The House of Favourite Newspapers

Mkuki Moyoni Mwangu 78

1

BAADA ya Catarina kuondoka, Jamal  ameamua kufuatilia NewYork ili kufahamu ni wapi alipo, kumpata na kurejea naye nyumbani kwake kwani tayari alikuwa ni mama wa mtoto wake lakini pia alimpenda kupita maelezo, kifupi hakuwa tayari kushuhudia Catarina akiondoka na mwanaume mwingine.

Jamal yupo ndani ya treni safari kuelekea NewYork, kichwani mwake akifikiria jambo moja tu; Catarina basi. Akiwa hapo anajaribu kudadisi kama waliwahi kumwona mwanamke mjamzito, ni hapo ndipo mfanyakazi mmoja ndani ya treni anamwambia waliwahi kumwona lakini hali ya binti  huyo ilibadilika ghafla na kulazimika kupelekwa Hospitali ya  NewYork Obstetrics & Gynaecology  kwani alikuwa akivuja damu nyingi.

Kwa saa kadhaa anafanikiwa kufika NewYork na moja kwa moja anakwenda kwenye hospitalini na kuuliza kisha kuelekezwa chumba ambacho ndicho haswa ndani yake alikuwepo Catarina. Anagonga mlango na kuingia ambako anakuta watu wakisali na yeye kuungana nao na sala inapomalizika watu wote ndani ya chumba wanafungua macho.

Ni hapo ndipo macho ya Jamal na Kevin yanagongana na Kevin anatoa maneno makali kwa Jamal akimwambia ni nini alikuwa amefuata hapo na kumkumbusha kwamba amesahau mambo aliyomtendea? Je, nini kitaendelea?

SONGA NAYO…

WATU wote ndani ya chumba walishikwa na mshangao, maneno aliyokuwa akisema Kevin yalimfanya kila mmoja ashike mdomo, mwanaume aliyekuwa amesimama mbele yake ndiye Jamal ambaye Kevin aliwaeleza wazazi wake wote kwamba alimtupa porini ili aliwe na wanyama wakali.

“Mama! Huyu ndiye Jamal, mwanaume aliyejifanya kunisaidia kumbe alikuwa anataka tu kuniua!”
“Mungu ni mwema, alikunusuru na sasa umekutana na Catarina tunakuomba umsamehe!”
“Hapana, anastahili kifo.”
“Kevin!” baba yake aliita.
“Naam baba.”
“Mimi ni nani kwako?”
“Baba yangu.”
“Basi ninakusihi uchukue maneno yangu na kuyafanyia kazi, hutakiwi kulipa ubaya kwa ubaya, Biblia inakuambia yakupasa kujifunza kutenda mambo mema tu na si vinginevyo.” Mzee Mdoe aliongea akimsogelea Kevin ambaye alionekana kufura muda wote kwa hasira.

Wakati hayo yote yakitokea, Catarina alikuwa kimya juu ya kitanda chake, kilichoonekana mashavuni mwake yalikuwa ni machozi tu yakitiririka kidevuni mwake, alifikiria mambo mengi sana, kichwani mwake alikumbuka jinsi Kevin alivyookoa maisha yake, akaenda mbele zaidi na kukumbuka pia wema wa Jamal, mwanaume aliyeokoa maisha yake porini akanusurika kuliwa na Simba. Moyo ukamuuma kupindukia.

Wakati hayo yakitokea ndani ya chumba hicho, Jamal alikuwa amepiga magoti pembeni mwa Catarina machozi yakimtoka, pamoja na kugundua kwamba alikuwa amefanya makosa, lakini bado hakuwa tayari kumwachia mwanamke aliyeamini kwamba alimpenda kupindukia.

“Catarina, mpenzi wangu, mke, mama wa watoto wangu nimekosa, naomba unisamehe na ikiwezekana urudi na tuishi kama zamani, ninakupenda mno, hakika siko tayari kuona unachukuliwa na mwanaume mwingine, tena nikishuhudia…” kwikwi ya kulia ikamkamata Jamal akashindwa kuendelea.

“Najua unanipenda, nami nakupenda pia ila kutoka ndani ya moyo wangu siwezi kuficha, ninampenda mno Kevin. Mwanaume huyo aliyesimama kando yangu, aliokoa maisha yangu, hakika bila yeye hata wewe usingenifahamu.”
“Usiniache Catarina, siwezi kuishi bila wewe, kumbuka ahadi yetu ya kufunga ndoa, ni kweli mimba imeharibika lakini bado tunayo nafasi ya kufanya mambo mazuri zaidi, kumbuka tuliongea nini mke wangu.”
“Jamal sikia nikuambie, uamuzi wangu ni kubaki na Kevin, hivyo ndivyo siwezi tena kuendelea na wewe, tafadhali nielewe,” aliongea Catarina kwa sauti ndogo.

Kauli hiyo ya Catarina ilikuwa ni kama mkuki ndani ya moyo wa Jamal, haraka akionekana kutokuamini maneno aliyoyasikia kutoka kwa mtu aliyeamini siku zote kwamba alimpenda kwa dhati, akamgeukia Kevin kisha kupiga magoti mbele yake, bila kujali akakusanya  mikono yake yote miwili kwa mbele kama mtu aliyekuwa akisali.

“Kevin naomba unisamehe, nilikutenda ubaya usiopimika yote hii ni kwa sababu nilimpenda Catarina, nilikupeleka porini ili uliwe na wanyama wakali kwa sababu sikuwa tayari kumpoteza, nilifahamu wazi kitendo cha wewe kukutana na Catarina kilikuwa ni kulipoteza penzi langu kwake, alikupenda mno, lakini niseme jambo moja hapa, Mungu alikuwa nalo kusudi ndiyo maana alikuokoa katika midomo ya simba na mpaka leo uko hai…naomba unisamehe, niachie Catarina wangu, mwanamke ninayempenda kuliko wote duniani, tukafunge ndoa na kuishi maisha ya raha mustarehe….” aliongea Jamal huku akilia.

Muda wote huo Kevin alionekana kuwa kimya, hasira kali zilionekana, alipumua kama vile mtu aliyetoka katika mbio ndefu, maneno ya Jamal yalimzidishia chuki isiyo kifani ndani yake, akatamani kuua bila huruma, taratibu bila kusema chochote akasogea karibu na Jamal kisha kukunjua mikono yake kama vile alitaka kumkumbatia.

Haikupita muda mrefu kelele kali zikasikika ndani ya chumba, Kevin alikuwa amemkaba Jamal akimwambia maneno yaliyoashiria chuki aliyokuwa nayo ndani juu yake.
“Hustahili kuishi Jamal, wewe unatakiwa kwenda kuzimu.”
“Ni.sa..me..he…” Aliongea Jamal kwa taabu.

“Hakuna, leo lazima nikuondoe duniani.”
“Na…omb..aaaa….” alijibu Jamal, mikono ya Kevin ikizidi kukamata vizuri shingo yake, jambo lililosababisha Jamal ashindwe kuendelea kuongea na kubaki akitoa macho ishara kwamba alikuwa katika hali ya kifo.

“Kevinnnnnn! Kevinnnnn!” Tafadhali mwache, nasemwa mwache Jamal, huoni kama utamuua,” Catarina alipiga kelele.
“Afe tu, hakuna sababu ya mtu katili kama huyu kuendelea kuishi hapa duniani.”
“Hapana, msamehe, mwache ili aondoke.”
Kevin hakutaka kusikia maneno ya Catarina, aliendelea kuzungusha vyema mikono yake kuzunguka shingo ya Jamal na kidogokidogo Jamal akaonekana kuishiwa nguvu japo alijitahidi kupambana kama mwanaume. Kwa takriban dakika kumi nzima, Kevin aliendelea kumkaba Jamal, hata wazazi walipojaribu kuamulia nao walisukumwa na kuangukia pembeni, nguvu za ajabu zilionekana kwake, mwisho wakabaki kuangalia tu bila kujua nini cha kufanya huku wakipiga kelele kuomba msaada.

“Kevin naomba unisikilize kama kweli unanipenda,” Catarina aliongea akijaribu kunyanyuka kitandani.
“Nakupenda Catarina ndiyo maana nafanya haya yote.”
“Najua, Jamal alikuwa mtu mbaya lakini pia aliokoa maisha yangu porini, pengine nisingekuwa hai kama si yeye na wewe pia uliokoa maisha yangu wote mliokoa maisha yangu kwa wakati tofauti, ninachokuomba umwache Jamal, tayari umeshanipata, msamehe ili maisha yaendelee huoni kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha yako kwa kuua na kuingia jela? Nakusihi umwache,” aliongea Catarina safari hii kwa upole.

Taratibu mikono ya Kevin ikaonekana kulegea kutoka shingoni mwa Jamal ambaye alianguka chini kama mzigo akionekana kuwa kimya kabisa.

“Jamal! Jamal!Jamal!” Catarina aliita mfululizo lakini Jamal hakuitika kwa ilivyoonekana alikuwa amepoteza fahamu.
“Unaona sasa? Kevin mwanetu umeua!” aliongea mzee Mdoe akisogea karibu na sehemu aliyoangukia Jamal, akanyoosha mkono wake na kukishika kifua chake, kilionekana kutulia, akasikiliza mapigo ya moyo nayo hakuyasikia, akahisi kuchanganyikiwa, ghafla wakiwa hapo wakashuhudia damu zikimtoka Jamal puani, masikioni na mdomoni pia huku akiwa hajitambui.

“Hili ni tatizo kubwa, hebu iteni wauguzi waje hapa haraka,” aliongea Catarina akitetemeka na mzee Mdoe akatoka mbio ndani ya chumba akipiga kelele ya kuwaita wauguzi kwa msaada.

Kila mtu ndani ya chumba aliingiwa na hofu, mtu aliyekuwa mzima muda mfupi uliopita iweje awe chini tena akitokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili wake? Lilikuwa ni swali la kila mmoja wao, yote hayo yakitokea Kevin alikuwa kimya kabisa, hakuongea neno lolote, naye pia alionekana kububujikwa na machozi.
“Ametaka mwenyewe, asingenitenda ubaya, haya yote yasingetokea na kama angekataa kunisaidia nisingemfahamu Jamal…” ndiyo maneno pekee aliyoongea Kevin na mlango wa chumba ukaonekana kufunguliwa, wakaingia wauguzi wawili wakikimbia huku wakitaka kufahamu ni nini kilikuwa kimetokea.

“Ameanguka tu ghafla, alikuwa mzima kabisa sijui kapatwa na nini?” Mzee Mdoe alidanganya.
“Ameangukaje?”
“Tulikuwa tunasali baada ya kufumbua macho tukamwona akiporomoka…” mama yake Catarina naye alidanganya.
“Basi ngoja tumpime na kuangalia.” Muuguzi akaanza kazi ya kupima mapigo ya moyo huku akitingisha kichwa kuonyesha kwamba hakuyasikia.

“Vipi?”
“Ili kuokoa maisha yake ni lazima apelekwe chumba cha wagonjwa mahututi, huko atakuja daktari kumwangalia na kuona kama anaweza kumsaidia kwani ninavyoona sisikii dalili yoyote ya mapigo ya moyo.” Muuguzi aliongea na kitanda maalum kilichokuwa ndani ya chumba hicho kikasogezwa na kwa kusaidiana wakampandisha Jamal juu yake, safari kuelekea wodi ya wagonjwa mahututi ikaanza mzee Mdoe akifuata kwa nyuma.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia kesho katika Gazeti la Championi Jumamosi.

SOCIAL MEDIA ZETU:

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE: @shigongotz

1 Comment
  1. neema mikey says

    na aende tu jela huyo kevin,nmejikuta namchukia ghafla ilhali jamal ndo mwenye makosa

Leave A Reply