The House of Favourite Newspapers

MNAHESABU LAKINI…YANGA YAMALIZANA NA ALLY ALLY

YANGA Buana! Jana mchana Simba walitupia picha ya beki wao mpya Mbrazil,Gerson Vieira wakawaambia mashabiki wao wakae mkao. Gerson akaibua mijadala kibao kwenye mitandao ya kijamii. Mida ya jioni Yanga wakamvutia waya beki wa KMC, Ally Ally ambaye ni Mzanzibar na kumwambia; “washa gari fasta njoo klabuni Jangwani.”

 

Akaingia kwenye gari alipofika klabu akakutana na nyomi la mashabiki wakimsubiria wakati anajiulizauliza huku akitafuta upenyo apite fasta watu wasimuone akashangaa mashabiki wakimpigia makofi ya kumkaribisha.

 

Akaingia ofisini akamalizana na viongozi wakatupia kwenye mitandao ya kijamii, wakawauliza watani wao wa jadi; “Mnahesabu lakini?”

 

Yanga imefanikisha usajili wa beki huyo wa kati mbishi wa KMC ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, huku akibebwa juu juu na kukabidhiwa jezi na juzi usiku walifanikisha usajili wa mshambuliaji wa Zesco, Maybin Kalengo.

 

Kwa usajili huo, Yanga wamefikisha wachezaji tisa wapya ambao imewasajili wengine ni Issa Bigirimana ‘Walcott’, Patrick Sibomana, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo, Juma Balinya, Lamine Moro, Selemani Mustapha, Abdulaziz Makame na Ally mwenyewe.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra na kuthibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kuwa beki huyo wamefikia makubaliano nayo mazuri na kusaini mkataba wa miaka miwili. Mwakalebela alisema kuwa, beki huyo amesaini mkataba huo baada ya mazungumzo ya muda mrefu kabla ya kufikia muafaka mzuri na kukubali kusaini mkataba huo kwa dau alilokuwa analitaka ambalo ni siri.

 

“Ni kweli tupo hapa klabuni Jangwani tunamsaini Ally beki wa KMC, lakini hizo taarifa hatukutaka kuzitoa hivi sasa, tulipanga siku ya utambulisho wa wachezaji wetu wapya,”alisema Mwakalebela ambae amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe.

 

“Na amesaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Yanga na tumemsajili Ally kwa mujibu wa mapendekezo ya kocha wetu Zahera (Mwinyi) aliyotuachia kwenye ripoti yake.

 

“Hivyo, usajili wa Ally unafikia jumla ya wachezaji tisa ambao hadi hivi sasa tayari tumemalizana nao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi,”alisema Mwakalebela na kuongeza kuwa; “Pia, jana (juzi) tulimalizana na Kalengo ambaye naye tumeingia makubaliano mazuri ya kusaini mkataba wa miaka miwili Yanga,” alisema Mwakalebela ambaye ni kiongozi wa zamani wa TFF na Mtibwa.

Comments are closed.