The House of Favourite Newspapers

MKE AGAWA MTOTO KWA BABA WAWILI!

Neema Lusaka na mumewe, Emmanuel Shimba pamoja na mtoto wao.

 

DAR ES SALAAM: Wanaume kaeni chonjo! Katika hali ya kushangaza, mwanamke mmoja ambaye ni mke wa mtu aliyejulikana kwa jina la Neema Lusaka, anadaiwa kugawa mtoto kwa wanaume wawili, hali iliyozua tafrani baina yao, Risasi Mchanganyiko lina mkanda kamili.

 

TUJIUNGE GLOBAL GROUP

Akisimulia kwa masikitiko ndani ya ofisi za gazeti hili zilizopo kwenye Jengo la Global Group maeneo ya Sinza-Mori jijini Dar, mume wa kwanza wa Neema aliyejitambulisha kwa jina la Emmanuel Shimba mkazi wa Mabibo alisema kuwa, aliishi na mkewe huyo yapata muda wa miaka mitatu.

Alisema kuwa, katika kuishi na Neema, Mungu si athumani kwani aliwajaliwa kupata mtoto mmoja wa kike kabla ya kutengana mwaka 2014 kwa madai ya kukosekana uaminifu kati yao, jambo ambalo ni sumu ya uhusiano wowote, uwe wa kimapenzi au wa kawaida.

 

Emmanuel Shimba akiwa katika chumba cha mahojiano cha Global Publishers.

 

NEEMA AONDOKA USIKU MNENE

Shimba aliendelea kusimulia kwamba, wakati Neema anaondoka nyumbani kwake usiku mnene, alikwenda kumchukua mtoto wao huyo kwa bibi yake maeneo ya Mabibo jijini Dar na kuondoka naye.

Alisema kuwa, tangu hapo Neema hakutaka Shimba amuone mwanaye huyo na hata alipofanya jitihada ili warudiane, mwanamke huyo alikataa katakata.

MWAKA 2014

“Mwaka 2014, nikiwa ninaishi na Neema, niliugua sana kama mara mbili hivi, nilikuwa nikisumbuliwa na malaria na kiharusi.

 

“Nikiwa kwenye hali hiyo, mke wangu alikuwa akiniacha nyumbani bila kunihudumia kwa chochote na kwenda zake kazini hadi ndugu zangu walipoingilia kati na kunichukua.

“Wakati ninachukuliwa na ndugu zangu niliondoka na mtoto maana alikuwa mdogo, nikaenda kukaa naye kwa wazazi wangu hivyo bibi yake akawa anamlea hadi Neema alipomchukua usiku wa manane.

“Baada ya kuniacha nyumbani, siku hiyo nilikwenda ghafla nyumbani kwangu yeye akiwa kazini nikiwa na ahueni, aliporudi saa sita usiku, nilimuuliza alikotoka ndipo akasema anaondoka.

Emmanuel Shimba na mwanaye.

 

“Nakumbuka, kweli alichukua nguo zake akaondoka. Kumbe alikwenda kwa mama yangu na kumchukua mtoto bila mimi kujua.

“Baada ya hapo, nilihangaika sana kwa ajili ya kumrudisha mke wangu tuendelee na maisha, lakini ilishindikana maana hata nikiwa ninahitaji kumuona mtoto wangu alikuwa akinikatalia katakata,” alisema Shimba.

 

Alisema kuwa, maisha yaliendelea huku akiwa hajamuona mwanaye kwa miaka mitatu ndipo mwaka huu akaamua kudodosa anaposoma ambapo alipapata na kubaini kwamba mwanaye amebadilishiwa jina na kupewa jina tofauti, yaani jina la baba mwingine ambaye ndiye huyo anayeishi na Neema kwa sasa.

 

ANASA ‘DOCUMENT’

Kutokana na hilo, Shimba aliwaomba walimu wakamsaidia ambapo aliweza kunasa ‘documents’ zilizoonesha kwamba mwanaye huyo mwenye umri wa miaka saba kwa sasa aliyekuwa anaitwa Brightnes Emmanuel Shimba, alikuwa anatambulika kwa jina la Queen Jackson.

 

“Mwanangu alizaliwa Hospitali ya Mwananyamala (Dar) mwaka 2011, lakini kwenye documents nilizozipata anazotumia kwa sasa na jina hilo lingine na baba mwingine, zinaonesha kwamba amezaliwa 2011 huko Iringa ambako ndiko nyumbani kwa wazazi wa Neema, jambo ambalo siyo kweli kwani sasa mwanangu ana vyeti viwili vya kuzaliwa vinavyoonesha baba tofauti.

Cheti kikiwa na majina mengine.

“Ukweli inaniuma sana, ninaomba kwa mtu yeyote anayejua sheria au mwanasheria, anisaidi licha ya kwamba sina hata uwezo wa kumlipa mwanasheria ndiyo maana nimekuja kwenu Watanzania wenzangu Kupitia Gazeti la Risasi Mchanganyiko mnisaidie nipate haki ya kumchukua mwanangu kwani inaniuma sana!

“Ninahitaji nikae na mwanangu, nimlee kwa sababu ni mwanangu kwa kuwa nilishapeleka hela na nguo za mtoto kwa mama yake anakofanyia kazi akazikataa,” alisema Shimba.

 

NEEMA ANASEMAJE?

Kama ilivyo desturi ya gazeti hili kuweka mzani wa habari, lilimtafuta Neema na kumuuliza kuhusiana na tuhuma hizo na sababu za kumkatalia mumewe kumuona mwanaye ambapo katika hali ya sintofahamu, alionekana kuwa na jazba.

Neema alidai kuwa, kuna vitu anamdai mwanaume huyo, lakini hakutaka kuvitekeleza.

 

“Kwanza alishakataa mtoto siyo wake na kuhusu kumbadilisha jina mwanangu siko tayari kueleza ila kikubwa ni kwamba alimkataa mtoto.

“Pia kuna haki zangu ninazomdai, siyo vyombo wala nguo, bali mwenyewe anajua ninachotaka ni kitu gani,” alisema Neema.

Hiki nacho majina tofauti.

 

 

SHAMBA AOMBA MSAADA

Katika kilio chake, Shimba alimalizia kwa kumuomba yeyote aliyeguswa na malalamiko yake na ana uwezo wa kumsaidia kisheria, awasiliane naye kwa namba 0719 509 919 kwani ameshatafuta ufumbuzi, lakini tatizo hilo halijapata ufumbuzi.

STORI: Gladness Mallya,, Risasi Mchanganyiko.

 

KWA HABARI NYINGINE KAMA HIZI UTAZIPATA KUPITIA APPLICATION YA GLOBAL PUBLISHERS.

Install

Android: ==>

iOS: ==>

Comments are closed.