The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-18

0

Alianza taratibu sana lakini mwisho wa siku David akaanza kuzoea, akawa mtumiaji mzuri wa madawa hayo, alifanya kwa siri, hakutaka Gloria ajue kilichokuwa kikiendelea. Kila alipokuwa akielekea kazini, alijifungia ofisini na kuanza kutumia madawa hayo.

Mzee Mpobela ambaye alikuwa karibu naye akashtukia kilichokuwa kikiendelea, kila alipomwangalia David aligundua kwamba mwanaume huyo alianza kutumia madawa ya kulevya. Ilimuumiza sana, japokuwa alikuwa akiwauzia watu wengine lakini alijua madhara ya kutumia madawa hayo.

Hakupenda kumuona David akitumia, akamuita kwa lengo la kuzungumza naye, alimwambia kwamba alikuwa akitumia madawa ya kulevya kitu ambacho hakikuwa kizuri lakini David akakataa na kumwambia kwamba hakuwa akitumia madawa hayo.

Kwa kumwangalia ilikuwa vigumu kuamini kwani dalili zote alikuwa akizionyesha. Mzee Mpobela aliendelea kumsisitizia kwamba madawa ya kulevya hayakuwa mazuri, alitakiwa kuachana nayo lakini kwa Davidi ilikuwa vigumu sana kumkubalia.

Siku ziliendelea kukatika, baada ya mwaka mmoja wa kutumia kisiri hatimaye mkewe, Gloria akaanza kugundua kwamba mumewe hakuwa sawa, hakuwa imara kama kipindi cha nyuma na mbaya zaidi sauti yake ikaanza kubadilika na kusikika kama ya mtu anayetumia madawa ya kulevya.

“Mume wangu!” aliita Gloria.

“Unasemaje mke wangu!”

“Kuna nini kinaendelea?”

“Wapi?”

“Sauti yako inabadilika kila siku, kuna nini?” aliuliza Gloria huku akimwangalia mumewe huyo.

“Hakuna kitu!” alijibu David.

Alijaribu kumdanganya mke wake, hakutaka kabisa mwanamke huyo agundue kile kilichokuwa kikiendelea, kila siku alijificha, alitumia kisiri na aliporudi nyumbani alionekana kuwa sawa lakini baadaye kila kitu kikawa hadharani.

Gloria hakutaka kukubali, alijua kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea kwa mume wake, alimtilia shaka kwamba alikuwa akitumia madawa hayo na hivyo kwenda ofisini kwake.

Hakutaka kumpa taarifa, kama mumewe alikuwa akirudi nyumbani salama, hakuwa akifanya kitu sasa madawa hayo alikuwa akivutia wapi zaidi ya kazini kwake? Gloria akaenda huko, alipofika sehemu ya mapokezi, hakutaka mumewe kupigiwa simu kwani alijua kwamba endapo angejua kwamba amekuja basi angeficha kila kitu.

“Karibu!” alimkaribisha sekretari.

“Ahsante! Yupo huyu?” aliuliza Gloria.

Hata kabla msichana huyo hajajibu kitu chochote kile Gloria akaanza kupiga hatua kuelekea ofisini kwa mumewe. Akaufungua mlango na kuingia ndani. David alipomuona, akashtuka, haraka sana akainuka kwenye kiti na kumfuata kwa lengo la kumkumbatia na kumbusu kama kawaida yake, Gloria akamsukumia pembeni na kuifuata meza yake.

Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kufungua droo za meza ile, kile ambacho alikitarajia ndicho alichokutana nacho humo. Macho yake yakatua katika mfuko wa nailoni, alipouchukua na kuufungua akakutana na madawa ya kulevya pamoja na bomba la sindano.

Gloria alihisi nguvu zikimuisha, hakuamini kile alichokuwa akikiona, akakifuata kiti na kutulia, akakiinamisha kiti chake na kuanza kulia. Hakuamini kile alichokiona, mumewe, mwanaume mtaratibu, mpole leo hii alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya.

Aliumia mno, David akamsogelea mkewe kwa lengo la kuzungumza naye, Gloria akamsukumia pembeni, alivimba kwa hasira na hakutaka kusikia lolote lile kutoka kwa mumewe.

“Let me explain,” (acha nikuelezee) alisema David.

“What do want to tell me?” (unataka kuniambia nini?) aliuliza mwanamke huyo kwa hasira.

“I’m not what you think I’m,” (mimi sipo kama unavyonifikiria) alisema David.

“Who are you?” (wewe nani?) aliuliza Gloria huku akionekana kubadilika, japokuwa mara kwa mara alikuwa akikasirika lakini siku hiyo alionekana kuwa tofauti na siku nyingine kiasi kwamba David mwenyewe alianza kuogopa.

Hakuwa na cha kujitetea, alikamatwa akiwa na madawa ya kulevya, Gloria hakutaka kusikia chochote kile, akatoka na kurudi nyumbani kwake. Njiani alikuwa akilia, hakuamini kile alichokutana nacho kwa mumewe, wakati mwingine alihisi kama alikuwa ndotoni ambapo baada ya muda fulani angeamka kutoka katika usingizi mzito.

Alimfahamu mumewe, alikuwa na sifa za kuitwa mume bora kutokana na jinsi alivyokuwa. Hakujua ni nini kingetokea kama angemwambia baba yake, hakujua kama kila kitu alichokuwa nacho David kuhusu madawa yalitoka kwa mzee huyo.

Gloria akabadilisha mawazo, hakutaka kurudi tena nyumbani, ilikuwa ni lazima kuwasiliana na baba yake kwa lengo la kuonana na kuzungumza naye. Hilo halikuwa tatizo, Mzee Mpobela akamwambia amfuate ofisini kwake ambapo huko wakaanza kuzungumza.

Hakushangaa, aliligundua hilo tangu kitambo na alijaribu kumwambia David kuachana nayo lakini mwanaume huyo hakutaka kusikia. Walimwaga maji na ilikuwa vigumu kuyazoa.

Akampigia simu David na kuomba kuonana naye baada ya kurudi nyumbani. Hilo halikuwa tatizo, wakaonana na kuweka kikao cha watu wanne tu, wazazi wa Gloria, Gloria mwenyewe na David.

David hakukataa, alikiri kutumia madawa hayo na aliahidi kuacha lakini hakukuwa na mtu aliyedhani kama mwanaume huyo angeacha kutumia madawa hayo kwani watumiaji wengi waliokuwa wakitumia, ilihitajika nguvu nyingi sana kuacha.

Kama walivyofikiria ndivyo ilivyotokea, madawa ya kulevya yakamchukua David, akaanza kupoteza nguvu, mwili wake ukaanza kuchoka japokuwa alijitahidi sana kula. Alibwia madawa ambayo hayakuwa yakimpenda hivyo kuanza kudhoofika mwili wake.

Yalikuwa ni maumivu makali kwa Gloria, kilichokuwa kikitokea hakuwa akikiamini, kitendo cha kumuona mumewe akianza kupotea kilimtia uchungu mkubwa moyoni mwake.

Mwaka mwingine uliofuata, David akachakaa, hakuwa yule wa kipindi cha nyuma, maisha yake yaliendeshwa kwa kutumia madawa ya kulevya na kila alipokuwa akikosa kutumia kwa saa kumi na mbili mwili mzima ulikuwa ukiwasha kana kwamba alipakwa upupu.

“Baba msaidie mume wangu! Anapotea,” alisema Gloria huku akilia.

“Nimemsaidia sana lakini sidhani kama itawezekana tena,” alisema Mzee Mpobela.

Alijitahidi kumpeleka katika vituo vya watumiaji wa madawa ya kulevya (soba) lakini kila hali yake iliporudi na kuwa nzuri, aliporudi nyumbani aliendelea kubiwa madawa ya kulevya.

Yalimuumiza, yaliichafua damu yake, mishipa yake ilitobolewa sana kwani alipokuwa akiikosa mikononi alikuwa akiifuata ya shingoni mwake. Aliumia lakini hakuwa na jinsi, alikuwa akiitafuta stimu ambayo ingemfanya kujisikia furaha kila wakati.

Akawa anakutana na wenzake na kuanza kutumia huko, tena wakati mwingine akitoroka nyumbani na kwenda kuishi mbali kabisa. Gloria na baba yake walimtafuta sana, kila walipompata, alitoroka tena na alikuwa akirudi nyumbani pale alipokuwa akiishiwa tu, alipopata pesa, alitoroka tena.

“David mume wangu unanitesa,” alisema Gloria huku akimwangalia mume wake huyo.

“Mimi?”

“Ndiyo! Unanitesa sana! Kwa nini lakini?” aliuliza Gloria.

Mwenyewe alijiona kuwa sawa, hakuacha, kila siku alikuwa mtu wa kutumia madawa hayo. Watu wengi walimuonea huruma, waliona jinsi alivyokuwa akipotea, jinsi alivyokuwa akiyahatarisha maisha yake, kila mmoja alihuzunika lakini hawakujua ni kwa namna gani wangeweza kumsaidia kuepuka na madawa hayo.

Baada ya mwaka mwingine kuingia, mishipa yake ikaanza kupata matatizo, utumbo wake uliokuwa ukipeleka chakula ukaanza kuhadhiriwa, figo zikachoka na hatimaye akapata kidonda kidogo ubavuni, kidonda kilichokuwa kikitoka usaha kila siku.

Mzee Mpobela hakutaka kukubali, bado alimpenda sana David, alichokifanya ni kuanza kumsaidia, alimpeleka katika Hospitali ya Muhimbili, akatibiwa, hakikupona, akarudishwa nyumbani.

Alikuwa akitia huruma, japokuwa alikuwa mgonjwa lakini hakutaka kuacha madawa ya kulevya. Kidonda kile kiliendelea kumtesa, wakati mwingine alikuwa akilia usiku lakini asubuhi kama kawaida aliendelea kubiwa madawa hayo.

Kidonda kile kidogo kikaanza kuongezeka taratibu na baada ya miezi miwili akapelekwa tena hospitalini ambapo daktari aliamua kuwaambia ukweli kwamba kidonda kile kisingeweza kupona maisha yake yote kwani madawa ya kulevya aliyokuwa akitumia yalimsababisha kansa ya damu iliyoanza kumtafuna.

“Unasemaje?” aliuliza Gloria huku akiwa haamini.

“Mumeo ana kansa ya damu,” alisema daktari kwa huruma huku uso wake ukiwa kwenye huruma nzito. Gloria akaanza kulia kwani aliamini mwisho wa kansa ile ndiyo ungekuwa mwanzo wa kifo cha mume wake kitu ambacho hakutaka kuona kikitokea.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa mahali hapa.

Leave A Reply