The House of Favourite Newspapers

Mjue Pauline Gekul Aliyetumbuliwa Uwaziri Akikabiliwa Na Tuhuma Nzito

0
Mbunge wa Babati Mjini mkoani Manyara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyekuwa Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Philipo Gekul.

Mbunge wa Babati Mjini mkoani Manyara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyekuwa Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Pauline Philipo Gekul amekuwa gumzo kubwa mno.
Hii ni baada ya kuwepo kwa madai ya udhalilishaji wa vijana wawili akiwatuhumu kwa imani za kishirikina na ushindani wa kibiashara.

Kufuatia tuhuma hizo, kulikuwa na shinikizo kubwa kwenye mitandao ya kijamii akitakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria na kuondolewa kwenye Baraza la Mawaziri.

Yote mawili yamefanyika; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan amemuondoa Gekul kwenye Baraza la Mawaziri kisha mbunge huyo amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Manyara kwa ajili ya upelelezi wa tuhuma zinazomkabili.

Kwa muhtasari tu ni kwamba sakata la Gekul lilianza baada ya kusambaa kwa video inayomuonesha kijana aliyetajwa kwa jina la Hashimu Ally akidai kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na kundi la vijana kwa maelekezo ya Gekul ambaye alikuwepo eneo la tukio.

Ally alidai Gekul aliamuru aingiziwe chupa sehemu ya haja kubwa au ampige risasi kwa madai alitumwa kimkakati kwenye Hoteli ya Paleii Lake View Garden inayodaiwa kumilikiwa na Gekul.

Mara tu baada ya kusambaa kwa video hiyo kwenye mitandao ya kijamii, wanasheria, watetezi wa haki za binadamu na wadau mbalimbali, walimtaka kiongozi huyo wa umma kuwajibika mara moja au mamlaka za juu kumchukulia hatua za kinidhamu ikiwemo kutengua uteuzi wake.

Taarifa ya ofisi ya Gekul ilidai kwamba imefuatilia kwa kina jambo hilo na kubaini Hashimu Ally alikuwa mtumishi wa Paleii Like View Garden na alikuwa akijitambulisha kwa jina la Jonathan, baada ya kuacha kazi eneo jingine (jina limehifadhiwa) linalodaiwa kuwa na ushindani wa kibiashara na Paleii Lake View Garden.

Kupitia video hiyo kijana huyo aliwaomba wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu kumsaidia apate haki yake, akidai Novemba 11, 2023 aliitwa na mwajiri wake kwenye chumba cha wageni maalum.
Alidai alimkuta Gekul akiwa na katibu wake na mtu mwingine ambaye hakumtaja na kijana mmoja aliyekuwa amepiga magoti hivyo naye alitakiwa apige magoti.

Kijana huyo anadai alishutumiwa kwamba aliweka dawa eneo la kazi na kuweka sumu kwenye chakula.
Alidai alikana ndipo akatajiwa jina la mtu aliyemtuma.
Hata hivyo, alidai aliendelea kukana na simu yake ilikaguliwa na hakuna kilichobainika.
Alidai walivuliwa nguo na kuingiziwa chupa, pia walitishiwa kuuawa kwa bastola.
“Aliita polisi wakaja kutuchukua tukakaa polisi siku nne tunahojiwa kuanzia saa mbili mpaka saa nane, siku ya tatu nikaitwa nikaulizwa tena ulitumwa nikakana nikarudishwa polisi,” alidai kijana huyo kwenye video hiyo.
Kijana huyo alieleza kuwa siku ya nne alitoa mawasiliano ya baba yake kwa ajili ya dhamana na alipotoka alichukua fomu ya polisi kwa ajili ya matibabu (PF3) kutokana na maumivu aliyopitia ndipo akaanza kuomba msaada wa kisheria.
Kufuatia sakata hilo wengi wamekuwa wakijiuliza Gekul ni nani?
Taarifa zilizokusanywa na GLOBAL TV zinaonesha Pauline Philipo Gekul amezaliwa siku ile ya Septemba 25 ya mwaka 1978.
Kati ya mwaka 1988 na 1994 Gekul alisoma Shule ya Msingi ya Dohom iliyopo Babati kisha alikwenda Shule ya Sekondari ya Dareda na baadaye Shule ya Sekondari Mkwawa.
Gekul alipata shahada yake ya kwanza ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2006 na Shahada ya pili; yaani masters alipata katika Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka 2014.
Gekul ni mwanasiasa Mtanzania na mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ila wakati fulani aliwika kwenye chama hasimu na CCM; yaani Chama cha Demokrasia na Maendelea (Chadema).
Baada ya kuhama Chadema, mwaka 2015 alirusha karata yake kwenye Jimbo la Babati Mjini kwa tiketi ya CCM ambapo aliibuka kidedea.
Gekul alirusha tena kete yake ya pili mwaka 2020 ambapo aliibuka tena kidedea na kuwa mbunge wa jimbo hilo hadi leo.

Leave A Reply