The House of Favourite Newspapers

MONDI FANYA YOTE LAKINI… MHESHIMU SANA WEMA

Nasibu Abdul ‘Diamond’

MOJA kati ya mtihani mkubwa ambao watu wengi huwa wanafeli duniani ni ule wa kupata mafanikio na kuwakumbuka wale ambao walitoa mchango katika mafanikio yao. 

 

Waswahili wanakwambia mpe mtu pesa uijue tabia yake. Msemo huo una maana kwamba, utazijua tabia mbaya za mtu pale anapopata mafanikio.

 

Anapokuwa hana, huwezi kumjua kama ana kiburi au kama ni mkorofi au pengine ni mtu wa ‘totoz’ kupita maelezo. Nikirejea kwenye msingi wa hoja yangu, leo namzungumzia mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ambaye nafahamu alikotoka, alikopita na anapoelekea.

 

Diamond amechipukia mwaka 2013 kwenye gemu, mambo yakamnyookea na hatimaye akafika kwenye ‘levo’ ambayo nathubutu kusema ana mafanikio makubwa kuliko wasanii wengi hata wale ambao walianza muziki kabla yake. Wakati akiwa kwenye kipindi cha ‘kuganga’ njaa kwenye gemu, aliingia kwenye uhusiano na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu ambaye nyota yake ilikuwa juu.

Wema alikuwa staa kuliko Diamond. Wema alikuwa na mvuto katika jamii, Wema alikuwa Wema kweli kwani mbali na kuwa na wafuasi wengi, alikuwa na mvuto si wa kitoto. Mapedeshee, watu wenye fedha zao walikuwa wakipi shana kumuwinda lakini mtoto wa kike aliamua kutulizana na kumpa moyo wake wote Diamond.

 

Kumbuka wakati huo Diamond alikuwa ndio kwanza anaanza ‘kusumbua sumbua’ na ‘kasingo kamoja’ kalikoitwa Kamwambie. Kutokana na jina alilokuwa nalo Wema wakati huo, Diamond alikuwa hafananii kuwa na Wema.

 

Wema ni kama alikuwa anamsaidia hivi, Diamond hata kifedha hakuwa na mtonyo wa kummiliki Wema. Nakumbuka kipindi hicho ndio Diamond alifanikiwa kuzichangachanga akawa amepanga upande wa nyumba maeneo ya Meeda jijini Dar, akiishi na mama yake mzazi Sanura Kassim ‘Sandra’.

Wema alikubaliana na changamoto hiyo, alikubali kumsapoti Mondi katika hali yoyote kwani alilazimika kujibanabana na ‘mkwewe’ katika nyumba hiyo. Akawa anamsapoti kwenye shoo zake, akawa anambusti sana kwenye vyombo vya habari hususan Global Publishers kwani Magazeti Pendwa yalikuwa yakimuwinda Wema na ndio Diamond akawa anapitia humohumo, anaonekana.

 

Uzuri ni kwamba Diamond naye alikuwa mtu wa kujiongeza, akawa ‘anajibusti’ naye kwenye matukio mbalimbali, yakawa yanamfanya azungumzwe zaidi. Lakini tazama hata katika hayo matukio mfano lile la mwaka 2014 la uchukuaji wa tuzo pale Mlimani City, Wema alionekana kumsapoti Mondi na hata ukitazama picha zao wakati huo, utakubaliana na mimi kwamba Mondi hakuwa akiendana na Wema.

Achana na hilo, kuna matukio ya bethidei ambazo zilikuwa zikitokea mwaka hadi mwaka, Wema alionekana kumuunga mkono na kumfanya Diamond awe juu zaidi, vyombo vya habari vikawa vinaripoti habari yao. Wema alikuwa muwazi kwa Diamond.

 

Kwa kuwa Global tulikuwa tukiwafuatilia, Wema alionekana kuwa muwazi sana kwa Mondi. Hakutaka kuchanganya mambo kwamba awe na Mondi halafu awe na mtu mwingine. Alipenda kuanika uhusiano wake wazi na dunia nzima ilikuwa inajua.

 

Niamini mimi, kutokana na penzi la dhati alilokuwa nalo Wema, ilikuwa ni vigumu sana kumuacha Diamond na hata ilipotokea mkali huyo wa Bongo Fleva alivyodaiwa kuchepuka, bado walitofautiana kwa muda na kisha wanarudiana. Wema huyuhuyu ndio anatajwa kuwa mwalimu mzuri wa Diamond katika suala zima la lugha ya Kingereza huku mtangazaji Penniel Mungilwa ‘Penny’ akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Wema.

Wema alikuwa jasiri wa kumzungumzia vizuri Diamond, hakuwa na kisirani, hata pale walipokuja kuachana jumla na Diamond kufanya maisha na warembo wengine akiwemo Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ aliyemzalia watoto wawili, Hamisa Mobeto aliyemzalia mtoto mmoja, Penny na wengineo bado aliendelea kushirikiana naye.

 

Kwenye matukio yake makubwa, hadi leo Wema amekuwa akiendelea kumsapoti kiroho safi hivyo kwa namna yoyote, Diamond anapaswa kumheshimu sana Wema. Ni mwanamke mwenye roho ya peke yake

Makala: Erick Evarist

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKI

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.