo.

 

AMUITA MJEDA FEKI

Baada ya kutaitiwa na kutakiwa ‘kuzitapika’ shilingi laki saba alizoamuru zitumwe katika namba ambayo haipatikani, Rebeca alidai kuwa kuna mtu angeweza kuja kumsaidia hivyo kuwaomba rai wenye hasira kali wasimdhuru.

Wakati macho ya watu yakisubiri kwa hamu kumuona huyo anayekuja kuokoa jahazi, huku tayari pia polisi wakiwa wameshaitwa eneo la tukio, ghafla alitokea jamaa mwenye rangi ya chungwa (Joseph) akiwa na gwanda zinazofanana na za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kutaka kumsaidia.

 

AUMBUKA

Alipobanwa maswali mawili matatu na polisi waliokuwa wamefika eneo hilo, mjeda huyo feki alijikuta akijikanganya na ndipo ilipobainika kuwa hakuwa mwanajeshi ‘orijino’ hivyo akatiwa ndani ya defenda pamoja na yule binti na wote wakapelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay.

Hadi OFM inaanua jamvi eneo hilo, ilishuhudia binti huyo na mjeda feki wakiunganishwa katika msala huo na kupelekwa polisi.

Hata hivyo, OFM ilifanikiwa kupata majalada ya washtakiwa hao ambapo Rebeca alishtakiwa kwa UTAPELI WA MTANDAO; RB/ OB/7872/2018 huku Joseph akishtakiwa kwa kosa la KUPATIKANA NA SARE ZA JESHI RB/OB/7880/2018.

 

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.