The House of Favourite Newspapers

Mkwasa: Simba SC Hawawezi Dk 90 za Mshike Mshike

0

CHARLES Boniface Mkwasa, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga kwa sasa amegeuka kuwa shujaa baada ya kuiongoza timu yake iliyokuwa haipewi nafasi ya kupata pointi hata moja mbele ya Simba, kupindua meza kibabe na kusepa na pointi moja katika mazingira ambayo yaliwaacha hoi mashabiki wa Simba.

 

Kwenye mechi ya watani wa jadi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Simba ikiwa na mastaa wake wengi wakiongozwa na Meddie Kagere, Deo Kanda, Francis Kahata, Aishi Manula na John Bocco waliambulia pointi moja mbele ya Yanga iliyokuwa na nyota wengi wapya kwa mara ya kwanza ikiwa ni pamoja na Haruna Niyonzima, Adeyum Suleimani, Ditram Nchimbi ambao walionyesha ukomavu uwanjani.

 

Sare ya kufungana mabao 2-2, Mkwasa hajaipenda ila alichofurahishwa ni namna wachezaji walivyotimiza majukumu uwanjani kwa kushambulia kwa kasi na kuanza kuyapunguza mabao yaliyofungwa na Kagere dakika ya 42 kwa penalti na lile la Deo Kanda dakika ya 47.

 

Ndani ya dakika chache walifunga la kwanza kupitia kwa Mapinduzi Balama akiwa nje ya 18 dakika ya 50 na la pili kupitia kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyejifunga dakika ya 53.

 

Championi Ijumaa limefanya mahojiano na Mkwasa kuhusu hali ya kikosi chake baada ya kupewa timu akipokea mikoba ya Mwinyi Zahera ambaye alipigwa chini kutokana na kuwa na matokeo mabovu kwenye mechi zake za ligi kuu pamoja na zile za kimataifa, huyu hapa anafunguka:

 

“Ligi yetu ya Bongo ina mambo mengi ambayo yanatokea ila ukienda nayo kichwakichwa itakuwa ngumu kuyafikia mafanikio, kuna mambo mengi ya kufanyia kazi ili kuweka usawa kwenye ligi yetu.

 

UNADHANI KIPI KINAIBEBA TIMU YAKO?

“Wachezaji wangu wanajua namna ya kufanya wakiwa ndani ya uwanja. Wanajituma na kufanya kazi bila kusukumwa, jambo ambalo linanishangaza wakati mwingine hata mimi ila ni kitu kizuri kwangu, kwao na mashabiki.

 

KIPI KILIKUWA KIGUMU KUKUPA MATOKEO DHIDI YA SIMBA?

“Mnapokutana wakubwa ni lazima kuwe na presha na ushindani mkubwa kwa kila timu. Tulifanya pale ambapo tuliweza na kupata kile ambacho tulikipata hakuna kilichoharibika kwa kuwa ni matokeo ambayo yalipangwa na Mungu.

 

ULIKUBALI KUPATA SARE YA MABAO 2-2?

“Hapana, nilihitaji kushinda ili kuendeleza ile kasi ambayo tulikuwa nayo na tulifanya jitihada kubwa kupata sare ambayo imetufanya tuambulie pointi moja pekee.

 

UNAIZUNGUMZIAJE TIMU YA SIMBA?

“Ni moja ya timu bora ila haina uwezo wa kuwa bora ndani ya dakika tisini, jambo ambalo linawamaliza wenyewe wakiwa ndani ya uwanja. Hawana ule uwezo wa kuhimili mikikimikiki ndani ya uwanja kwa dakika zote tisini hapo ndipo ambapo niliweza kuwatega.

 

“Wao walikaa muda mrefu kwenye kambi zaidi ya mwezi ila Yanga hatukuwa katika timu kwa muda mrefu. Wachezaji wengi niliowatumia ni wale ambao tumewasajili dirisha dogo ili waongeze nguvu kikosini na wamefanya kazi.

 

UWEZO WA NYOTA WAPYA UNAUZUNGUMZIAJE?

“Ukiachana na Haruna Niyonzima yeye ni mzoefu na anajua kucheza mechi ngumu ila hawa wengine akina Ditram Nchimbi, Adeyum, Ikpe bado hawakuwa na uzoefu ila wameonyesha kile kitu nilichowafundisha japo kwa muda mfupi.

 

KWA NINI KIPINDI CHA KWANZA KILIKUWA KIGUMU KWENU?

“Aina ya timu ambayo nacheza nayo ilikuwa ni ile inayotegemea kupewa penalti, sasa hapo inakuwa ngumu kutafuta ushindi ndiyo maana kipindi cha kwanza niliwaacha wacheze kisha nikabadili mipango kipindi cha pili na tukapata matokeo, muda ungetosha tulikuwa na nafasi ya kuongeza bao lingine kwani wao walikosa ubora ‘fitnesi’ kipindi cha pili.

 

HESABU ZAKO KWA SASA ZINAKWENDAJE?

“Baada ya kumalizana na Simba sasa tumegeukia michuano ya Mapinduzi Zanzibar, mashabiki watupe sapoti katika hili,” anamaliza Mkwasa ambaye timu yake ilitarajiwa kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar, jana usiku katika nusu fainali ya Mapinduzi Cup.

LUNYAMADZO MLYUKA, DAR ES SALAAM

Leave A Reply