The House of Favourite Newspapers

Mmoja wa Waasisi wa ACT Wazalendo Atimkia NCCR Mageuzi – Video

0

NDUGU wana habari, kwa majina naitwa Wiston Mogha niliyekuwa mwanachama wa ACT- Wazalendo. Mnamo Machi 18, 2020 nilijivua uanachama wa ACT-Wazalendo na kuujulisha umma wa watanzania kupitia mitandao ya kijamii juu ya maamuzi yangu hayo.

 

Katika andiko langu la kuujulisha umma nilieleza kuwa nilikuwa kijana mdogo kuliko wote kwenye harakati za uasisi wa chama. Hicho. Lakini pia nilieleza shukrani zangu kwa chama, viongozi na wanachama wa ACT -wazalendo kwa muda wote tuliokuwa pamoja.

 

Narejea kusema nimeondoka nikiwa na kumbukumbu nyingi za matumaini na masikitiko. Kubwa zaidi naondoka kutokana na kujipa fursa ya kufikiri msingi wa kesho yangu kama kijana na hatma yangu kwenye siasa za mageuzi.

 

Ndugu wanahabari, leo nimewaita kuueleza umma kupitia kwenu sababu tatu za kuondoka ACT:

1. Ni kweli niligombea Uenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa na sikushinda ila siondoki kwa sababu ya kushindwa. Isipokuwa sikuridhika na yaliyotokea kwenye uchaguzi yaliyopelekea mimi kushindwa.

 

Yanaweza yakawa ni mambo ya kawaida kwenye chaguzi za vyama vingine ila kwa kilichokuwa chama changu hayakuwa mambo ya kawaida ambayo tuliyataka yatokee kwenye chaguzi zetu. Hii ni kwa sababu baadhi ya misingi tuliyojiwekea wakati wa uanzishaji chama hicho ni kulinda utu na kuipigania demokrasia.

 

Ndiyo maana kabla ya uchaguzi nilipiga kelele sana kwenye chama nikitaka demokrasia tunayoihubiri itendeke.

 

Kwenye nafasi niliyogombea, wagombea wote tulikuwa vijana wa chama, lakini kitendo cha viongozi wakuu kushiriki moja kwa moja kwenye uchaguzi wetu kwa kusema fulani ndiye hitaji la chama na fulani anatumika na CCM au fulani ni mtumishi wa usalama wa Taifa, Kitendo kile ni kibaya na kinatengeneza makundi kwa vijana ambao bado kwa sehemu kubwa sana tunahitajiana kesho. Sisi bado vijana wadogo na wote ndoto zetu ni kushiriki kwenye kuongoza historia ya mabadiliko ya nchi yetu.

 

2. Yalitokea kwenye uchaguzi yamejenga tafsiri ya wazi ya nafasi yangu kwenye chama, Mwonekano wangu kwa viongozi na taswira iliyojengwa na viongozi wakuu kwa wanachama wenzangu.

 

Sikuwa Na budi bali kujieweka pembeni kwa kuwa mambo haya hajaanza leo na kadri tunavyoendelea yanazidi kuchafua uanachama na utu wangu mpaka kufikia hata rafiki zangu wa karibu kuanza kuwa na mashaka na mimi.

 

3. Septemba 24, 2014 nilitangaza kwenye vyombo vya habari juu ya dhamira yangu kutaka kugombea ubunge katika Jimbo la Kigoma Mjini. Baada ya kutangaza tu nilifuatwa na viongozi kadhaa na marafiki wakiniomba kukaa pembeni ili kumwachia Zitto.

 

Ilipofika mwaka 2015 baada ya Zitto kujiunga rasmi na ACT-Wazalendo, tukiwa mkoani Shinyanga kwenye ziara tulizungumza na akaniambia dhamira yake ya kugombea ubunge Kigoma mjini na akaniomba mimi nigombee udiwani ili kuendelea kujifunza kwa ukaribu. Kwa heshima na mapenzi kwa kiongozi wangu nilikubali.

 

Mwaka 2015 niligombea udiwani Kata ya Mwanga Kusini Manispaa ya Kigoma Ujiji lakini nilishindwa kwa idadi ya kura chache kabisa na moja ya sababu ikiwa ni viongozi wangu kumtaka mgombea wa CCM badala yangu.

 

Viongozi walioniomba na kunishawishi wakanifanya kama chambo na njia ya kunidhalilisha kwa kuhakikisha nashindwa udiwani ili ionekane sikuwa mtu sahihi hata kuuwazia ubunge. Mambo haya yote yamenifanya nione ni bora kuchukua tahadhari kwa kuiangalia kesho yangu na kwa sababu hizo natangaza rasmi kujiondoa ACT-Wazalendo.

 

Kwa kuwa mimi ni mwanasiasa tena kijana ambaye bado nina maisha marefu ya kuitumikia nchi yangu, sitaweza kustaafu siasa kwenye umri mdogo nilionao. Hivyo baada ya maamuzi ya kujivua uanachama wa ACT-Wazalendo, nimeamua kujiunga na chama cha NCCR-Mageuzi.

 

Kwa nini NCCR- Mageuzi na siyo chama kingine?

1. Nimepitia katiba za vyama mbalimbali vya siasa na kuridhika na muundo wa NCCR-Mageuzi

2. Itikadi yao ya UTU ndiyo niliyokosa kuiona huko nilipotoka na ndicho kitu ambacho moyo wangu unataka kukiishi kwa sasa.

3. Utayari wa viongozi na wanachama wa NCCR kunipokea ili nami nitoe mchango wangu kwenye ujenzi wa chama hiki. Hivyo NCCR-Mageuzi ni sahihi kwangu kujiunga nao.

 

BAADA ya tafakuri ya kina na muda wangu wa zaidi ya miaka 10 niliyokuwepo ndani ya mfumo wa vyama vingi, Kujiunga kwangu na NCCR Mageuzi itakuwa ni kupata jukwaa jipya la kuendeleza yale ninayoyamini katika siasa za UTU na uzalendo wa kweli wa kumletea maendeleo mtanzania mnyonge.

 

Najiunga na NCCR Mageuzi nikiwa na matumaini makubwa nipo kwenye Chama salama chenye kuwatumikia wananchi na siyo kumtumikia mtu na kutekeleza kile anachotaka badala ya maamuzi ya wote.

 

Naamini uwepo wangu ndani ya NCCR Mageuzi ni maamuzi thabiti yenye kuamsha hisia za kuwakomboa wanyonge, ambapo Chama hiki chini ya Mwenyekiti James Mbatia kimeamua na kina dira ya dhati ya kuwakomboa wananchi wa Tanzania.

 

Najivunia kujiunga na Chama ambacho tutaendelea kukijenga na chenye mwelekeo wa kuleta maendeleo hasa wakati huu kuelekea katika uchaguzi mkuu wa 2020, ambapo naamini ni wakati wa kwenda kubadilisha siasa za mkoa wetu na Taifa kwa ujumla.

 

Siasa za Kigoma sasa zinahitaji uwepo wa Chama mbadala, Chama cha kuwaunganisha na kuwapigania wananchi wetu na kujali shida zao ili kushiriki kwa pamoja kuzitatua. Kigoma yetu italindwa na sisi hasa vijana ambao tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maendeleo yetu na kufika mbali zaidi kutoka hapa tulipo.

 

Nimeshawishika kujiunga na NCCR Mageuzi nikiwa naamini nipo kwenye Chama kilicholeta mageuzi ya kweli ya siasa za ustarabu ambazo kila mtanzania anazipenda na mwelekeo thabiti wa siasa za kimaendeleo kwa wanakigoma, watanzania na si siasa za kimadaraka kama ambavyo vyama vingine vinaeleza.

Shukrani kwa kunisikiliza na
Ahsanteni sana!

Leave A Reply