The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu – 13

2

Catarina ameingizwa chumba cha upasuaji na kupandikizwa Uboho mwingine lakini ghafla hali yake inabadilika presha yake inashuka jambo linalowachanganya madaktari na juhudi za kunusuru maisha yake zinaanza kufanyika.

Nje ya chumba wazazi wa pande zote mbili pamoja na Kevin, hamu ya kila mmoja ni kumwona akitoka salama na kurejea tena katika hali yake ya kawaida hakuna anayefahamu jambo linaloendelea ndani ya chumba cha upasuaji.

Ghafla wakiwa katika mawazo hayo, mlango wa chumba cha upasuaji unafunguliwa na Dk. Ngamila anatoka akiwa amelowa jasho mwili mzima jambo ambalo si la kawaida na wote wanashtuka, mama yake Catarina anaangua kilio.
Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

Kila mtu alikuwa na hamu ya kufahamu
kilichoendelea ndani
ya chumba cha upasuaji, mioyo yao ilijawa hofu, hasa baada ya kumwona Dk. Ngamila akitoka jasho jingi mbele yao, hali iliyoonyesha wazi kuwa kilichoendelea ndani ya chumba cha upasuaji hakikuwa kidogo kwani ilikuwa si rahisi kwa mtu kutokwa jasho jingi kiasi kile ukiwa ndani ya chumba chenye kiyoyozi.

“Daktari tueleze, mioyo yetu haijatulia, kitu gani kinaendelea?” baba Catarina aliuliza.
“Pfuuuu!” badala ya kujibu swali alishusha pumzi hali iliyozidi kuwaongezea wasiwasi.
“Tueleze tu daktari, amekufa?” Kevin aliuliza akilengwa lengwa na machozi.
“Hapana, ila kilichotokea ni muujiza!”

“Kivipi?” mama yake Catarina aliuliza.
Daktari akaanza kuwaeleza namna hatua za mwanzo za kupandikiza Uboho kwenye mifupa ya Catarina zilivyofanyika kwa mafanikio, sindano yenye mrija iliingizwa ndani ya mshipa mkubwa wa damu kifuani kwa Catarina bila matatizo yoyote na mrija huo ukaunganishwa kwenye chumba chenye Uboho ambao ulianza kudondoka taratibu kuingia mwilini.

“Ghafla tukaona shinikizo lake la damu limeshuka kwa kasi kubwa, akaanza kutupa macho juu na kuhema kwa kasi, kazi ya kuokoa maisha ikaanzia hapo kwa kutumia mashine maalum ya kushtua moyo pamoja na kumchoma sindano za kupandisha mapigo juu, kama muujiza, hali yake ikatengamaa tukamalizia kazi iliyokuwa imebaki, humo ndani hakuna mtu anayeamini kwamba Catarina yuko hai, kifupi alishatuacha!”
“Mungu ni mwema, maombi yetu ameyasikia, hivi sasa anaendeleaje?” Kevin aliuliza.
“Anaendelea vizuri, muda si mrefu atatolewa kupelekwa chumbani kwake akaendelee na matibabu mengine!”

Ilikuwa ni furaha mno kwa Kevin na ndivyo ilivyokuwa kwa wazazi wake na pia wazazi wa Catarina, wakakumbatiana na baadaye kusujudu wakiomba kumshukuru Mungu kwa kitendo alichokifanya, mioyoni mwao waliamini maombi waliyoyafanya kabla ya kazi ya kupandikiza Uboho haijafanyika ndiyo yaliyowezesha Catarina kuwa hai.

Baada tu ya kumaliza kusali, Dk. Ngamila akiwa ameshaondoka ndipo mlango wa chumba cha upasuaji ulifunguliwa, machela ambayo juu yake alilala mgonjwa ilisukumwa, walipomwangalia mgonjwa huyo waligundua ni Catarina, Kevin akatabasamu akijisikia mshindi, alikuwa ameokoa maisha ya mwanamke aliyempenda kupindukia.

Wakaanza kuifuata machela hiyo hadi kwenye wodi maalum iliyokuwa kwenye jengo la watu maarufu, madaktari waliamua awekwe huko kuepusha kuambukizwa magonjwa na wagonjwa wengine kwa sababu mwili wake haukuwa na kinga ya kutosha wakati huo.

Kilichofanyika baada ya kulazwa kitandani ni dripu za dawa mbalimbali za kuua wadudu pamoja na chupa ya damu kuchomekwa kwenye mishipa yake, zikaanza kudondosha matone taratibu kuingia kwenye mishipa yake, bado hakuwa na fahamu, Kevin na wazazi wote walisimama wakiwa wamekizunguka kitanda mpaka baadaye muuguzi alipofika na kuwaomba angalau abaki mtu mmoja ili waendelee kumhudumia mgonjwa vizuri.

“Nitabaki mimi!” Kevin alisema haraka haraka.
“Utaweza?” mama yake Catarina aliuliza.
“Hakuna kinachonishinda mama!”
“Sawa, sisi tuko hapo nje, ukipata tatizo lolote kubwa utatueleza.”
“Sawa!”

Wote wakatoka nje na kumwacha peke yake na mgonjwa, alibaki kando ya kitanda mpaka saa tisa alasiri, wazazi wake walipoaga kwenda nyumbani wakimtaka aongozane nao lakini Kevin alikataa akidai angelala hospitali pamoja na mtu yeyote ambaye angebaki.

“Sisi hatuna kipingamizi, tutakuona kesho asubuhi!”
“Sawa baba.”

Alibaki na wazazi wa Catarina mpaka jioni baba yake Catarina naye akaaga akiwaacha Kevin na mama, naye akiahidi kurejea asubuhi ya siku iliyofuata, wakasali pamoja kabla ya mzee huyo kuondoka mke wake akimsindikiza, dakika kama kumi hivi tangu waondoke chumbani, Kevin alishtuka baada ya kumwona Catarina amefumbua macho.
“Catarina!”

“B..e…e!”
“Tumshukuru Mungu!”
“Ka…bi…sa!”
“Amekutendea!”

“Sa…na, ahsa…nte…kwa…kila…kitu!”
“Usijali!”
Alichokifanya Kevin ni kunyanyuka mahali alipokaa na kumbusu Catarina kwenye paji la uso, kisha kuketi kitini na kuanza kumweleza juu ya kilichokuwa kimetokea, Catarina akauliza kama kuna sehemu yoyote ya mwili wake iliyokuwa imepasuliwa lakini Kevin alimwondoa wasiwasi na kumweleza jinsi kazi ya kupandikiza Uboho ilivyofanyika.
“Nasikia maumivu kifuani!”

“Hapo ndipo sindano ilipopitia, daktari alisema walitumia kuingiza Uboho kwa njia ambayo kitaalam inaitwa Apheresis, yaani wanapitisha sindano kifuani mpaka kwenye mshipa wa damu kisha Uboho huingizwa kupitia sindano hiyo hadi kwenye damu ambayo husafirisha mpaka kwenye mifupa.”

“Baba na mama wako wapi?”
“Baba ameondoka, mama amemsindi…” hakumalizia mlango wa chumba ukafunguliwa, akaingia mama yake Catarina na kukimbia moja kwa moja hadi kitandani alipomwona mwanaye akiwa na fahamu.

“Mwanangu! Mwanangu! Nakupenda!”
“Nakupenda pia mama.”
“Pole! Utapona, tumemwomba sana Mungu na amejibu maombi yetu.”
“Ahsante mama, Kevin ameokoa maisha yangu, naomba msipinge mpango wetu wowote?”

“Hatutapinga tena, kila mmoja wetu ameanza kuamini kila mmoja alizaliwa kwa ajili ya mwenzake.”
“Ahsante mama.”

Kevin alikuwa akitabasamu muda wote, hakuwahi kuwa na furaha maishani mwake kama kipindi hicho, aliamini kila kilichotokea kuanzia ajali yake, kuugua kwa Catarina kilimaanisha kuwaunganisha wao badala ya kuwatenganisha, ilikuwa rahisi sasa kwa wazazi wao kukubaliana na kitu walichoomba kwa sababu ya mapito magumu waliyopitia.

“Hivi kweli Catarina kwa wema wote huu niliomfanyia, anaweza kuja kuniacha kwa sababu ya mwanaume mwingine? Haiwezekani, akifanya hivyo atakuwa ameniumiza sana.” Aliwaza Kevin.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika gazeti la Championi Ijumaa.

2 Comments
  1. Emmanuel says

    Mmmh!

  2. Kelvin Mwinuka says

    Daaah Ni Hatariii

Leave A Reply