The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu -10

0

ILIPOISHIA…
Wakati furaha ilikuwa imeingia kwenye familia, baada ya matibabu ya mionzi na Catarina kurejewa na fahamu Kevin alipofika wodini kumwona, mambo yamebadilika kufuatia kipimo cha kipande cha Uboho kutoka kwenye mfupa wa Catarina kilipochukuliwa kwenda kuangaliwa kama dawa alizopewa zilikuwa zimefanikiwa kuziua chembechembe za Saratani.

Majibu yamekuja vibaya kwamba pamoja na dawa zote za mionzi alizopewa, chembechembe za Saratani bado zipo katika mwili wa Catarina, jopo la madaktari limeamua kufanya matibabu yaitwayo Bone Marrow Transplant au kifupi BMT.

Katika matibabu haya ambayo hutumika kutibu Saratani ya damu, uboho wa mtu asiye na Saratani ya damu huchukuliwa na kupandikizwa kitalaam kwenye mifupa ya mgonjwa, Uboho huo ndio huanza kutengeneza chembechembe za damu imara, kwa mujibu wa daktari matibabu haya hufanikiwa katika wagonjwa wengi.

Catarina analia, anahisi kukata tamaa, anapofikiria suala la kupandikiziwa Uboho kwenye mifupa yake kama tiba anaona ni jambo lisilowezekana, wazazi wake wamemtuliza mpaka alipofika Kevin na kupewa taarifa hizo, yeye amemwambia yuko tayari kutoa Uboho wake ili Catarina aponeJe, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

Majibu hayo yalirejesha hali ya Catarina nyuma kabisa, akadhoofika kupita kiasi, kumbe ugonjwa wa saratani ulikuwa na uhusiano mkubwa sana na saikolojia na mtu, aliyejisikia kudhoofishwa na ugonjwa huo kweli alidhoofika na aliyejisikia mshindi, imani yake ilimfanya kuwa mshindi. Ndani ya wiki mbili tu Catarina alishaongezewa damu nyingi mno na uwezo wake wa kuongea ulizidi kupungua, hata chakula hakutaka kula kabisa.

Wazazi wake walichanganyikiwa kabisa, lakini Kevin alichanganyikiwa zaidi, hakutaka kabisa Catarina afe! Alisababisha usumbufu mkubwa sana kwa madaktari akiwafutilia ili utaratibu wa kupimwa kama alikuwa na uwezo wa kutoa uboho wake ufanyike mara moja.

“Uko tayari?”
“Nipo tayari daktari.”
“Tatizo umri wako.”
“Una nini?”

“Wewe bado mdogo Kevin!”
“Hapana, ninatosha.”

“Sijui kama itawezekana kwako, nilimwambia baba yake na Catarina akusanye watu wa kutosha ili tuwafanyie vipimo, tayari mgonjwa alishapimwa na kuonekana ana kundi la damu O Chanya, watu wa kumpa Uboho ni lazima nao wawe na kundi hilo la damu na pia wapimwe vipimo vingine vingi, vikiwemo vya Ukimwi na Homa ya Ini!”

“Baba yake alisema atawaleta lini?”
“Leo.”
Siku hiyo hiyo mchana watu kumi na tano walijitolea kupimwa ili kuona kama wangeweza kutoa Uboho ili upandikizwe kwenye mifupa ya Catarina, hali yake ilizidi kuwa mbaya, majibu yao yalipotoka yalionyesha wote wakiwemo wazazi wa Catarina wasingeweza kumpa Catarina Uboho! Binti huyo alipopata hizo taarifa alilia.
“Mimi nimewaambia wanipime lakini wamekataa!” Kevin alilalamika.
“Wewe bado mdogo!”

“Labda niwaambia baba na mama yangu!”
“Tutashukuru.”

Jioni ya siku hiyo wazazi wake walipompitia kwa ajili ya kwenda nyumbani, Kevin aliwaketisha chini akaongea huku akibubujikwa na machozi kuwasihi wakubali kupimwa ili mwisho wa siku wampe Catarina Uboho kuokoa maisha yake, hawakuwa na kizuizi, walikubali mara moja.

“Chochote kitakachokufurahisha tuko tayari kufanya, tulishakupoteza mtoto wetu!”
“Baba nawaomba mumpe Catarina Uboho!”
“Tuko tayari, wakati wowote.”
Dk. Ngamila alipewa taarifa na akawachukua wazazi wote wawili hadi maabara ambako vipimo vyao vilichukuliwa, wao peke yao ndiyo walionekana kuwa tumaini la mwisho la Catarina ambaye tayari alishaanza kupoteza fahamu, dalili kwamba kama hatua zisingechukuliwa haraka angekufa, kufikiria jambo hilo tu kulimfanya Kevin alie kama mtoto mdogo akimwomba Mungu abadilishe msimamo wake.
Mkuki mkali zaidi moyoni ulikuwa ni pale majibu yalipotoka kuwa hata wazazi wake na Kevin wasingeweza kumpa Catarina Uboho, miili yao haikushabihiana naye! Kevin alichanganyikiwa kabisa na kuanza kuwafuata madaktari akitaka wampime yeye pia lakini walikataa kwa madai kuwa umri wake ulikuwa mdogo.
Wazazi wa Catarina baada ya matukio hayo waliamua kwenda kwenye vyombo vya habari kutafuta watu ambao wangekuwa tayari kumpa mtoto wao Uboho kwa malipo yoyote ambayo wangeyahitaji, waliojitokeza baadaye wengi wao damu hazikurandana! Hayo yakitokea hali ya Catarina ilizidi kudhoofika.
“Daktari!” Kevin alimwita Dk. Ngamila.
“Ndiyo.”
“Kwa nini mimi unanikatalia?”
“Umri wako.”
“Kama nimeridhia?”
“Huwezi kuridhia labda wazazi wako wafanye hivyo.”
“Madhara gani yanaweza kutokea?”
“Hakuna madhara makubwa sana, Uboho ukishautoa mwili wako utatengeneza mwingine tena!”
“Sasa tatizo lako ni nini daktari?”
“Mpaka wazazi wako wakubali kutia saini.”
“Hilo tu?”
“Ndiyo!”
“Nitaongea nao leo jioni wakija, kama wakikubali unaweza kunitolea Uboho leo?”
“Itakuwa kesho.”
“Wacha nisubiri waje, mimi kundi langu la damu nalifahamu.”
“Ni lipi?”
“O Chanya!”
“Kama Catarina! Basi itakuwa vizuri iwapo vipimo vingine vyote vitakuwa sawa.”
“Kwa nini msinipime kabisa? Kwani hata kupimwa ni lazima wazazi wangu waridhie?”
“Hapana!”
Kevin akapelekwa maabara ambako alipimwa vipimo vyote, majibu yalipotoka kila kitu kilikuwa kimerandana na Catarina, yeye peke yake ndiye alikuwa na uwezo wa kutoa Uboho wake kumpa binti huyo lakini kama wazazi wake wangetia saini! Akiwa na furaha alibaki akiwasubiri baba na mama yake wafike.
Je, nini kitaendelea? Wazazi wake watakubali? Fuatilia siku ya Jumatano katika gazeti la Championi Jumatano.

Leave A Reply