Mkwabi: Bosi Mpya Simba Achukue Tahadhari

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Swed Mkwabi ambaye alitangaza kujiuzulu hivi karibuni, ametoa tahadhari kwa mwenyekiti mpya atakayepata dhamana ya kuiongoza klabu hiyo baada ya kuchaguliwa kwa kudai anatakiwa kuwa makini kutokana na mfumo uliopo hivi sasa.

 

Mkwabi aliachia ngazi ndani ya Simba, wiki iliyopita kwa kile kilichodaiwa mvutano uliokuwa ukijitokeza ndani ya bodi lakini mwenyewe alisema ni sababu za biashara zake binafsi.

 

Uongozi wa Simba upo katika mchakato wa kufanya uchaguzi mwingine ili kuziba nafasi ya Mkwabi ambaye aliingia madarakani Novemba 4, mwaka jana akiwa na wajumbe saba waliounda bodi ya wakurugenzi pamoja na wale waliotoka upande wa mwekezaji Mohamed Dewji ‘Mo’ ili kuunda kampuni.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkwabi alisema kutokana na mfumo wa mabadiliko ulivyo ndani ya Simba kwa sasa ni vyema kiongozi mpya atakayepata nafasi hiyo ahakikishe anafanya kazi kwa umakini zaidi bila kuyumba.

 

“Busara zangu ndizo zilizonifanya niamue kuachia madaraka ndani ya Simba, lakini nitaendelea kuwa mwanachama mtiifu kwa kuhudhuria vikao vyote vya wanachama watakapohitajika na hata mkutano mkuu.

 

“Kwa sasa ni mapema mno kumzungumzia kiongozi mpya ajae ndani ya Simba lakini ningependa kutoa ushauri wangu kwa kiongozi mpya kuwa anatakiwa awe makini na uongozi wake kwani, mfumo wa Simba kwa sasa unahitaji umakini, anahitaji umakini zaidi katika kutekeleza majukumu yake,” alisema Mkwabi.


Loading...

Toa comment