MPENZI WANGU SARAFINA-14

Bianca aliendelea kumfuatilia Richard, hakuwa radhi kuona akimkosa mwanaume huyo ambaye kwake alikuwa kama mwanaume wa maisha yake. Alikuwa mgumu lakini kila siku alijitahidi kumfikishia ujumbe kwamba alikuwa akimpenda sana.

Richard alikuwa akikataa, aliyaogopa mapenzi, hakutaka kuwa na msichana yeyote kwani kumbukumbu kuhusu Sarafina zilimjia kichwani mwake na kuyachukia mapenzi hayo. Hakutaka kuyapa nafasi, alitaka kubaki peke yake kwa kuamini kwamba kungekuwa na siku moja ambayo angefurahi kwa kumpata mwanamke wa maisha yake lakini si Bianca.

Siku zikakatika, ukaribu wa Bianca kwa Richard ukazidi kushamiri. Wakati mwingine mwanaume huyo alikuwa akichukia sana, hakutaka kuwa karibu na msichana huyo lakini alishindwa, kila alichokuwa akikifanya, Bianca alikuwa pembeni yake.

Bianca akawa hakwepeki, alimtawala kila sehemu, ndiye alikuwa mtu ambaye alimpigia kumpigia simu huku akiwa wa mwisho kuzungumza naye kwa njia ya simu. Hakutaka ukaribu na msichana huyo lakini kikafika kipindi akawa hana jinsi, akakubaliana na ukweli uliokuwepo kwamba awe tu na msichana huyo.

Akamkubalia kuwa mpenzi wake, wakawa pamoja na mapenzi kuanza kama ambavyo msichana huyo alivyotaka. Kila siku ilikuwa ni lazima wawili hao kugandana kama ruba. Uhusiano huo wala haukuwa siri kwani baada ya siku tatu tu chuo kizima kikagundua kwamba wawili hao walikuwa kwenye uhusiano mzima wa mapenzi.

Siku zikakatika, mwaka wa kwanza ukaondoka, Richard hakutaka kurudi nchini Tanzania, moyo wake ulikuwa na chembechembe za maumivu kutoka kwa msichana Sarafina ambaye alimuumiza sana, msichana ambaye alimtesa usiku na mchana.

Hakutaka kuonana naye, alitamani kuona akiendelea na maisha yake akiwa na Bianca, msichana ambaye alijitolea kwa asilimia mia moja kuwa naye katika maisha yake yote. Richard na Bianca walichukua miaka mitatu kusoma nchini Marekani na ndipo wakarudi nchini Tanzania.

Kitu cha kwanza kabisa walichokifanya kilikuwa ni kutambulishana kwa wazazi kwamba walikuwa wapenzi, wazazi wakakubaliana nao, wakawapa baraka zao na kisha wawili hao kuvalishana pete na hatimaye kuingia kwenye uchumba.

“Nitataka nikuoe, uwe mke wangu wa ndoa,” alisema Richard, alikuwa akimwambia mchumba wake Bianca aliyeonekana kuwa na furaha tele, kwake, kuwa na msichana huyo ndani ya nyumba yake ndicho kitu alichokuwa akikihitaji kuliko vyote katika maisha yao.

Hilo halikuwa la kusubiri, kilichotokea baada ya miezi kadhaa ni kufunga ndoa na hatimaye kuwa mume na mke kitu ambacho kilimpa furaha kila mmoja.

Maisha yao yakabadilika kabisa, kila mmoja alionekana kuwa na furaha, katika maisha yao, wote walitamaniana, ukaribu ukaongezeka, wakazoeana kupita kawaida kiasi kwamba kuna kipindi wakawa wakiishi kama marafiki hali iliyoyafanya mapenzi yao kudumu zaidi.

Wakapanga kuwa na watoto na baada ya miaka miwili ya ndoa ndipo wakaamua kumtafuta mtoto huku tayari wakiwa na miaka mitano tangu walipokutana chuoni. Kupata mimba kwa Bianca hakukuwa tatizo lolote, kwani tangu waamue, ndani ya miezi miwili akaanza kuhisi dalili zote za kuwa na mtoto tumboni mwake.

Hilo lilimpa furaha kila mmoja, wakasubiri na baada ya miezi michache kwenda hospitali ambapo daktari aliwaambia kwamba walitegemea kupata mtoto wa kike kitu kilichomfanya kila mmoja kufurahi.

“Unasemaje?” aliuliza Richard huku akiwa haamini.

“Mtoto wa kike.”
“Ataitwa Claire! Mke wangu naomba usinipinge katika hili,” alisema Richard huku akiachia tabasamu pana usoni mwake.

“Wewe tu!”

Wakaanza kupanga mipango juu ya mtoto huyo, walikuwa wakimpenda hata kabla hajazaliwa hospitalini. Wakafanya sana shopping, wakanunua vitu vingi kwa ajili ya mtoto huyo. Wakawaambia marafiki zao kwamba hatimaye walikuwa wakienda kupata mtoto wa kike hivyo wangefanya sherehe moja kubwa ambayo ingewafanya waandishi kuiandika sana na kutawala mno katika mitandao ya kijamii.

Siku zikaenda mbele, miezi ikakatika na hatimaye miezi tisa kutimia, siku ambayo Bianca alitakiwa kujisikia uchungu akaanza kujisikia hivyo. Alipiga kelele chumbani na kwa sababu kulikuwa na mfanyakazi wa ndani, akamsaidia na mtunza bustani na kumuingiza ndani ya gari huku damu zikivuja.

Aliogopesha, kwa jinsi alivyokuwa akilia, wakajua kulikuwa na tatizo kubwa, haikuwa kawaida kwa mwanamke kulia kama alivyofanya, huku Mrisho, kijana wa bustani akiendesha gari, dada wa kazi akampigia simu Richard na kumweleza kilichokuwa kikiendelea.

“Mpo wapi?”
“Tupo njiani tunakwenda Ocean Road,” alijibu dada wa kazi.

“Nakuja!”

Hakutaka kuchelewa, alikuwa na kazi nyingi ofisini lakini hazikuonekana kuwa na umuhimu wowote ule, kitu alichokuwa akikifikiria kilikuwa ni mke wake, akaacha kila kitu na kwenda hospitalini huko.

Siku hiyo alionekana kuwa tofauti, moyo wake ulikuwa na majonzi kuliko siku nyingine, alijitahidi kujifurahisha kwamba alikuwa akienda kupata mtoto lakini moyo wake haukuwa na furaha hata kidogo.

Aliendesha gari kwa hofu kubwa, alipofika katika hospitali hiyo, akateremka na kwenda ndani ambapo huko akawakuta dada wa kazi na kaka wa bustani ambapo alipowauliza, akaambiwa kwamba hali ya Bianca haikuwa nzuri.

“Imekuwaje?” aliuliza huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Alipoteza damu nyingi mno,” alijibu Mrisho.

“Unasemaje? Mungu wangu! Amejifungua?” aliuliza Richard huku akitembeatembea, hata kukaa kwenye kiti alicshindwa.

“Bado! Madaktari ndiyo wanafanya kazi yao ndani,” alijibu Mrisha.

Alikaa mahali hapo huku akiwa na hofu tele, bado moyo wake ulikuwa na hofu, alihisi kabisa kwamba kulikuwa na tatizo lililokuwa njiani kutokea, akapiga magoti na kuanza kumuomba Mungu huku kijasho chembamba kikimtoka.

“Mungu! Ninahitaji mtoto! Mungu naomba umuongoze mke wangu ajifungue salama,” alisema Richard huku akipiga kelele. Kadiri dakika zilivyozidi kwenda mbele ndivyo ambavyo moyo wake ulikosa amani zaidi.

****

Vijana wa David waliogopa, walimfahamu bosi wao, hakuwa mtu wa mchezo, aliposema kwamba alihitaji kitu fulani, haraka sana alitaka kupata majibu ya kitu hicho. Alichukia kufanyiwa uhuni wa kuibiwa laptop yake na pesa zake, alikasirika, hakutaka kuona mwizi huyo akiendelea kuishi, alichokitaka ni kumuua kama malipo kwa kile alichokuwa amekifanya.

Vijana wakaingia mitaani, kwa kuwa Ibrahim alikuwa akijulikana sana kama muokota chupa, hata walipoanza kumtafuta hakukuwa na ugumu wowote ule, ilikuwa ni kumuulizia kijana aliyekuwa akiokota chupa na hivyo kuonyeshewa mahali alipokuwa akiishi.

“Ni mtoto wa mitaani?” aliuliza Jumanne, mmoja wa wanaume waliotumwa na David.

“Ndiyo!”
“Anauza chupa wapi?”
“Ilala Mabondeni!”
“Twende!”

Hawakutaka kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima waende kumtafuta, waliamini kwamba kama kweli alikuwa ameelekea huko ilikuwa ni lazima wampate. Njiani walikuwa wakizungumza, walimuona mkuu wao alivyokuwa na hasira, siku hiyo hasira zake zilikuwa tofauti na siku nyingine, alivimba, aliwaka, alichokuwa akikihitaji ni vitu vyake tu.

Jumanne na mwenzake, Fred wakafika mpaka Ilala Mabondeni, hapo, kulikuwa na sehemu iliyokuwa na milima mikubwa ya chupa, wakawafuata vijana fulani waliokuwa mahali hapo na kuwauliza kuhusu Ibrahim, kijana aliyekuwa akiokota chupa maeneo ya Posta.

“Huko Posta hawaruhusu watu kwenda kuokota, sasa iweje huyo aende huko?” aliuliza kijana aliyekuwa mahali hapo.

“Hatujui, ila alikwenda huko. Unamjua?” aliuliza Jumanne.

“Hapana! Wapo wengi sana, au labda mngenionyeshea picha zake,” alisema kijana huyo.

Hawakutaka kumficha, waliona kwamba huyo ndiye angekuwa msaada wao mkubwa. Wakamwambia kilichokuwa kimetokea, jinsi kijana huyo alivyotumia nafasi ya kuokota chupa na kuwaibia kiasi kikubwa cha pesa.

“Huyo atakuwa Ibra!” alisema kijana huyo.

“Kwa nini?”
“Alikuja hapa na kusema kwamba haokoti tena chupa! Maisha yake yanakwenda kuwa ya kitajiri,” alisema kijana huyo.

“Tutampata wapi?”
“Nendeni Ilala Bungoni, kule kulipokuwa na Chuo cha DSJ, kuna nyumba ina rangi ya Bluu, hapo kuna watoto wengi wa mitaani, yupo hapohapo,” alisema kijana huyo.

Jumanne na Fred hawakutaka kupoteza muda, wakaingia ndani ya gari na kisha kuanza kuelekea huko walipoelekezwa. Njiani walikuwa na presha kubwa, waliambiwa kwamba kama itawezekana wamuue mtu huyo kwani hakutakiwa kabisa kuishi kutokana na kile alichokuwa amekifanya.

Hawakuchukua muda mrefu wakafika mahali hapo, kama walivyoambiwa kulikuwa na watoto wengi wa mitaani, wakaanza kuangalia huku na kule, hawakujua Ibrahim alikuwa yupi kwani hata kamera za CCTV walizoonyeshwa hawakumuona vizuri.

Wakamuita msichana mmoja na kumuuliza, huyo ndiye aliyewaambia kwamba Ibrahim alikuwa ameondoka na demu wake kuelekea Magomeni kwa lengo la kupanga chumba na muda huo hawakuwa mbali, kama wangekimbia kuelekea Ilala Boma wangekutana nao njiani.

Wakarudi garini na kuanza kuelekea huko Ilala Boma, njiani walikuwa wakiangalia huku na kule, walipofika Amana, kwa mbele wakawaona watoto wawili, walikuwa wachafuwachafu na walikuwa wakitembea kwa mwendo wa kasi, hivyo kuanza kuwafuata.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa.

Toa comment