The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu – 52

0

ILIPOISHIA…
JACKSON Motown pamoja na ukatili wake alioutenda, bado hayuko tayari kukubali kuingia kwenye mikono ya sheria, hivyo akiwa hospitalini anawatumia vijana wake wa kazi walioko nje ili kuhakikisha Kevin anakufa kwani aliamini kama Kevin anaendelea kuwa hai ingekuwa tatizo kwake.

Vijana wa kazi wanafanya uchunguzi na hatimaye wanafanikiwa kujua mahali Kevin alipo, kisha wanampa taarifa Jackson Motown ambaye anaamuru nyumba aliyomo ilipuliwe kwa bomu na ikiwezekana mzee Thomas Edmund aliyemhifadhi Kevin naye afe.

Usiku wa siku hiyo, vijana wa kazi wanakwenda na kufanya kama walivyoambiwa. Wanafanikiwa na kuondoka huko huku wakiamini kwamba Kevin amekufa. Baadaye, wanapokwenda hospitalini kumpa taarifa Jackson Motown, wanapewa taarifa zingine kwamba msichana Catarina yupo nchini Marekani, hivyo wamtafute mpaka wampate na kumuua kwa gharama yoyote ile.
Je, nini kiliendelea?
SONGA NAYO…

Japokuwa Jackson Motown alikuwa hospitali lakini aliweza kugundua kila kitu kilichokuwa kikiendelea husasan maisha ya Catarina ambaye kipindi hicho alikuwa hapo nchini Marekani. Alikuwa mtu mwenye fedha nyingi na mwenye mtandao mkubwa, watu waliounda mtandao wake hawakuwa vijana wake tu bali pia walikuwepo maafisa kutoka FBI na hata CIA.
Hiyo ndiyo iliyompa nguvu ya kumtafuta msichana Catarina na kumuua. Akawaambia vijana wake kwamba msichana huyo alikuwa nchini Marekani, hivyo ilikuwa ni lazima atafutwe na kuuawa kama njia mojawapo ya kuficha siri kubwa iliyokuwa nyuma yake na kushinda kesi kubwa ambayo kwa kipindi hicho ilikuwa gumzo nchi nzima.
Vijana hao wakaondoka, vichwani mwao wakiwa na kazi moja kubwa, waliambiwa kwamba msichana huyo alikuwa nchini Marekani lakini hawakujua ni wapi, hivyo walichokifanya ni kuwasiliana na vibaraka wao kutoka FBI ili wawape uhakika juu ya mahali alipokuwa msichana huyo.
“Bado hatujajua, sasa hivi imekuwa siri kubwa mno, ila usijali, tutawapeni taarifa,” alisema mmoja wa FBI.
“Fanyeni haraka, tunataka kujua mahali alipo huyo msichana kabla mambo hayajaharibika, kumbuka tunachokitaka ni kujua sehemu tu, hayo mengine tuachieni sisi,” alisema kijana huyo kwa sauti yake yenye mikwaruzo mingi.
Jackson Motown akapelekewa taarifa kwamba ilithibitishwa kwamba msichana huyo alikuwa ndani ya nchi hiyo ila hakuna aliyejua mahali alipofichwa kwani kwa kipindi kama hicho, hata FBI ambao walipewa jukumu la kumlinda msichana huyo walikuwa makini, hawakuingilika hovyo, mbaya zaidi wao wenyewe walikuwa wakilindwa ili wasifanye usaliti wowote ule.
Maofisa wa FBI ambao waliangalia sana fedha kuliko misingi ya kazi yao wakaanza kufanya kazi ya kupeleleza ili wajue mahali alipokuwa msichana huyo. Hiyo haikuwa kazi nyepesi, ilikuwa ngumu mno.
Waliwasiliana na wenzao, kila aliyeulizwa, hakuna aliyejua zaidi ya maofisa wakuu wa FBI ambao hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kuwaingia watu hao kutokana na umakini wao katika kazi na pia kutokubali kuhongwa.
“Mmepajua alipo?” aliuliza Jackson Motown.
“Bado mkuu! Ila watu wapo wanafanyia kazi!”
“Huu ni ujinga, yaani kujua mahali kalipo hako kabinti imekuwa kazi kubwa namna hii? Siku zinasogea, hivi hamlioni hilo? Au hamjui hatari iliyopo mbele yangu? Au mnafurahia kuona ushahidi unapatikana na mimi kufungwa gerezani maisha?” aliuliza Jackson Motown ambaye alionyesha kuchanganyikiwa, aliongea kwa hasira mpaka mishipa ya shingo kumtoka.
“Tunahakikisha tutakuletea taarifa muhimu mkuu! Tuamini…”
“Ninawapa siku mbili tu, mkishindwa, msifike hapa, tena mkajifiche maana naweza kuwaua muda wowote ule,” alisema Jackson Motown.
Vijana wale wakarudi mitaani, walichokifanya ni kuwasiliana na wale FBI waliokuwa upande wao na kuwaambia kila kitu kilichotokea, hivyo walitakiwa kuhakikisha wanafanya haraka kujua mahali msichana huyo alipofichwa kipindi hicho.
“Tupe saa kadhaa…” alisikika afisa mmoja wa FBI.
Walifanya kazi siku nzima, ilipofika mchana, wakapata taarifa kwamba mtu huyo waliyekuwa wakimtafuta alikuwa amehifadhiwa katika nyumba moja iliyokuwa na ulinzi mkubwa ambao usingekuwa rahisi kupitika.
“Kwa hiyo tutafanikiwaje?” aliuliza Dracula, mmoja wa vijana wa Jackson Motown.
“Usijali, miongoni mwa watu waliowekwa huko kwa ajili ya ulinzi, yupo afisa mmoja ambaye tutafanikiwa kupata kila kitu kupitia yeye,” alisema afisa huyo.
“Basi sawa! Fanyeni kila liwezekanalo mpaka tujue kila kitu kinachoendelea huko,” alisema Dracula.
“Hakuna shida!”
****
Ulinzi uliimarishwa kila kona, maafisa watano wa FBI waliokuwa na bunduki walikuwa wakilinda vilivyo, hakukutakiwa mtu yeyote kuingia ndani ya nyumba hiyo kwani mtu waliyekuwa wakimlinda alikuwa muhimu mno.
Ndani, Catarina alikuwa na mawazo tele, hakuwa na furaha hata kidogo, tangu aingie ndani ya nyumba hiyo, alijikuta akishindwa kufanya kitu chochote kile zaidi ya kulala siku nzima. Hata kula, hakuwa anakula, hakusikia njaa hata kidogo kitu kilichoifanya afya yake kuwa mbaya zaidi.
Upweke ulikuwa mkubwa, kila wakati alikuwa mtu wa kumuwaza Kevin. Alimpenda mpenzi wake na katika kipindi hicho hakuamini kama kweli mwanaume huyo alikufa na asingeweza kumuona tena katika maisha yote.
Alimchukia mno Jackson Motown, hakutaka hata kumuona, kitendo cha kumuua mpenzi wake kilimfanya kumchukia mtu huyo hata zaidi ya alivyomchukia shetani.
Hali yake iliendelea kuwa mbaya kila siku kitu kilichowafanya FBI kumuuliza ni kipi alikihitaji katika maisha yake, akachagua kuwa karibu na wazazi wake, hivyo kuanza harakati za kuwatafuta watu hao na kuwaambia kwa haraka sana waende nchini Marekani.
Simu ikapigwa mpaka makao makuu, taarifa zilizofika ni kwamba Catarina aliwahitaji wazazi wake na hivyo harakati za kuwaleta nchini Marekani kuanza mara moja. Maafisa wanne wa FBI wakatumwa mpaka nchini Tanzania ambapo wazazi hao wakachukuliwa na kupelekwa jijini New York nchini Marekani.
Catarina alipowaona, hakuamini, machozi yakaanza kumbubujika, akawasogelea na kuwakumbatia. Mbali na Kevin, hao ndiyo walikuwa faraja yake, hakutaka kuwaona watu hao wakiondoka mikononi mwake, aliwapenda, aliwathamini na muda wote alitaka kuwa nao.
“Nimewakumbuka mno…” alisema Catarina huku akiwakumbatia.
“Mbona unaonekana hivyo? Unakula kweli?” aliuliza baba yake, mzee David.
“Ninamkumbuka Kevin wangu baba….” alijibu Catarina.
“Pole sana, usiwe na mawazo, hautakiwi kuwa hivyo, kula, achana na mawazo binti yangu, cha msingi angalia kilicho mbele yako. Ni lazima huyu mtu afungwe gerezani,” alisema baba yake kwa sauti ya chini na yenye kufariji.
Japokuwa wazazi wake walifika hapo lakini mawazo hayakuweza kumuisha, bado upweke uliendelea, kichwa chake kilimfikiria zaidi Kevin huku muda mwingi moyo wake ukibeba hasira nzito juu ya Jackson Motown ambaye kwake alionekana kama shetani.
Wazazi wake waliumia, walijua kwamba kama wasingemtafuta mchungaji kwa ajili ya kumfanyia maombi na kumpa ushauri kuhusu mambo ya kiroho basi hali yake ingezidi kuwa mbaya. Walichokifanya ni kuzungumza naye na kumwambia kile walichotaka kukifanya kwa ajili yake.
“Hakuna tatizo, nitafurahi, sijihisi kuwa sawa kabisa, ninahitaji maombezi na ushauri wa kiroho,” alisema Catarina huku akiwaangalia wazazi wake kwa macho yaliyoonyesha ni jinsi gani akili yake haikuwa sawa.
Walichokifanya wazazi hao ni kuwasiliana na maafisa wa FBI na kuwaambia kwamba walihitaji kupata mchungaji ambaye kazi yake ingekuwa ni kumfanyia maombezi Catarina na kumpa ushauri wa kiroho.
Hilo wala halikuwa tatizo, walichokifanya ni kuwasiliana na makao makuu ambapo wakawaambia kile walichoambiwa na wazazi wa Catarina, kumtafuta mchungaji wala halikuwa tatizo, walichokifanya ni kumwangalia mchungaji ambaye angefaa kufika katika nyumba hiyo na kuanza kumhudumia Catarina kiroho.
Hawakufikiria kabisa kama kufanya kitu hicho pia ingekuwa hatari katika maisha ya Catarina. Majibu waliyorudisha ni kwamba wapewe siku mbili, hatimaye huyo mchungaji angepatikana.
“Nina wasiwasi mno…” alisema Catarina.
“Wasiwasi wa nini?”
“Sijui, ila nina wasiwasi mno,” Catarina aliwaambia wazazi wake. Wala hawakujali zaidi ya kumwambia kwamba asiwe na wasiwasi wowote, mchungaji angepatikana.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply