The House of Favourite Newspapers

MKE MZURI, TAJIRI ILA LIMBUKENI WA MAPENZI WA KAZI GANI ?

U HALI gani mpenzi msomaji wangu wa safu hii. Karibu tena kwenye eneo lako hili la kujidai ambalo linayaweka sawa maisha yako ya kimapenzi.  Kabla ya kwenda kwenye kiini cha mada ya leo, kwanza niseme kwamba, raha ya ndoa ni kumpata mtu ambaye anajua maisha na anajua mapenzi pia. Ukipata mwanamke ambaye anajua kutafuta pesa tu lakini kwenye ulimwengu wa mapenzi ni limbukeni, atakusumbua sana.

Lakini pia ukijichanganya ukaoa mwanamke ambaye ni mtaalamu wa mapenzi asiyejua pesa inavyotafutwa, nalo ni tatizo licha ya kwamba kwa wengine si tatizo kwani wapo ambao hawataki kuoa wanawake wenye vipato kutokana na yale yanayosemwa kuwa, baadhi yao wakijua kutafuta pesa, wanakuwa na kiburi. Hata hivyo, kwa wanaume wanapofikia muda wa kuoa kila mmoja huwa na chaguo lake. Kila mtu atakuwa na vigezo vyake ambavyo vinaweza kutofautiana kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine.

Tofauti hiyo inakuja hata kwenye suala la tabia na uzuri. Kwa mfano, wapo ambao wanaangalia sana suala la tabia nzuri na muonekano mzuri pia. Lakini unaweza kushangaa mwanaume akatafuta mwanamke ambaye anakunywa pombe na anayependa kujirusha kwa kuwa na yeye ni mtu wa mambo hayo.

Aidha, wanaume wengine watakuambia hawataki kuoa wanawake wanaokunywa pombe, wanaoendekeza mambo ya anasa. Wanataka wanawake wa kutulia nyumbani, wanaomjua Mungu. Huo ni utofauti mdogo tu kwa baadhi ya wanaume wanapochagua wanawake wa kuingia nao kwenye ndoa.

Hata hivyo, hili suala la kutaka kuoa mwanamke mzuri huwa lina tofauti ya aina yake. Mwanamke ambaye wewe unaweza kuona umeng’oa kifaa, wenzako wanaweza kukuponda kuwa ni wa kawaida tu. Ukweli uko hivyo kwamba, kibaya kwako ni kizuri kwa mwenzio. Nigeukie sasa kwenye kile nilichodhamiria kukizungumzia leo. Ni kuhusu hasara ambazo mwanaume anaweza kuzipata endapo ataoa mwanamke mzuri kwa sura na umbo, mwenye pesa lakini limbukeni.

Hapa namaanisha kwamba, wapo ambao ni wazuri, waliokwenda shule, wenye kazi zao ila wanapoingia kwenye maisha ya ndoa, wanawaheshimu waume zao kupita maelezo. Yaani vipato vyao, elimu na mali zao havina thamani mbele ya mume. Ukibahatika kuoa mwanamke wa sampuli hii utayafurahia maisha. Lakini ukioa aliyejaaliwa vitu hivyo kisha akawa si muelewa wala hajui thamani ya mume na ndoa, andika maumivu. Kimsingi zipo hasara nyingi za kuoa mwanamke mwenye pesa, mzuri kwa muonekano, aliyesoma sana lakini akawa limbukeni.

JIANDAE KUSALITIWA

Wanawake wengi malimbukeni ambao wanajijua ni wazuri na wana pesa zao wakiudhiwa kidogo tu ni wepesi kuchepuka hata kwa kuwashawishi wanaume wengine kwa pesa. Utakuta mume kamkosea kidogo au kamkera bila kudhamiria lakini yeye anaona njia sahihi ni kutorudi nyumbani. Anaweza kwenda kulala hotelini mpaka pale mume atakapomfuata na kumpigia magoti. Wapo wanawake wa hivyo!

KUTAKA MUACHANE

Ukifuatilia sana wanawake wenye pesa, elimu na wazuri wanajiamini sana. Hawa ndiyo wanaoongoza kwa kuomba talaka. Kosa dogo tu, atakuambia muachane.

Anasema hivyo akijua wapo wanaume wengi wanaomsumbua na hatapungikiwa lolote. Tena hali inaweza kuwa mbaya sana kama wakati huo hamjajaaliwa mtoto kwani atajua hatakosa kitu akikuacha. Pesa anayo, ana uhakika wa kupata mwanaume mwingine fasta, kwa hiyo anaona hana cha kupoteza au kukikosa akikutosa.

USIPOANGALIA ATAKUTAWALA

Baadhi ya wanawake wenye pesa na wanajijua ni wazuri wanapenda sana kuonekana wao ndiyo wenye sauti ndani ya nyumba. Watakataa kuelekezwa wala kupewa amri na wanaume zao hata kwenye masuala ya msingi. Hawa ndiyo wale ambao wanataka kurudi nyumbani muda wowote wanaotaka na wasiulizwe. Watataka wawe wenye maamuzi ya mwisho na kila jambo la kifamilia washirikishwe la sivyo kinanuka. Hili ni tatizo!

Kimsingi ninachotaka kukifikisha kwa wanawake ni kwamba, ndoa ni heshima. Ukijaaliwa kupata mwanaume wa kukuingiza ndani, jitahidi kuithamini ndoa yako. Jua wapo wanawake wenye kila kitu lakini wamekosa wanaume wa kuwaoa na wanaitamani heshima ya ndoa.

 

Comments are closed.