The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-19

0

Yalikuwa ni majibu mabaya kwa Gloria, hakuamini kile alichokisikia kwamba mume wake mpendwa, David alikuwa na kansa ya damu iliyokuwa ikimtafuna ambayo kitaalamu ilijulikana kama Leukemia.

Alilia usiku na mchana, kila alipokuwa akimwangalia mume wake kitandani pale, moyo wake ulimuuma na kumchoma. Hakuona kama mume wake huyo angeweza kupona kwani kila siku kile kidonda kilichokuwa ubavuni mwake kilizidi kutoa usaha na mbaya zaidi kiliendelea kuchimbika kwenda ndani.

David aliumia, alilia kitandani pale, hakujua kama ugonjwa huo ulikuwa ni laana kutokana na yote aliyokuwa ameyafanya. Alitembea na wanawake wengi, aliwapa mimba na kuwalazimisha kutoa. Hakuona thamani ya wanawake wale, hakujua kama mwisho wake huo ulitengenezwa na wanawake wale ambao kila siku walilia kwa ajili yake.

Machozi ya uchungu waliyokuwa wameyatoa kwa ajili yake leo hii yalikuwa yakilipwa kwa maumivu makali mwilini mwake. Aliendelea kuteseka, kila siku Gloria alikuwa akishinda hospitalini hapo, kila alipokuwa akimwangalia mume wake, alibadilika, hakuwa kama yule aliyekuwa kipindi cha nyuma.

Mwili wake ulikongoroka, madawa yale yalimuumiza mno, wakati mwingine, alikuwa akitetemek, mwili wake ulizoea madawa hayo, alipokuwa akiyakosa, alikuwa akiteseka kupita kawaida.

Mzee Mpobela akamnunulia dawa za kuondoa usongo wa kutumia madawa ya kulevya, dawa za Methadone, David alianza kuzitumia hizo lakini hazikusaidia, bado alikuwa na usongo mkubwa wa kutumia madawa hayo.

Walitaka aachane kabisa na utumiaji wa madawa hayo, wakaamua kumsafirisha na kumpeleka nchini Malaysia, huko alitakiwa kukaa katika kituo kimoja cha watu waliokuwa wanatumia madawa ya kulevya lakini wakawa wanapatiwa tiba.

Akawekwa huko, kidogo ilimsaidia, hamu ya kutumia madawa hayo ikaanza kuondoka, mwili ukaanza kurudi katika hali yake ya kawaida ila ni kitu kimoja tu ndiyo kilichokuwa kikimtesa, nacho kilikuwa ni kidonda alichokuwa nacho ubavuni.

Hakikupata nafuu, kila siku kilitoa usaha, wakati mwingine kilikuwa kikinuka sana hali iliyomfanya kutengwa na watu mbalimbali. Kwa kuwa alikuwa kero katika kituo hicho, uongozi ukamwambia kwamba alitakiwa kurudi nchini Tanzania.

Akarudishwa, Gloria akabaki naye akiendelea kumuuguza mume wake. Hakupata nafuu, kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, aliteseka, aliumia lakini hakukuwa na nafuu yoyote ile aliyokuwa akiipata.

Kidonda kikachimba na kuchimba, mbavu zikaanza kuonekana, mbali na kuchimbika kwa kidonda hicho, kansa ikaongezeka kwani hata dawa alizokuwa akizitumia hazikumsaidia hata kidogo.

Macho yakaanza kuwa mekundu, kila alipokuwa akikaa, alihisi mwili wake kuwasha kupita kawaida. Akaanza kuviona viungo vyake kuwa vizito, akashindwa kutembea, alihisi damu zikiwa zimejaa miguuni, akahisi moyo wake kuwa mzito, aliteseka na kuteseka lakini hakupata nafuu hata mara moja.

“Sarafina ananiua…” alijikuta akisema mbele ya mkewe.

Gloria alishindwa kuelewa ni kitu gani kilitokea, alimwangalia mume wake kwa macho yaliyomtaka kurudia tena kile alichokisema. David hakunyamaza, alimwambia mke wake kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa akisababisha yeye kuwa katika hali hiyo.

Aliwachezea wanawake wengi, aliwaambia wanawake hao watoe mimba lakini wote hakuwakumbuka, mtu aliyemkumbuka zaidi alikuwa Sarafina. Picha aliyokutana naye barabarani ikamjia, hakuwa Sarafina yule wa kipindi cha nyuma, alikuwa mwingine kabisa, aliyechoka, ambaye alihitaji msaada mkubwa ila kwa kuwa alikuwa jeuri, akaondoa gari lake pasipo kumsikiliza kwa chochote kile.

Picha hiyo ilimuumiza kupita kawaida. Alibaki kitandani pale akilia kwa uchungu. Ulikuwa ni muda wa kutubu dhambi zake, alijua kwamba alikuwa katika hatua ya mwisho ya kuvuta pumzi ya dunia hii, alitubu, Mungu amsamehe kwa yote aliyokuwa ameyatenda.

“Mtafute Sarafina umuombe msamaha!” aliisikia sauti ikizungumza moyoni mwake.

Hakujua mwanamke huyo alikuwa wapi, hakujua kama bado alikuwa akiendelea kukaa mitaani au wapi. Alimshirikisha mke wake juu ya jambo hilo, hakutaka kumficha, alimwambia ukweli juu ya kila kitu.

Ilipita miaka mingi nyuma lakini Gloria alikumbuka kila kitu. Moyo wake uliumia, haukuumia kwa sababu ya mwanamke mwingine bali uliumia kwa kuwa mwanamke mwenzake alifanyiwa jambo kama hilo, hakika alijiona kama yeye ndiye aliyefanyiwa.

“Namkumbuka. Ni miaka mingi imepita,” alisema Gloria.

“Ninaamini yeye ndiye chanzo cha kila kitu kilichotokea mke wangu! Nahitaji kumtafuta mwanamke huyu nimuombe msamaha,” alisema David huku akimwangalia mke wake.

Alidhamiria kwa moyo mmoja, siku iliyofuata, hakutaka kukaa hospitalini, wakaomba ruhusa kutoka, wakapewa na kuanza kumtafuta Sarafina. Kila alipokuwa akitembea, david hakutembea vizuri, alikuwa akichechemea na muda mwingi alihitaji kupumzika.

Kidonda kilimtafuta, kilimtesa, kilitoa usaha, kilinuka lakini hakutaka kuona akibaki hospitali, alitaka kumtafuta mwanamke huyo, amuone mtoto wake na kumlea lakini si kuona akifa pasipo kumuona mwanamke huyo.

Alimtafuta Sarafina kwa siku ishirini, alitembea sehemu kubwa na mkewe, mitaani lakini kote huku hakufanikiwa kumuona mwanamke huyo. Moyo wake uliuma, ulichoma, alijutia maisha yake, ni kweli alikuwa na pesa lakini amani ya moyo ilikuwa ni zaidi ya pesa alizokuwa nazo.

Siku hizo zikakatika, hakumuona Sarafina wala mtoto wake. Akarudi hospitalini, akalia sana, akakata tamaa na kadiri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele ndivyo alivyokuwa akizidi kuumia kitandani pale.

“Daktari!” alimuita daktari aliyekuwa akiingia na kutoka ndani ya chumba alichokuwemo.

“Unasemaje?”

“Naomba kalamu na karatasi!” alisema David kwa sauti ndogo, daktari akaondoka, ba baada ya dakika chache akarudi na kalamu, karatasi mikononi mwake, David akaichukua, akainuka kitandani pale, kwa tabu sana akakaa na kuegemea mtu kwa nyuma.

Alisikia mauamivu makali, alivumilia, alitaka kuandika vitu kwa ajili ya Sarafina, aliamini kwamba kamwe asingeweza kumuona ila aliamini kwamba maandishi yalikuwa yakiishi na ingetokea siku moja yangeweza kumfikia mwanamke huyo.

Kabla ya kuandika maneno yoyote yale katika karatasi ile, akatulia, akaangalia juu, mawazo yake yakaanza kurudi nyuma kabisa, tangu siku ya kwanza kuonana na msichana huyo, alikuwa mrembo, alimpenda, lakini kwa ujinga wake, kwa tamaa zake mwisho wa siku akampa mimba na kumshinikiza kuitoa kitu ambacho msichana huyo alikataa.

Kila kitu alichokuwa akikiwaza wakati huo, kiliuchoma moyo wake. Aliendelea kukumbuka mambo mengi, kumbukumbu zilizomuumiza ambazo zilimfanya kujuta zaidi na zaidi. Baada ya kukumbuka kwa dakika chache, akaanza kuandika maneno hayo.

Mpenzi Wangu Sarafina.

Nakumbuka siku ya kwanza nilipokuona, hakika ulikuwa msichana mrembo ambaye sikuamini kama ningeweza kuwa pamoja nawe. Nilikupenda kupita kawaida na nilipokwambia, ulijitambua, uliutambua uzuri wako, ukanikatalia lakini mwisho wa siku ukanikubalia.

Mpenzi Wangu Sarafina.

Nilikupata, nikakupenda, sikuwa na akili, nilikuwa kijana mwenye mambo mengi. Mbali na wewe nilikuwa na wanawake wengine, nilikuchukulia kama nilivyowachukulia wengine, sikukujali sana, nilikuchukulia kuwa mwanamke wa kupita, sikukuthamini inavyotakiwa. Nisamehe sana Sarafina.

Mpenzi Wangu Sarafina.

Baadaye ukaniambia kwamba una mimba. Sikuwa tayari kuwa na mtoto, nilikuchukulia kama mwanamke wa starehe, niwe na mtoto ili iweje? Nikaamua kukwambia kwamba ulitakiwa kutoa, kama nilivyokwambia, ndivyo nilivyowaambia wengine. Nisamehe sana Sarafina.

Mpenzi Wangu Sarafina.

Niliendelea kutembea na wanawake wengine, kulala nao ndiyo ilikuwa sifa ya ujanani, niliwatambia wenzangu kwamba nilikuwa kiwembe, nilimchukua kila msichana niliyekuwa nikimtaka, sikujua kama muda unakwenda, sikujua kwamba kila ubaya unaoufanya una gharama zake, nisamee sana Sarafina, sikujua, wakati mwingine natamani sana kama muda ungerudi nyuma, nisafishe pale nilipokosea ila sitoweza tena.

Mpenzi Wangu Sarafina.

Najua ulijifungua, sikujua ulikuwa ukiishi vipi. Nilipokuona barabarani ukiwa na mtoto ambaye niliamini ni wangu kwa kuwa tulifanana sana, nilichukia. Niliona ukitaka kuniharibia uhusiano wangu kwa mke wangu, kwa kuwa sikukuhitaji, nikaondoka. Hicho ni kitu ambacho kinaniumiza mpaka leo hii. Kwa nini nimekufanyia yote hayo? Kwa nini sikukuonea huruma Sarafaina wangu? Hakika ninastahili kupata yote ninayopata kwani mauamivu ninayoyasikia moyoni, ni makubwa kuliko maumivu ya kidonda nilichokuwa nacho.

Mpenzi Wangu Sarafina.

Nilijiona mjanja, nilijiona mjuaji, baada ya kuhangaika sana na kuoa, hatimaye nikapata pesa, nikajiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya. Ninahisi kuna kitu hapa. Nilichukia madawa ya kulevya, ila kwa nini niliingia? Nahisi Mungu aliniingiza ili baadaye nipate kile kilichokusudiwa na kuutambua uovu wote niliokuwa nimekutendea maishani mwako. Sarafina! Mimi ni mkosaji, nimekukosea sana, nimekuumiza sana, ila pamoja na yote hayo, naomba unisamehe, nisamehe kwa yote niliyokutendea, ni ujinga, ni upumbavu, hakika ninastahili haya ninayoyapata. Hakika nimejifunza mambo mengi, na kupitia maisha yangu natumaini wanaume wengi watajifunza.

Mpenzi Wangu Sarafina.

Nina hamu ya kumuona tena mtoto wangu. Ninaumia ninapokufa nikiwa na mtoto mmoja tu. Nilijiona mjanja kumpa muda mke wangu kwamba hatutakiwi kuwa na mtoto kwa sasa mpaka baadaye. Ni upumbavu pia kwani kuwa na mtoto ni jambo jema mno. Sarafina, nina hamu ya kumuona tena mtoto wangu, sijui nitamuona vipi, ila ninamkumbuka mno.

Mpenzi Wangu Sarafina.

Ninaomba msamaha! Nisamehe kwa yo…..

Aliandika maneno mengi, kwa sana alihitaji msamaha kwa yote aliyokuwa ameyafanya. Hakumaliza kuandika tena, vidole vyake vikalegea, kalamu ikaanguka, macho yakawa mazito na hatimaye kufumba milele.

David akafariki kitandani pale kwa maumivu makali. Kansa ya damu ilimtafuta kwa kiasi kikubwa mno. Kilichokuwa kimemuuma mno si kansa bali moyo wake uliokuwa ukijuta kwa kila kitu alichokuwa amemfanyia msichana ambaye kila siku alimwambia kwamba alikuwa akimpenda kwa moyo wote.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho.

Leave A Reply