The House of Favourite Newspapers

Molinga Apewa Mkono Wa Kwaheri Yanga SC

0

TAARIFA zinasema kuwa, Yanga imeamua kuonyesha waziwazi kuachana na straika wake David Molinga baada ya jana kumuacha kwenye msafara wa kikosi cha timu hiyo kilichosafiri kwenda Shinyanga kuifuata Mwadui FC.Jumamosi hii, Yanga itacheza dhidi ya Mwadui ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.

 

Meneja wa Yanga, Abeid Mziba, ameliambia Spoti Xtra kuwa: “Kikosi kipo vizuri, wachezaji waliobaki ni Lamine Moro, Ally Mtoni ‘Sonso’, Abdulaziz Makame, Andrew Vincent ‘Dante’ na Rafael Daud ambao wanaumwa. All Ally na Eric Kabamba wameachwa kwa sababu ni mpango wa mwalimu kuwatumia wakati ujao.

 

“Papy Tshishimbi bado hajawa sawa kwa mujibu wa daktari, hivyo ameachiwa program maalumu akiifanya ili arejee kwenye

 

ubora wake.“Kuhusu Bernard Morrison na Metacha Mnata, watajiunga na kikosi kesho (leo Alhamisi) asubuhi wakitufuata kwa ndege.“Najua unahitaji kujua kuhusu Molinga, ila ukweli ni kwamba hajaachwa makusudi, alikuwa kwenye mpango wa mwalimu ila aliamua kubaki mwenyewe, hakuna tatizo lililopo ni maamuzi yake.”

SIMBA YAHUSISHWA KUMUWANIA

Wakati Molinga akitajwa huenda akaachwa na Yanga huku mkataba wake ukitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, Simba imekuwa ikitajwa mara kwa mara kwamba inaiwania saini yake ili kuimarisha safu yake ya ushambuliaji ambayo kwa sasa ina John Bocco na Meddie Kagere pekee.

 

Molinga ndiye kinara wa mabao wa Yanga katika Ligi Kuu Bara akifunga nane msimu huu ukiwa ni wa kwanza kuichezea timu hiyo. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.Rekodi zinaonesha kuwa, Molinga amecheza mechi 20 za Ligi Kuu Bara msimu huu akitumia dakika 1,402.

 

Dakika zake hizi hapa; Polisi Tanzania (dk 90), JKT Tanzania (dk 60), Alliance FC (dk 90), Ruvu Shooting (dk 90), Coastal Union (dk 90), Mbao FC (dk 74), Ndanda (dk 90), KMC (dk 90), Mbeya City (dk 90), Tanzania Prisons (dk 90), Biashara United (dk 45), Azam FC (dk 90), Singida United (dk 67), Mtibwa Sugar (dk 68), Lipuli (dk 29), Ruvu Shooting (dk 68), Mbeya City (dk 64), Prisons (dk 30) na Mbao (dk 63), KMC (24).

 

SABABU ZA KUACHWA

Vyanzo kutoka ndani ya Yanga vinasema kuwa, Molinga hakubaliki na benchi la ufundi la timu hiyo tangu kuondoka kwa Kocha Mwinyi Zahera ambaye ndiye alimsajili.

 

MSIKIE MWENYEWE

Alipotafutwa Molinga ili kuweka sawa sakata lake la kushindwa kusafiri na timu, alisema: “Nataka nikanushe hii habari kwamba nimegoma kusafiri na timu, kwanza niwakumbushe kitu cha pekee kilichonileta Tanzania ni mpira na kazi yangu ndio hiyo.

 

“Sasa iko hivi, tangu timu imeanza mazoezi sijawahi kukosa na nafuata program za mwalimu vizuri, lakini jana (juzi) listi ilitoka na mimi jina langu halijakuwepo, sasa itasemekana vipi nimegoma. Kama ndio hivyo muulizeni kocha ndiye alitaja listi yake.”

Leave A Reply