The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu – 11

0

Hali ya Catarina bado ni mbaya na amelazwa katika hospitali ya Saratani ya Ocean Road, Jopo la madaktari wakishirikiana na Dk. Ngamila wamefanya matibabu ya awali ya dawa ya mionzi kuona kama angeweza kupata nafuu lakini haikuwa hivyo, Dk. Ngamila analazimika kuwaita wazazi wake na kuwaeleza majibu ya mtoto wao akiwaeleza kwamba pamoja na matibabu ya awali bado vimelea vya Saratani vilikuwepo kwenye damu.

Ushauri pekee anaowaeleza ni kumpandikizia Catarina Uboho kutoka kwa mtu mwingine hivyo watafute watu ambao wangepimwa kuona kama angepatikana mtu ambaye angerandana naye. Mzee David na mkewe wanapimwa na majibu yanatoka tofauti, hivyo wanaamua kuwaomba ndugu, jamaa na marafiki nao pia wanapopimwa majibu yanatofuatiana na mgonjwa jambo linalozidi kuwachanganya kabisa akili zao.

Upande wa Kevin kwa penzi alilonalo kwa Catarina anajaribu kuwaomba wazazi wake wamsaidie binti huyo kwani asingependa kuona anakufa, mzee Mdoe na mkewe nao wanapimwa kuangalia kama damu zao zingerandana na Catarina. Majibu yanatoka kwamba hawakuwa na uwezo wakufanya hivyo, mkuki unachoma ndani ya moyo wa Kevin, haelewi ni nini afanye ili kuokoa maisha ya mpenzi wake huyo.

Akiwa katika mawazo hayo anaamua kuzungumza na daktari akimweleza kwamba yeye alikuwa tayari kufanya hivyo ili kuokoa maisha ya mwanamke aliyempenda, Dk. Ngamila anakubaliana naye na kumchukua Kevin na kumwingiza maabara kufanyiwa vipimo na majibu yanapotoka kila kitu kilirandana na Catarina, ni furaha kubwa kwa Kevin watu wawili tu wanasubiriwa ambao ni wazazi wake kutia saini.
Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

Vipimo kuonyesha kuwa Kevin alikuwa na uwezo wa kutoa Uboho wake na kuwekewa Catarina ili kuokoa maisha yake kutokana na saratani ya damu iliyokuwa ikimtesa, zilikuwa ni habari njema kwa kila aliyezisikia, wazazi wa Catarina walifurahi mno na waliamini kitendo hicho ndicho kingethibitisha upendo ambao kijana huyo alikuwa nao kwa mtoto wao.

Waliokuwa wakisubiriwa sasa ni wazazi wa Kevin kutia saini kwenye fomu kuruhusu utaratibu wa Uboho kutolewa uanze, kwa maelezo yake Kevin alisema wasingekuwa na kizuizi hata kidogo kwani walimpenda na walikuwa tayari kufanya lolote ili kumpa mtoto wao furaha.

Wote walibaki wakisubiri, macho kwenye saa ambayo siku hiyo mishale yake ilionekana kwenda taratibu kuliko siku nyingine zote. Ilivyokuwa wazazi wa Kevin walikuwa na utaratibu wa kumpitisha mtoto wao hospitali asubuhi kisha kwenda ofisini na kurejea jioni saa kumi na moja kumpitia, kila Kevin alipotupa macho yake kwenye saa, mshale ulikuwa haubanduki kwenye saa kumi.

“Au saa yangu imesimama?” alimuuliza baba yake na Catarina.
“Kwa nini?”
“Kila nikiangalia naona inaniambia ni saa kumi.”
“Una hamu sana wazazi wafike hapa ndiyo sababu, hivi sasa ni saa kumi na moja kasoro dakika kumi na saba.”
“Kweli!”

Ilipogonga saa kumi na moja na dakika ishirini bwana na bibi Mdoe walionekana wakiegesha gari nje ya wadi ya wanawake na kushuka, Kevin hakuweza kuvumilia kuwasubiri mpaka wafike, akanyanyuka na kuanza kuwakimbilia jambo ambalo kwa muda mrefu sana alikuwa hajalifanya, walipomwona waliduwaa na kupatwa na mshtuko.

“Shikamoo baba! Shikamoo mama!” aliamkia kwa mpigo.
“Marahaba, mwenzetu vipi mbona leo uko mbiombio?”
“Majibu yametoka!”
“Ya mtihani?”

“Hapana, nimepimwa vipimo vyote ikaonekana mimi peke yangu ndiye naweza kumpa Catarina Uboho!”
“Unasema?”

“Mimi peke yangu ndiye naweza kumpa Catarina Uboho wangu ili apone saratani ya damu inayotaka kumuua!”
“Halafu sisi?”
“Ninyi vipi baba?”
“Yeye apone sisi tubaki na mgonjwa?”
“Sio hivyo!”

“Haiwezekani, wewe ni mtoto mdogo sana kutoa Uboho wako!” Mama yake aliongea akionyesha kukerwa.
“Mama najua unanipenda sana, lakini nakuomba kwa mara ya kwanza maishani mwako, ruhusu niingie katika hatari hii ili nimwokoe mwanamke nimpendaye!”
“Mimi ni mwanamke pia mwanangu, nakupenda mno Kevin, sipo tayari kuona unatoa Uboho halafu unabaki mgonjwa!”

“Mama sio hivyo!” aliongea Kevin, safari hii akiwa amepiga magoti chini mbele ya wazazi wake, watu wote waliopita jirani na eneo hilo walimshangaa wengine walisimama na kumkodolea macho wakijiuliza kama kulikuwa na kosa alilofanya mpaka kuomba msamaha mbele ya wazazi wake.

“Hebu ingia kwenye gari!” ilikuwa ni sauti ya mzee Mdoe akiwa amehamaki kupindukia huku mlango wa gari ukiwa umefunguliwa.
“Twende wapi baba?”

“Umeongea pumba kabisa, tunakupenda mno hatuwezi kuruhusu utoe Uboho, kwani familia ya Catarina hawana ndugu mpaka utoe wewe?”
“Wote wamepimwa hakuna hata mmoja!”

“Uongo huo, ukoo gani mdogo kiasi hicho, kupima siku moja tu watu wote wamekwisha? Hebu ingia kwenye gari usiniudhi!”

Tayari machozi yalianzaa kumtoka Kevin, hakuwa na uwezo wa kubishana na wazazi wake ndivyo alivyolelewa akiambiwa uamuzi wa wazazi ulikuwa ni wa mwisho na kutishwa kwamba mtu yeyote aliyeenenda tofauti na wazazi wake alipatwa na laana maishani, huku akilia kwa uchungu aliingia ndani ya gari na mlango ukafungwa, bila huruma mzee Mdoe akaanza kurudisha gari kinyumenyume.

Wazazi wa Catarina waliposhuhudia tukio hilo, walinyanyuka kwenye benchi walipokuwa wameketi na kuanza kukimbia wakilifuata gari, hawakubahatika kulifikia, lilishakata kona na kutokomea! Huzuni ikawashika, mama yake Catarina akaanza kulia, kwani tumaini la kuokoa maisha ya mtoto wake lilishahamia kwa Kevin, kwa alichokishuhudia ilionyesha kabisa wazi wazazi wa Kevin hawakuwa tayari mtoto wao afanye hivyo.

“Mungu wangu tutafanya nini sasa?”
“Hata sijui cha kufanya tena, Mungu ndiye anajua!”
Wote walitembea haraka kurejea wodini ambako walimkuta Catarina akiwa katika hali mbaya kupindukia, akitupa shingo yake huku na kule, mambo yote yalikuwa yamebadilika ghafla, nafuu yote ambayo ilijitokeza sasa ilikuwa imepotea na Catarina kwa mara nyingine tena alionekana katika hatari ya kufa!

“Mnaweza mkatuitia Dk. Ngamila?” mzee David aliwaeleza wauguzi walipoingia chumbani dakika kumi baadaye na kukuta Catarina akihangaika.
“Haina shida!”

“Tafadhali nisaidie kumwita, hali ya mgonjwa wangu imebadilika sana.”
Muuguzi akaondoka akikimbia kuelekea ofisini kwao ambako alitarajia kumpigia simu ya dharura Dk. Ngamila ili afike wodini kumwona Catarina katika hali aliyokuwa nayo.
***
Mzee Mdoe aliendesha gari kwa kasi, ndani kukiwa na kilio kama cha mtu aliyefiwa, Kevin alikuwa habembelezeki akidai wazazi wake hawakumpenda ndiyo maana hawakuwa tayari kumfanyia jambo la kumfurahisha kama walivyomuahidi, mama yake alizidi kumtuliza lakini Kevin hakuelewa.

“Hatuwezi kukuruhusu ufanye kila kitu hata kama kina hatari kwako!”
“Hakuna hatari yoyote mama ni kwa sababu uelewa wenu wa mambo ya sayansi ya mwili wa mwanadamu sio mkubwa, sisemi hivyo kuwadharau wazazi wangu, bali nasema hivi kuonyesha kuwa inawezekana mtu kutoa Uboho na akaendelea na maisha yake kama kawaida!”

“Kivipi?” mzee Mdoe akauliza akiwa kwenye usukani, tayari gari lao lilishafika maeneo ya Mbuyuni kwenye kona ya kuelekea Kanisa Katoliki la St. Peter, barabara ya Masaki, jijini Dar es Salaam.

“Uboho ukitolewa kwenye mifupa mwili hutengeneza mwingine na kuna dawa mgonjwa anaweza kupewa kumsaidia atengeneze mwingi na kwa haraka zaidi, sasa kama hivyo ndivyo sayansi inavyosema, ni kwa nini ninyi mnanizuia?”

“Haiwezekani, hatuwezi kukuweka katika hatari kubwa kiasi hicho, umekiepuka kifo kupitia tundu la sindano kwa ajali uliyoipata, leo hii tukuruhusu ukatoe Uboho kumpa mtu yule yule aliyekusababishia ajali? Hapana!” Mzee Mdoe aliongea kwa ukali.
“Baba nilikwishamsamehe Catarina, hayo tuliyaongelea yakaisha, kwa nini mnayafufua tena? Niacheni nikamtolee Catarina Uboho ili apone, sitaki afe, nampenda mno!”
“HAIWEZEKANI!”

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika gazeti la Championi Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply