The House of Favourite Newspapers

Mo Dewji Ang’ara Orodha ya Mabilionea 20 wa Afrika, Dangote Aongoza

0

Jarida la Forbes limetoa orodha ya mabilionea 20 wa Afrika kwa mwaka 2024 ambapo Mtanzania pekee aliyepo kwenye orodha hiyo, Mohamed Dewji aking’ara kwa utajiri wake kuongezeka kutoka Dola za Kimarekani bilioni 1.5 hadi Dola za Kimarekani bilioni 1.8 na kumfanya ashike nafasi ya 12 katika orodha hiyo.

Orodha ya matajiri wa Afrika mwaka huu, inaongozwa na Aliko Dangote wa Nigeria, ambaye ametajwa kuwa na utajiri wa Dola za Kimarekani Bilioni 13.9, huku kukishuhudiwa kupanda na kushuka kwa matajiri wengi, wengine wakiporomoka na kutoka kwenye orodha ya Mabilionea 20, huku wengine wakipanda na kuingia kwenye orodha hiyo.

Taarifa iliyotolewa na Forbes, imeonesha kwamba kwa jumla, utajiri wa mabilionea wa Afrika, umeongezeka kwa dola za Kimarekani milioni 900, kutoka jumla ya dola bilioni 81.5 kwa mwaka 2023 hadi dola bilioni 82.4 kwa mwaka huu.

Utajiri wa Mo Dewji, umeelezwa na Forbes kuwa ni kutokana na biashara za Kampuni ya Mohadem Enterprises Tanzania Limited iliyoanzishwa miaka ya 1970, aliyoirithi kutoka kwa wazazi wake.

METL inafanya biashara za kuzalisha unga wa chakula, vinywaji, mafuta ya kupikia na malighafi na bidhaa za nguo, ikiwa ndiyo kinara katika maeneo ya Afrika Mashariki, Kusini na Afrika ya Kati, ikifanya biashara zake katika nchi 10 za Kiafrika, ikiwemo Uganda, Ethiopia na Kenya na nyinginezo.

Kampuni hiyo imeajiri zaidi ya watu 40,000 katika maeneo yote inakoendesha shughuli zake za uzalishaji, na inatajwa kuwa ndiyo kampuni tajiri zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Bilionea Femi Otedola wa Nigeria, ambaye alionekana mara ya mwisho kwenye orodha ya Forbes ya Afrika mwaka 2017 alipokuwa na hisa kubwa katika kampuni ya usambazaji wa mafuta ya Forte Oil, amerejea kwenye orodha hiyo, akishika nafasi ya 19.

Kwa upande wa kinara wa orodha hiyo, Aliko Dangote wa Nigeria, utajiri wake umeongezeka kwa dola milioni 400 na kufikia dola bilioni 13.9, akishika nafasi ya kwanza kwa mwaka wa 13 mfululizo.

Leave A Reply