The House of Favourite Newspapers

Mke Wangu Amenikimbia Baada ya Kuvunjika Kiuno, Kupasuliwa Kibofu

0

Stori: Na Makongoro Oging’,  UWAZI

Kulwa Maganga (37) mkazi wa Mbande, Mbagala jijini Dar amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jengo la Sewa Haji kutokana na majeraha aliyonayo baada ya kudondoka toka juu ya mti na kuvunjika kiuno.

Maganga akiwa katika hospitali hiyo Kitengo cha Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), alipohojiwa na safu hii anasema alipelekwa hospitalini hapo na wasamaria wema, Mei mwaka jana.

Anaongeza kuwa mbali na kuvunjika kiuno alipata tatizo lingine la haja ndogo kutotoka, hivyo alifanyiwa upasuaji katika kibofu lakini hata hivyo tatizo hilo halijakoma kwani bado anakojoa kwa shida.

Maganga anasema:

“Kinachoniumiza sana ni kuhusu watoto wangu ambao niliwaacha na bibi yao huko Kahama, Shinyanga huku wakiishi kwa shida kwani mama yao alishanitoroka na hajulikani alipo.

“Nilitoka nyumbani Mei mwaka jana kuja hapa Dar kutafuta kazi, nilifikia Mbande, nilienda kwa mwenyekiti wa mtaa angalau kama kuna kibarua nipatiwe, nilipatiwa kazi ya kumlindia mtu nyumba yake iliyokuwa ikiendelea kujengwa.

“Nilikuwa nalipwa fedha kidogo sana kwani nilikuwa naishi pale bure bila kulipa kodi.”

SIKU YA KUVUNJIKA KIUNO

“Siku moja nilipata kibarua cha kukata matawi ya mti, sikuwa na uzoefu wa kufanya kazi hiyo ya kupanda mitini, huku nikiendelea kukata matawi niliteleza na kudondoka chini nikashindwa kuinuka.

“Kila nilipojaribu kuinuka nilishindwa, nilipatwa na maumivu makali sana, ikagundulika nilivunjika kiuno.”

KUFIKISHWA MUHIMBILI

“Nililia kwa sauti na wasamaria wema walijitokeza na kunichukua hadi hapa Hospitali ya Muhimbili ambapo nilianza matibabu, baadaye kulitokea tatizo la kutotoka kwa mkojo kwa urahisi ambapo nilifanyiwa upasuaji lakini hata hivyo bado hali siyo nzuri kwani mkojo unaendelea kutoka kwa shida.

“Natembea kwa shida tena kwa kutumia magongo,wakati fulani nadondoka nayo chini kwa sababu sina uzoefu, hakuna mtu anayekuja kuniona, hata wale wasamaria wema walionileta hawajarudi tena.”

KAHAMA HAWANA TAARIFA

“Ndugu zangu huko Kahama hawana taarifa kuwa nimevunjika kiuno, nawaarifu nipo hapa hospitalini. Nawashukuru sana madaktari wanaonisaidia na wameniambia naweza kwenda nyumbani kwani nimepata nafuu.

“Sijui nitakwenda wapi, sina uwezo wa kifedha, nani atakayenipokea? Watoto wangu najua wanateseka, niliamini nikija hapa mjini ningepata kazi na kuwasaidia, sikujua kama nakuja kuishia hospitalini huku nikiteseka,” alisema Maganga kwa huzuni.

Kwa yeyote aliyeguswa na habari hii anaweza kumsaidia mgonjwa huyu kwa kupitia simu yake namba 0712 462514.

Leave A Reply