The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu 37

0

ILIPOISHIA…
Bilionea Jackson Motown ameapa kwamba ni lazima Catarina, msichana mrembo kutoka Tanzania awe mke wake, jambo ambalo msichana huyo analikataa kabisa kwa sababu anaye mchumba, Kevin, waliyeahidiana kufunga ndoa mara baada ya kijana huyo kumaliza masomo.

Catarina anajihusisha na mitindo, jina lake ni kubwa sana duniani hivi sasa, amekwishahamia Afrika Kusini kufanya shughuli hiyo, huko ndiko alikougundua upande wa pili wa kazi ya mitindo ambao dunia nzima haiufahamu, yaani urembo kutumiwa kama vifaa vya ngono na matajiri duniani.

Wakala wake Craig aliyemgundua nchini Tanzania, anamuuza kwa mara ya kwanza kwa Jackson Motown, akiwa amemlewesha pombe, alimpeleka chumbani kwa bilionea huyo ambako Catarina alipoteza bikira yake bila ridhaa, kitu ambacho alikuwa amekitunza kwa ajili ya Kevin.

Jambo hili limemchukiza sana Catarina, amelia mno na hana cha kumwambia Kevin wanapoongea kwenye simu, uamuzi alioufikia wakiwa katika jiji la Paris nchini Ufaransa ni Catarina kuachana na Craig baada ya kukutana na wakala mwingine aitwaye Mario Pizzaro, huyu amemuahidi kumtafutia kampuni nyingine ya tajiri mmoja ambaye hakumtaja jina, iliyopo New York, Marekani.

Wanapanda ndege ya tajiri huyo kuelekea Marekani, wakiwa angani anataarifiwa kuwa tajiri angekuja chumbani kwake kuongea naye, dakika tano baadaye alishangaa tajiri huyo alipoingia; alikuwa ni Jackson Motown, tena akiwa mtupu! Kilichofanyika ndani ya chumba hicho ni kukamatwa kwa nguvu na baunsa wa tajiri huyo ili kurahisisha zoezi la Catarina kubakwa, mpaka akapoteza fahamu!

Nchini Tanzania baada ya mawasiliano na Catarina kupotea, familia yake imechanganyikiwa, wanafanya kila juhudi kufahamu mtoto wao alipo, walipopiga simu Afrika Kusini waliambiwa aliondoka Paris kuelekea Marekani, Catarina alikuwa ameahidi mara akifika katika jiji hilo angepiga simu, jambo ambalo hakufanya.

Wamefikia uamuzi wa kwenda Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje kuomba msaada wa mtoto wao kutafutwa na serikali, wizara ikawasiliana na balozi wa Tanzania aliyeko Washington DC ambaye ameahidi kumtuma mtu kwenda New York siku iliyofuata kumfuatilia mtu aitwaye Mario Pizzaro, aliyedaiwa kuondoka na Catarina.
Je, nini kitaendelea?
SONGA NAYO…

Hofu kwamba Catarina hakuwa hai ilikuwa imetanda kila mahali, vyombo mbalimbali vya habari nchini Tanzania na hata nje ya nchi viliandika sana juu ya tukio hilo. Kwa mtu maarufu kama Catarina haikuwa rahisi kupotea hivihivi bila dunia nzima kuongelea upoteaji wake.
Serikali ya Tanzania ilikuwa imeamua kulivalia njuga suala hilo, ili kuhakikisha kwamba msichana huyo aliyeliletea taifa sifa anapatikana mara moja. Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Mheshimiwa Faida Kalokozi, alipopewa taarifa hizo na kutakiwa kufuatilia, mara moja alituma ofisa wa ubalozi kwenda New York ambako juhudi za kumtafuta Mario Pizzaro zilianza.
Umaarufu wa Mario Pizzaro katika jiji la New York ulikuwa mkubwa mno, haikuchukua muda hata wa saa mbili kufika ofisini kwake, kwenye jengo kubwa lililoandikwa kwa juu maandishi MP DESIGNS INC., ofisa wa ubalozi alipokewa vizuri sana hasa alipoonyesha kitambulisho chake.
“So you are here to see Mr Pizzaro?” (Kwa hiyo uko hapa kumwona Bw. Pizzaro?)
“Yes!” (Ndiyo)
“On what specific reason?” (Kwa sababu gani hasa?)
“I’ve been sent by the embassy to enquire the whereabouts of the model Catarina!” (Nimetumwa na ubalozi kuja kufuatilia taarifa za mwanamitindo Catarina.)
“Oh, hold on a second!” (Subiri sekunde moja) alisema msichana wa mapokezi kisha kupiga simu, ambaye alionekana kabisa aliyekuwa akiongea naye ni Mario Pizzaro, simu ilipokatwa, alimgeukia ofisa wa ubalozi na kumtaka amfuate mpaka kwenye ngazi ambako walipandisha ghorofa iliyofuata na kuingia kwenye mlango uliokuwa mbele yao.
“My name is Mario Pizzaro!” (Jina langu naitwa Mario Pizzaro.)
“I am Athumani Iddi, from Tanzanian embassy in Washington DC!” (Ninaitwa Athumani Iddi kutoka ubalozi wa Tanzania Washington DC.)
“Oh! Good to see you, what can I do for you Mr Iddi?” (Oh! Nafurahi kukuona, nikusaidie nini Bw. Iddi?)
“Do you know a model by the name of Catarina?” (Unamfahamu mwanamitindo anayeitwa Catarina?)
“Yeah! The most beautiful model from Tanzania, I met her in Paris, she worked for us!” (Namfahamu! Ni mwanamitindo mrembo sana kutoka Tanzania, nilikutana naye Paris, alitufanyia kazi!)
“Do you know where she is at the moment?” (Unafahamu mahali alipo kwa sasa?)
“No! We left her in Paris!” (Hapana! Tulimuacha Paris.)
“Are you telling the truth?” (Unasema ukweli?)
“Why should I lie?” (Kwa nini nidanganye?)
“We were told that you travelled with her from Paris to New York, where you were to sign her with another company!” (Tuliambiwa kwamba ulisafiri naye kutoka Paris kuja New York, ambako ulitarajiwa kumtafutia kazi kwenye kampuni nyingine!)
“We were to do so, but at the airport she changed her mind!” (Ilikuwa tufanye hivyo lakini tukiwa uwanja wa ndege alibadilisha mawazo!) aliongea Mario Pizzaro akiwa amekaza macho.
“Thank you so much Mr Pizzaro that’s all I came here for!” (Asante sana Bwana Pizzaro, hayo tu ndiyo niliyoyafuata.)
“You are welcome, in case you need my help, here is my card, call me any time!” (Karibu sana, ukihitaji msaada, kadi yangu hii hapa, nipigie wakati wowote!) aliongea Pizzaro kwa kujiamini, moyoni mwake akifahamu kabisa alichokuwa akikisema ni uwongo.
Ofisa wa ubalozi alirejea Washington siku hiyohiyo na kutoa taarifa kwa bosi wake ambaye naye aliwasiliana na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ambayo iliwapigia simu wazazi wa Catarina na kuwataka wafike wizarani siku iliyofuata ili wapewe taarifa kutoka Washington.
Walikuwa ni watu wa kwanza kufika ubalozini, akiwepo pia Kevin ambaye kupotea kwa Catarina kulikuwa kumemchanganya akili kabisa, alikuwa hali, halali wala hasomi huko chuo kikuu, muda wote alimfikiria Catarina na alikuwa amedhamiria kukatisha masomo ili asafiri kwenda Paris na baadaye New York kumfuatilia mchumba wake aliyekuwa kila kitu katika maisha yake, bila Catarina maisha yake hayakuwa na maana, hivyo ndivyo alivyoamini.
“Karibuni sana!” Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Mheshimiwa Juma Shatila aliwakaribisha.
“Asante sana baba!” mama yake Catarina aliitikia.
Kevin alikuwa kimya, akijifuta machozi kwa kitambaa chake cheupe, kichwani mwake alikuwa akiwaza juu ya nini cha kufanya iwapo waziri angewaambia kwamba Catarina alikuwa bado hajapatikana, akaendelea kubaki kimya akisikiliza maelezo.
“Balozi wetu huko Washington DC alimtuma ofisa wa ubalozi kwenda New York, akakutana na Bwana Mario Pizzaro, aliyedaiwa kumchukua Catarina na kusafiri naye kwenda New York na kufanya naye mazungumzo!”
“Akasemaje?” Kevin akauliza, alishindwa kabisa kuwa mvumilivu.
“Akamweleza kwamba mpango wa kusafiri na Catarina kwenda New York ulikuwepo, lakini wakiwa uwanja wa ndege alibadilisha mawazo, wakaamua kumuacha, kwa hiyo basi hiyo ina maana Catarina alibaki Paris!”
“Hiyo siyo kweli, Catarina hajabaki Paris, hapa kuna tatizo kubwa sana limetokea ambalo watu wanajaribu kulificha, huyo Mario Pizzaro anafahamu mahali Catarina alipo, Mheshimiwa Waziri, kwa niaba ya familia nakushukuru sana, umeonyesha juhudi kubwa za kutusaidia, mimi nitasafiri kwenda huko Paris na baadaye New York, sitarudi hapa mpaka nimempata Catarina, awe hai au amekufa!” Kevin aliongea kwa kujiamini huku akibubujikwa na machozi, moyoni mwake alisikia sauti ikimwambia “Catarina walishamuua, sababu alikuwa tishio kwa wanamitindo wengine ndani ya muda mfupi!”
Je, nini kitaendelea? Catarina yuko hai au amekufa? Kwa nini Mario Pizzaro anasema hakusaifiri naye huku akielewa huo ni uwongo? Jambo gani linafichwa hapa? Fuatilia siku ya Jumatano katika gazeti la Championi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply