The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu-40

2

ILIPOISHIA…
Catarina hajulikani aliko, aliondoka nchini Afrika Kusini kwenda Paris, Ufaransa kuonyesha mitindo, akiwa huko alikutana na mtu aitwaye Mario Pizaro ambaye alikuwa akionyesha mavazi yake, huyu alimwambia kwa uzuri aliokuwa nao kama wangefika New York angemuunganisha na kampuni nyingine ya kufanya nao kazi ili ahame Afrika.

Kwa sababu alikuwa na chuki moyoni dhidi ya wakala wake Craig Anderson ambaye alimlewesha na baadaye kumuuza kwa tajiri Jackson Motown, aliyeapa mbele ya Catarina kwamba angekuwa mke wake atake asitake, akiwa chumbani kwa tajiri huyo alibakwa na kuipoteza bikira yake akiwa hana fahamu kutokana na kilevi alichopewa na Craig.

Jambo hili lilimuuma sana kwani bikira yake aliitunza kwa ajili ya mtu mmoja tu; Kevin ambaye kwa wakati huo alikuwa nchini Tanzania akiendelea na masomo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akakubali kuondoka na Mario kwenda New York kwa kutumia ndege ya tajiri ambaye hakumfahamu.

Akiwa ndani ya ndege hiyo alishangaa kugundua alikuwa amepanda ndege ya Jackson Motown ambaye aliingia chumbani kwake akiwa mtupu na kumwamuru mlinzi wake amgandamize Catarina kitandani ili yeye ambake, tukio hilo likafanyika kinyama mpaka Catarina akapoteza fahamu, wote wakashtuka na kuanza kummwagia maji huku wakimtingisha lakini hakuzinduka, wakahisi alikuwa amepoteza uhai.

Baadaye ilipogundulika kuwa Catarina alikuwa amepotea, hasa baada ya Mario Pizaro kudai hakusafiri naye kutoka Paris, Kevin, mchumba wake aliamua kukatisha masomo na kusafiri mpaka Paris na baadaye Marekani kufuatilia, akiwa Paris alijifunza kuwa Mario Pizaro aliondoka na Catarina lakini alikuwa anadanganya kwa sababu ambayo Kevin hakuifahamu.

Akiwa Marekani ameongozana na Afisa wa Ubalozi wa Tanzania, Maofisa wa FBI kwenda uwanja wa ndege wa JF Kennedy kukagua kwenye kamera za uwanja, zikaonyesha kweli Mario Pizaro, Jackson Motown hawakuingia Marekani wakiwa na Catarina! Swali likawa Catarina alipotelea angani wakati ndege hiyo haikutua mahali popote?SONGA NAYO…

Mario Pizaro alikuwa ofisini kwake, mwenye mawazo mengi, kitendo cha afisa wa Balozi wa Tanzania kuja kufuatilia juu ya mahali alipokuwa Catarina kilimpa wasiwasi mwingi hasa alipokumbuka yaliyotokea ndani ya ndege wakati wakiruka kurejea New York.

Moyo wake ulijaa majuto mengi, akajilaumu ni kwa nini alikubali kutumiwa na Jackson Motown katika jambo ambalo sasa lingeweza kumfikisha mahakamani na hatimaye akahukumiwa kifo au kifungo cha maisha jela, alitamani siku zirudi nyuma na ile ambayo walikuwa na Catarina ndani ya ndege iondolewe katika orodha ya siku za dunia.

“I wish I knew!” (Laiti ningejua!) alijisemea Mario Pizaro moyoni mwake.
Kitendo chake cha kupokea dola za Kimarekani laki mbili ili tu awezeshe zoezi la kumkabidhi Catarina kwa Jackson Motown ndiyo kilikuwa kimemuingiza kwenye matatizo, aliogopa jela kwani alikuwa na ndoto nyingi sana maishani mwake hasa kwenye ulimwengu wa mitindo.

Mawazo yake yalimrejesha kwenye kumbukumbu ya kilichotokea kwenye ndege kabla ya kutua New York, akamwona Catarina akiwa amezimia, wote wakihangaika kummwagia maji ili azinduke lakini haikuwezekana, daktari wa Jackson Motown ambaye husafiri naye kwenye ndege yake alipoitwa alisema moyo ulikuwa ukipiga kwa mbali sana na kama kusingefanyika jambo lolote la ziada angepoteza uhai.
“What can you do?” (Unaweza kufanya nini?), Jackson Motown alimuuliza daktari wake.

“May be inject her with steroids and adrenaline, it might help!” (Labda tumchome sindano za kusisimua mwili na Adrenaline, pengine inaweza kusaidia!).
“Go ahead and do it, I don’t want to get into trouble!” (Mchome, sitaki kuingia kwenye matatizo!), Jackson Motown alifoka, tayari alishachanganyikiwa, hakuna aliyetegemea Catarina angeingia katika hali hiyo.

Sindano zikachomwa lakini Catarina hakushtuka, moyo wake ukaendelea kutingishwa kwa nguvu na daktari, wakati mwingine akimpulizia pumzi puani ili kuyashtua mapafu lakini bado Catarina alikuwa ametulia, kulikuwa na kila dalili angekufa! Mario Pizaro alikuwa akitetemeka huku akimwangalia Jackson Motown.

“What are we going to do?” (Tutafanya nini?)
“If she dies?” (Kama akifa?)
“Yes.” (Ndiyo!)

“I will find the way to burry her within the airport compound!” (Nitafanya mpango wa kumzika ndani ya uwanja wa ndege!)
“Is it possible?” (Inawezakana?)
“There is nothing impossible to Jackson Motown!” (Hakuna kisichowezekana kwa Jackson Motown!)
“Really?” (Hakika?)

“I know the airport manager, once we land I will ask him to come and talk to me, I will pay him anything so that Catarina’s body wont be taken out of the airport!” (Namjua Meneja wa Uwanja, tukishatua nitamwomba aje kuongea nami, nitamlipa kiasi chochote cha fedha ili mwili wa Catarina usitolewe nje ya uwanja!)

“That will be good, atleast we wont go to jail, I am scared of that place!” (Hiyo itakuwa sawa, hatutakwenda jela, naogopa eneo hilo vibaya mno!)
“Me too!” (Mimi pia!)

Ndivyo ilivyotokea, ndege ilipotua tu kwenye uwanja wa ndege wa JF Kennedy, Jackson Motown alichukua simu yake na kumpigia Boniphace Hill, meneja uwanja na kumtaka aje kwenye ndege yake kwa mazungumzo, hazikupita dakika ishirini akawa tayari amekwishaingia kwenye chumba cha Jackson Motown na kuzungumza kwa nusu saa.

Alichokishuhudia Mario Pizaro baadaye ni mfuko wa plastiki mkubwa ukiingizwa ndani ya ndege na kikundi cha askari wa uwanja wa ndege watano, walipotoka vijana hao walikuwa wamebeba mzigo ambao bila hata kuuliza swali, Mario Pizaro alielewa ni maiti ya Catarina inakwenda kuzikwa mahali fulani ndani ya uwanja.

Akashusha pumzi kwa uwoga, lilikuwa ni tukio baya kabisa kulishuhudia maishani mwake, roho ikamuuma na machozi yakamtoka kwa sababu alikuwa amesababisha kifo cha msichana mrembo kupindukia aliyekuwa na ndoto za kufanikiwa maishani mwake.

“God forgive me!” (Mungu nisamehe!) alitamka maneno hayo moyoni mwake wakati yeye na Jackson Motown wakishuka ndani ya ndege tayari kwa kutoka nje ya uwanja bila mwili wa Catarina.

Je, nini kitaendelea? Catarina amekufa? Kevin atafanikiwa kuufahamu ukweli huu? Fuatilia siku ya Jumatano katika gazeti la Championi Jumatano.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

2 Comments
  1. winnie lucas says

    Global rudishen prosses ya search kwa habari uitakayo

    1. Global Publishers says

      ipo, angalia kwenye menu bar mwishoni utaiona

Leave A Reply