The House of Favourite Newspapers

Mkuki moyoni mwangu – 65

0

Kevin amefanikiwa kuingia ndani ya hifadhi ya wanyama ya American National Park, akiwa hapo anakutana na kijana anayejitambulisha kwake kwa jina la Jamal, akiwa hajui siri iliyojificha ndani ya kijana huyo Kevin kwa uchungu mkubwa anamsimulia kijana huyo kila kitu kwamba ni kwa nini alikuwa ndani ya hifadhi hiyo.

Kevin anaeleza kila kitu jinsi alivyompenda Catarina na kwa jinsi maisha yake yasingekuwa bila Catarina kwa jinsi alivyompenda jambo linalompa wakati mgumu Jamal kwani tayari anaishi na Catarina na anampenda kupita kiasi lakini pia msichana huyo ni mjamzito hayuko tayari kuona anaondoka na kumwacha peke yake.

Jamal anamweleza Kevin kwamba yuko tayari kumsaidia mpaka ahakikishe anampata mpenzi wake huyo. Safari inapangwa na Jamal anarejea nyumbani kumweleza Catarina kwamba alipata safari ya dhararu usiku wa siku hiyo na angerejea alfajiri.

Safari ikazidi kuendelea, mpaka saa nne na nusu usiku ndipo gari likasimamishwa kando ya bwawa kubwa la maji, mbalamwezi ilikuwa ikipita angani na kusaidia kupunguza giza gari linasimama na Jamal anamweleza Kevin kwamba hapo walipokuwa ndipo mahali sahihi ambako wahalifu wengi hutupa watu.

“Shuka tu uanze kumulika huku na kule, namalizia kuongea na simu moja hapa halafu nitaungana na wewe!” aliongea Jamal. Je, nini kitaendelea?SONGA NAYO…

Palitisha mno mahali pale, giza lilikuwa nene isipokuwa katika zile sehemu zilizomulikwa na taa ya gari. Moyo wa Kevin ulisita lakini akalazimika kumwamini mwenyeji wake aliyeonekana tangu mwanzo kuwa mtu mwema, akachukua tochi, kufungua mlango na kutoka nje akiuacha mlango wazi.
“Usiku huu nitaona kitu kweli?” aliuliza akijaribu kuzunguka nyuma ya gari.
“Wewe nenda tu!”

“Unafikiri hakuna tatizo lolote kama wanyama wakali au?”
“Mimi ni mwenyeji, eneo hili huwa hakuna tatizo kabisa, hata mimi naegesha gari kisha naungana na wewe.”

“Sawa!” Kevin aliitikia.
Akimulika kwa tochi yake mbele aligeuza shingo na kushuhudia gari likienda mbele taratibu kisha kugeuka kuelekea lilikotokea, hakuamini alipoliona likiondolewa kwa kasi ya ajabu na kutimua vumbi! Kevin akabaki peke yake, akishuhudia taa za nyuma ya gari zikipotea na yeye kuzungukwa na giza.

Hapo ndipo alielewa sababu ya kuletwa porini pale, haikuwa nyingine zaidi ya kuuawa, kichwani mwake akawa na maswali mengi ni kwa nini Jamal aliamua kumtelekeza porini aliwe na Simba, hakupata jibu! Sababu hapakuwa na wakati wowote maishani walikutana akamkosea jambo lililopelekea labda aamua kulipa kisasi.

Aliizungusha mwanga wake wa tochi kila upande akichora duara kumzunguka yeye, mwanga wa tochi yake ukakutana na mianga kadhaa yenye kung’ara ambayo aligundua ilikuwa ni macho ya Simba au wanyama wengine wakali, yeye pia kama ilivyokuwa kwa Catarina angekuwa chakula cha wanyama wa porini, kwa nini? Aliendelea kujiuliza bila kupata majibu.

“Grrrrrr!Grrrrrr!Grrrrrrr!” ulikuwa ni muungurumo wa mnyama, hakuwahi kumwona Simba wala kuusikia muungurumo wake lakini kwa jinsi ulivyotikisa msitu, alijua kabisa huyo alikuwa ni Mfalme wa Nyika, pengine akifurahi kitoweo.

“Inavyooneka huyu Simba alikuwa na ugali tu, sasa ameletewa mboga! Mungu nisaidie!” aliwaza Kevin.
Alipotupa macho pembeni, mita kama kumi na tano hivi kutoka mahali alipokuwa amesimama, aliona mti alioufananisha na mkwaju baada ya kumulika na tochi yake, hakuona mnyama yoyote upande ule, kwa kasi ya ajabu akaukimbilia mti ule na kuuparamia hadi juu, Simba watatu wakafunga breki chini ya mti huo wakiunguruma.

“Ahsante Yesu!” alijikuta akitamka maneno hayo ingawa hakuwa mwendaji sana wa kanisani katika maisha yake ya kawaida.

Ilikuwa ni kama ndoto kwake, kwamba angeamka na kujikuta yu nchini Tanzania amelala kitandani kwake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Catarina akiwa Marekani kufanya masuala ya mitindo, wakitarajia kufunga ndoa! Haikuwa hivyo, Simba watatu waliendelea kumsubiri chini ya mti, mara kadhaa wakijaribu kuuparamia mti lakini hawakuweza kufika juu.

Kukacha asubuhi Simba wakiwa bado wako eneo hilohilo na kushinda wakimsubiri Kevin ashuke, ikawa hivyo kwa siku tatu mfululizo, kiu na njaa vikizidi kumbana, alishindwa kabisa kuelewa kama wangeendelea kumsubiri hapo kwa wiki nzima ingekuwaje.

Siku ya tano nguvu zilishaanza kumuishia, Simba wakiwa bado wako palepale, hata ilipotokea akaondoka mmoja kwenda kutafuta kilichoonekana kuwa ni mawindo, wawili walibaki wakimsubiri Kevin ashuke! Ilikuwa ni kama vile walifahamu kuwa asingeweza kukaa mtini kwa siku nyingi bila kushuka.

Siku ya saba Kevin alikuwa hawezi tena, akafungua mkanda wa suruali yake na kujifunga mkono kwenye tawi, ili kama akizidiwa kabisa na kutakiwa kuanguka, angalau aning’inie bila kufika chini! Macho yalishaanza kuingia giza, kulikuwa na kila dalili kwamba angedondoka chini, Simba walikaa chini vichwa vyao vikiwa vimeelekezwa juu kumwangalia.
***
Jamal aliendesha gari lake kwa kasi ya ajabu, kilometa mia moja na ishirini kwa saa katika njia yenye mabonde mengi, moyoni mwake hakuwa na furaha pamoja na kufanikiwa kumuua Kevin, hii ni kwa sababu alielewa kabisa kijana huyo hakuwa na hatia yoyote, pamoja na kukosa furaha, hakujuta kwani alichokifanya kilikuwa ni kutetea ambacho yeye aliona ni haki yake yaani Catarina na mtoto aliyekuwa tumboni.

Aliegesha gari ndani ya ngome ya nyumba yake saa kumi na mbili na dakika ishirini asubuhi, likiwa limejaa tope kiasi cha rangi kutoonekana, akashuka na kufunga mlango,mwili wake ulikuwa umechoka kupindukia, kwani safari aliyokuwa amesafiri kwa kuiunganisha ilikuwa ni sawa na kilometa elfu moja na mia sita, alihisi kitu pekee alichohitaji wakati huo kilikuwa ni kulala.

Mlango ulikuwa wazi, akausukuma na kuingia ndani ambako alinyoosha moja kwa moja hadi chumbani na kumkuta Catarina ameketi kitako akimsubiri, wakakumbatiana na kupeana mabusu ya salamu! Jamal hakuwa katika hali ya kawaida ambayo Catarina aliizoea, jambo lililomfanya bila kupoteza wakati aulize.
“Mbona uko hivyo?”
“Nimechoka tu.”

“Basi inabidi upumzike sababu leo ni Jumapili, huhitaji kwenda ofisini!”
“Hivyo ndivyo nitakavyofanya, niamshe saa tano kamili!”
“Nenda basi ukaoge kwanza.”
“Sawa mpenzi.”

Jamal akavua nguo zake chafu kisha kuingia bafuni ambako alioga kwa dakika kumi tu na kutoka, akajifuta maji kwa taulo kisha kujitupa kitandani, nusu saa tu baadaye alikuwa akikoroma! Saa mbili kamili, Catarina alichungulia kupitia dirishani na kuliona gari lilivyochafuka, uamuzi wake ukawa ni kutoka nje na kuliosha, hakuogopa sana sababu angekuwa ndani ya ngome ya nyumba yao, watu wasingemwona.

Wakati analiosha gari hilo kwa kutumia mpira wa maji, macho yake yalitua ndani ya gari kiti cha nyuma na kuliona begi ambalo tangu aishi na Jamal hakuwahi kuliona, akaufungua mlango na kulisogeza karibu yake, moyo ukamtuma kufungua ndani ili aone kulikuwa na nini, macho yake yakakutana na nguo lakini pia kulikuwa na kitabu cha kuandika kumbukumbu, ambacho Waingereza hukiita Diary.

Alikichukua kitabu hicho na kukisoma juu yake, kiliandikwa; Kevin Mdoe’s Diary, special events in the search for my love Catarina are recorded in this book! Aliyasoma maneno hayo yaliyomaanisha Kitabu cha Kutunzia kumbukumbu ambamo matukio muhimu katika kumtafuta mpenzi wangu Catarina hutunzwa! Moyo wake ukalipuka, mapigo kadhaa yakarukwa, jasho jingi likamtoka, akatamani kufungua ndani asome kilichoandikwa.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply