The House of Favourite Newspapers

Morrison Kumrudisha Chirwa Yanga SC

0

WAKATI michuano ya Ligi Kuu Bara ikiwa imesimama kwa muda kutokana na ugonjwa wa Corona, mshambuliaji wa kimataifa wa Azam FC, Mzambia, Obrey Chirwa, ameanza kuhusishwa na mipango ya kutaka kurudi kwenye timu yake ya zamani ya Yanga.

 

Chirwa ambaye kwa sasa ni mmoja wa washambuliaji wa kutumainiwa wa Azam, anadaiwa kuwa tayari ameshaanza mipango hiyo ili msimu ujao aweze kuungana na Mghana, Bernard Morrison katika safu ya ushambuliaji ya Yanga.

 

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo Championi Jumatatu limezipata zimedai kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Luc Eymael pia amebariki mpango huo baada ya kuvutiwa na uwezo wake aliouonyesha uwanjani wakati timu hiyo ilipopambana na Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

“Mkataba wa Chirwa na Azam umebakiza miezi mitatu tu kabla ya kumalizika, unamalizika mwezi Juni, kwa hiyo hivi sasa anaruhusiwa kufanya mazungumzo na timu yoyote inayomtaka.

 

“Kwa hiyo kutokana na hali hiyo, tayari tumeshanza mazungumzo naye ya kutaka kumrudisha kikosini, kwani ni mchezaji mzuri na anayeijua vyema ligi yetu.

“Lakini pia yeye mwenyewe anataka kurudi Yanga kwani anadai hana faraha na maisha katika kikosi cha Azam,” kilisema chanzo hicho cha habari.

 

Alipotafutwa Chirwa ili aweze kuzungumzia hilo hakupatikana lakini kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema: “Ni kweli tumeshaanza harakati za usajili kwa ajili ya msimu ujao lakini kwa sasa sipo tayari kusema chochote juu ya hilo ila ninachoweza kusema ni kwamba tumeanza na Morrison tayari tumeshamwongeza mkataba mwingine wa miaka miwili.”

 

Ikumbukwe tu kuwa wakati Chirwa akiitumikia Yanga katika mechi 62 alizoitumikia timu hiyo, alifanikiwa kufunga mabao zaidi ya 30 na msimu huu akiwa Azam FC amefunga mabao 8 na kutoa asisti tatu.

 

SWEETBERT LUKONGE, Dar es Salaam

Leave A Reply