The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu 08

0

ILIPOISHIA…
BAADA ya kusikia jina lake linaitwa akiwa ndani ya gari la shule, Kevin aligeuza shingo kuangalia nyuma, akamwona Catarina! Msichana aliyempenda kupindukia, ambaye wazazi waliwatenganisha ili wasiendelee na upendo wao kwa kumpeleka kusoma nchini Uganda.

Uamuzi alioufikia Kevin ulikuwa ni wa kuruka kutoka kwenye gari likiwa katika mwendo mkali, akaangukia kichwa, damu zikamtoka puani, mdomoni na masikioni! Catarina alimfuata chini alipoanguka na kumkumbatia lakini baadaye watu wakamwondoa na Kevin kupakiwa garini ili apelekwe hospitali, alichobaki nacho Catarina ni begi la Kevin.

Akafuatilia hospitali ambako wazazi wa Kevin walimfukuza wakati mtoto wao anapelekwa chumba cha upasuaji, walionyesha chuki ya wazi, iliyomfanya Catarina ashindwe kubaki hospitalini na kuamua kwenda nyumbani ambako aliendelea kulia akisoma daftari la Kevin alilotunza kumbukumbu zake, akagundua kumbe kijana huyo alimpenda lakini alishindwa kufungua mdomo na kuweka wazi hisia zake.

Hii ilimuuma sana, baadaye wazazi wake walikuja na kumkuta akilia, kazi ya kumdadisi juu ya kilichokuwa kikimsumbua ikafanyika, Catarina akaweka wazi kila kitu.

Upande mwingine, baba yake Kevin anaondoka hospitali kwa kasi kubwa na wakati Catarina akiwa chumbani anazungumza na wazazi wake juu ya kilichompata Kevin, huko nje baba yake Kevin amejitokeza akiwa ameshikilia bastola mkononi, mfanyakazi anakimbia ndani kwa kasi kuwaita wazazi waone kinachotokea nje.
Je, nini kinaendelea?SONGA NAYO…

PAMOJA na kuambiwa kwamba baba yake Kevin, mzee Mdoe alikuwa nje ya nyumba akiwa na bastola, baba yake Catarina hakuogopa kwani hakuona kosa kubwa alilokuwa amefanya, akajitokeza mbele ya mlango akiwa amenyoosha mikono juu karibu kabisa na bastola ya Mzee Mdoe.

“Nini tena jirani? Mbona umekuja na silaha mkononi?”
“Nakuambia ukweli, mwanangu akifa, nitafanya kitu kibaya sana hapa kwako!”
“Kwa kosa gani jirani?”

“Mwanao amemsababishia mwanangu matatizo makubwa, hivi sasa yuko chumba cha wagonjwa mahututi!”

“Amekwishanieleza, lakini ndiyo uhamaki na kuchukua bastola jirani yangu? Nakusihi rudisha bastola yako kibindoni ili tuongee, sipuuzi kwamba mwanao anaumwa na Catarina ndiye aliyemfanya aruke kwenye gari, najua uchungu ulionao lakini ninakuomba urudishe silaha yako kibindoni ili tuongee.”

“Sina cha kuongea, nasema mwanangu apone!” aliongea mzee Mdoe na kuanza kuondoka kwa kasi kurejea nyumbani kwake.

Ilikuwa ni hali ya kutisha, hakuna aliyewahi kufikiria kwamba Mzee Mdoe ambaye siku zote alionekana ni mpole na mwenye hekima, angeweza kufanya jambo hilo ambalo lingetosha kabisa kuripotiwa polisi na kuchukuliwa hatua za kisheria kwani lilikuwa ni kosa kumtisha mtu na silaha.

Baba yake Catarina akielewa kabisa hali ambayo wazazi wa Kevin walikuwa nayo, aliona kwa hekima lisingekuwa jambo jema kwenda kumripoti mzee Mdoe polisi ili achukuliwe hatua za kisheria, hasa alipojiweka yeye katika nafasi ambayo alikuwa nayo, akamwonea huruma na kuamua kurejea ndani akiwa bado anatetemeka.

“Vipi?” mama yake Catarina alimuuliza.
“Hakuna tatizo,” akaficha.
“Nimesikia sauti ya mtu anafoka!”
“Ndiyo.”

“Ni nani?”
“Tutaongea.”
Hakutaka Catarina aelewe kilichokuwa kikiendelea, hivyo waliendelea kumbembeleza mpaka asubuhi bila kupata hata usingizi kidogo. Walipohamia chumbani kwao baada ya Catarina kutulia ndipo alimsimulia mke wake kilichotokea na maneno ambayo mzee Mdoe aliyasema, mama Catarina akaingiwa na hofu kubwa moyoni mwake.

“Hatuwezi tena kuishi hapa, mtoto wake akifa kweli anaweza hata kutuchomea ndani ya nyumba.”
“Hawezi.”

“Anaweza, usifanye mzaha, mtoto mwenyewe wanaye mmoja kama huyu wa kwetu na hawana uwezo wa kuzaa tena, hiyo hasira ya kufiwa ataipoza na nini?”
“Kwa hiyo?”

“Tutafute mahali pengine pa kuishi kwa muda, mtoto wao akipona tutarejea.”
Mzee Mdoe hakuwa na ubishi juu ya hilo, alichokifanya siku hiyo ni kuondoka kuelekea maeneo ya Mikocheni ambako alitafuta nyumba ya vyumba vitatu kwenye nyumba za kupangisha za Abla Apartments, akalipia nyumba hiyo kwa miezi mitatu na kwa sababu ilikuwa na kila kitu ndani, siku hiyo hiyo yeye, mke wake, Catarina na wafanyakazi wao wa ndani walihamia.

Pamoja na kuhama huko walikokwenda walibaki na kazi moja tu ya kuendelea kumbembeleza Catarina ambaye bado alimlilia Kevin, akitaka aelezwe kama alikuwa hai ama amekufa! Siku tatu baadaye alikuwa ametulia kidogo na wazazi wake wakaamua kurejea kazini, walipoondoka tu asubuhi hiyo, naye hakukaa hata dakika ishirini, akatoka na kutembea hadi stendi ya teksi.

“Muhimbili.”
“Shilingi elfu tano.”
“Sawa.”

Gari likaendeshwa na dereva huyo kupitia Barabara ya Old Bagamoyo hadi Morocco ambako waliingia Ali Hassan Mwinyi hadi Daraja la Salenda, hapo taa ziliporuhusu wakakata kulia kuingia Barabara ya Umoja wa Mataifa, mbele kama mita mia mbili walikata kulia tena kuingia Barabara ya Ali Khan hadi Muhimbili ambako Catarina alishuka na kuingia kwenye moja ya maduka yaliyojihusika na biashara ya kuuza kadi za salamu.

“Naweza kununua kadi hapa halafu mkaifunga vizuri kwa ajili ya mgonjwa?”
“Inawezakana.”
“Maua mnayo?”
“Tunayo.”
“Basi niuzieni.”

Akachagua kadi moja nzuri na maua ya kuvutia, kwenye kadi aliandika maneno ambayo hakutaka mtu yeyote ayaone, akafungiwa vizuri kisha kulipa na kuondoka na boksi lake hadi wodi ya wagonjwa mahututi. Saa yake ya mkononi ilisomeka saa tatu na nusu wakati wanasimama mbele ya jengo hilo, muda wa kuona wagonjwa ulishapita.

“Shikamoo sista,” akamwamkia muuguzi aliyetoka ndani ya wodi hiyo.
“Marahaba binti hujambo?”
“Sista nina shida.”
“Shida gani?”

“Naomba unisaidie, mimi ni sawa na mtoto wako au mjukuu wako!”
“Ndiyo.”
“Humo ndani kuna mgonjwa anayeitwa Kevin Mdoe?”
“Ndiyo.”
“Anaendeleaje?”
“Ni nani wako?”
“Rafiki yangu.”

“Bado, hana fahamu, ubongo wake umeumia!”
“Mungu wangu! Haongei?”
“Sijui kama atakuja kuongea!”
“Wazazi wake wapo?”
“Wamekwi-shaondoka.”

“Sista naomba unisaidie nimwone!”
“Muda wa kuona wagonjwa umepita lakini!”
“Nisaidie, nisaidie!” aliongea Catarina akionyesha huzuni na machozi yakimlengalenga.
“Hebu njoo,” Sista alisema, wakaingia ndani wote wawili ambako alimwamuru avue viatu na kuvaa vilivyokuwepo ambavyo hutumiwa na watu wanaoingia kuona wagonjwa.

Baada ya hapo alimpeleka moja kwa moja hadi kitandani kwa Kevin, Catarina alibubujikwa na machozi, Kevin alikuwa amelala kichwa kikiwa kimevimba mara mbili ya saizi ya kichwa chake cha kawaida huku kikiwa kimefungwa bendeji nyingi, hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa macho yake, pia yalikuwa yamevimba mno na haikuwa rahisi kumtambua.

“Kevin! Kevin! Kevin!” aliita huku akilia.
“Hawezi kukusikia.”

Catarina akaweka maua yake juu ya meza pamoja na boksi lenye kadi, kisha kupiga magoti chini na kuanza kusali akimwomba Mungu anusuru maisha ya mwanaume aliyempenda kuliko wengine wote, aliponyanyuka alifuta machozi na kumwangalia Sista.

“Ahsante Sista, Mungu akubariki sana, naomba tu ninapokuja uwe unaniruhusu nimwone na kumletea kadi na maua, waeleze wazazi wake wasifungue kadi hizi mpaka yeye mwenyewe na ninaomba usiwatajie jina langu, mimi naitwa Catarina, hawanipendi sababu nilisababisha ajali ya mtoto wao!”

“Aaah! Nimeshasikia wakikutaja, sitawaambia na nitawaeleza pia wauguzi wenzangu, pole sana mwanangu!”
“Ahsante!”

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

Leave A Reply