The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-22

0

Moyo wa Richard ulikuwa na presha kubwa, pale alipokaa alikuwa akitetemeka kwa furaha, aliikutanisha mikono yake huku akimuomba Mungu, wazazi wake walikuwa pembeni huku wakimtia moyo kwa kumwambia kwamba mkewe angejifungua salama.

Hakutulia kwenye benchi alilokuwa amekaa, wakati mwingine alikuwa akismama na kuzunguka huku na kule, alitaka kusikia sauti ya watoto wake mapacha ambao aliamini kwamba Mungu aliwabariki.

Wala hazikupita dakika nyingi, akasikia sauti ya mtoto ikilia ndani ya chumba kile, akaruka kwa furaha, hatimaye ndoto yake ya kuwa na mtoto akaiona ikiwa imetimia.

Akawakumbatia wazazi wake, alikuwa akilia kwa furaha, hazikupita dakika nyingi mkewe akatolewa ndani ya chumba kile, alikuwa hoi, akapelekwa katika chumba cha mapumziko na kutakiwa kutulia huko.

Richard alibaki akimwangalia mkewe aliyekuwa amelazwa katika machela iliyokuwa ikisukumwa kuelekea katika chumba cha mapumziko. Kwa mbali, japokuwa hakuonekana kuwa na nguvu sana Bianca alikuwa akitabasamu kwa furaha, hakuamini kama alikuwa amejifungua salama kabisa.

Kumuona mkewe haikutosha, akamwambia daktari kwamba alitaka kuwaona watoto wake wa kiume kwani ndicho kitu ambacho alikisubiri kwa miaka mingi sana. Hapohapo daktari akamwambia asubiri katika chumba alicholazwa mkewe huku mtoto alikiandaliwa kwa ajili ya kupelekwa katika chumba cha mama yake.

Hilo halikuwa tatizo, yeye na wazazi wake na wakwe zake wakaondoka na kuelekea katika chumba kile, kila mmoja alionekana kuwa na furaha tele, hawakuamini kama mwisho wa siku walifanikiwa kupata wajukuu.

“Hongera sana mke wangu!” alisema Richard huku akimwangalia mkewe, Bianca aliyekuwa kitandani.

“Nashukuru!” alisema Bianca kwa sauti ndogo.

Wala hazikupita dakika nyingi, mlango ukafunguliwa, nesi mmoja akaingia huku akiwa na mtoto mikononi mwake, alipofika, akamgawia Bianca ambaye akampokea huku akiwa na furaha tele, hakuamini kama mwisho wa siku angekuwa mama.

“Mwingine yupo wapi?” aliuliza Richard huku akiwa na hamu ya kubeba mtoto.

“Mwingine nani?” aliuliza nesi.

“Mtoto!”

“Mbona alijifungua mtoto mmoja,” alisema nesi huyo huku akimwangalia Richard.

“Mtoto mmoja? Kivipi na wakati alikuwa na ujauzito wa mimba ya mapacha?” aliuliza Richard, alishtuka, si yeye tu bali hata wazazi wake walishtuka baada ya kuambiwa kwamba Bianca alijifungua mtoto mmoja.

Richard akahisi kulikuwa na kitu kimetokea, hakuamini kile alichoambiwa, vipimo vyote vya ultra sound alivyokuwa amepiga mke wake vilionyesha kwamba alikuwa na watoto wawili tumboni, sasa ilikuwaje aambiwe kwamba alijifungua mtoto mmoja.

Kwa jicho alilokuwa akimwangalia nesi huyo, akaogopa, akatoka ndani ya chumba hicho kwa lengo la kwenda kumuita daktari mkuu. Richard hakubaki ndani, akatoka huku akiwa na hasira kali, alijua kulikuwa na kitu kilichokuwa kimetokea, alijua dhahiri kwamba madaktari na manesi walicheza mchezo wa kumuibia mtoto mmoja.

“Dokta…” aliita nesi huku akiingia ofisini kwa daktari.

“Kuna nini?” aliuliza daktari.

Richard akaingia ndani ya ofisi hiyo, alikuwa akitetemeka kwa hasira, alimwangalia daktari huku akitaka kujua ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea, alitaka kufahamu mahali mtoto wake mwingine alipokuwa.

Akamwambia daktari kila kitu kwamba alikuwa na uhakika kuwa mkewe alijifungua watoto mapacha kwani vipimo vyote vya ultra sound vilionyesha kwamba alikuwa na ujauzito wa watoto mapacha, sasa iweje aambiwe kwamba alikuwa amejifungua mtoto mmoja.

“Dokta! Ninamtaka mtoto wangu!” alisema Richard, alibadilika, alikuwa na muonekano uliomaanisha kwamba muda wowote ule angeweza kufanya jambo lolote.

“Hebu subiri kwanza!”
“Dokta! Unaniambia nisubiri! Nisubiri nini?” aliuliza Richard, alipoona hiyo haitoshi, akaufunga mlango kwa ufunguo na kisha kuuweka mfukoni, humo ndani walikuwa watatu tu, hapohapo akachomoa bastola yake.

“Nawapeni dakika mbili tu za kujua mahali alipo mtoto wangu mwingine! Vinginevyo nawamaliza wote humu ndani,” alisema Richard huku akiwa ameishika bastola yake.

Alidhamiria kuua, alikwishawahi kusikia namna watoto walivyokuwa wakiibwa hospitalini, hakutaka kuona hilo likimtokea na ndiyo maana alikuwa radhi kufanya jambo lolote lile.

Dokta mkuu hakuwa akijua lolote, alimwangalia Richard, aliogopa kwa kuhisi kwamba kweli mwanaume huyo angeweza kuwapiga risasi mahali hapo. Dokta akamtaka Richard atulie na amsikilize nesi kile alichotaka kukizungumza.

Nesi huyo hakutaka kuzungumza ukweli, alidanganya kwamba Bianc alijifungua mtoto mmoja na si wawili kama alivyosema Richard. Maneno hayo yakamtia hasira zaidi na ili kumuonyeshea kwamba alikasirika, akamnyooshea bastola, pasipo kuvutwa mkono na daktari risasi iliyotoka ingempiga kichwani.

“Paaa!” ulisikika mlio wa risasi ndani ya chumba cha daktari huyo.

“Nawaua wote wawili! Yaani mnanifanyia uhuni na hamjui nilisubiri kwa kipindi gani! Nawaua wote humu ndani,” alisema Richard huku akiikoki bastola yake.

Mlio ule wa risasi ukawashtua watu wengine waliokuwa nje ya chumba kile, haraka sana wanaume wawili wakavunja mlango, wakaingia ndani, wakamkuta Richard akiwa na bastola yake mkononi, alidhamiria kuua kwani kwa uhuni aliokuwa amefanyiwa asingeweza kuuvumilia hata mara moja.

Watu hao wakamuwahi na kumtuliza, kwa hasira alizokuwa nazo akabaki akilia huku akitetemeka, nesi yule akakimbia kwenda kutoa taarifa kwa wenzake kwamba picha ilikuwa imeungua kwani kabla ya kwenda hospitalini hapo tayari mwanaume alijua kwamba mkewe alikuwa na watoto mapacha tumboni.

“Una uhakika?” aliuliza Dk. Massawe ambaye naye alihusika katika wizi wa mtoto huyo kwa lengo la kupata pesa.

“Ndiyo!”

“Hebu wasiliana na Mzee Ngamanywa umwambie kuhusu mtoto,” alisema Dk. Massawe huku akionekana kuchanganyikiwa.

“Tumwambieje?”

“Amrudishe, tutamtafutia mtoto mwingine,” alisema Dk. Massawe.

Nesi yule akachukua simu yake kwa lengo la kumpigia mzee huyo, kitu cha kwanza kabisa alichokutana nacho ni missed calls zaidi ya kumi kutoka kwa huyo mzee, alichofikiri zilikuwa simu za kumtaka kumshukuru kwa kile alichokuwa amemfanyia.

Akampigia simu, kitu cha kwanza kabisa alichokutana nacho ni malalamiko kutoka kwa mzee huyo kwamba hakumpata mtoto, pale walipokubaliana kwamba mtoto angekuwepo, hakumkuta.

“Unasemaje?” aliuliza nesi huku akishtuka.

“Hakuna mtoto! Yupo wapi?”
“Si nilikwambia kwenye lile pipa nililokuonyeshea jana!”

“Sikumkuta!”
“Yo must be kidding me,” (unanitakia) alisema nesi huku akionekana kuchanganyikiwa.

Hakutaka kubaki ndani ya hospitali, akatoka huku akiwa na presha kubwa, hakutegemea kusikia kile alichokisikia kwamba mtoto hakuwepo katika pipa lile na wakati alimuweka na kurudi ndani.
Alipotoka nje, akaelekea katika pipa lile, hakumkuta mtoto kitu kilichomchanganya. Hakuridhika kuangalia juu ya pipa tu bali akaanza kuangalia kila kona, hakikubadilika kitu, kila kona hakuona mtoto kitu kilichomfanya kuwa na hofu kubwa.

“Ila alikuwa hapa,” alisema nesi.

“Yupo wapi sasa?”
“Nilimuweka hapa,” alisema nesi na kuondoka mahali hapo, akaenda kwa walinzi getini, alijua fika kwamba kama mtoto alichukuliwa mahali pale ilikuwa ni lazima mtu huyo apite pale getini, akaenda mpaka kule, alipouliza akaambiwa kwamba kulikuwa na mwanaume aliyepita dakika chache zilizopita akiwa na mtoto.

“Mbona hamkumzuia?” aliuliza nesi huku akichanganyikiwa.

“Sisi tulijua ndiyo mtu wa mipango ndiyo maana tukaachana naye!” alijibu mlinzi mmoja.

“Mungu wangu! Tumekwisha!”

Nesi akarudi ndani huku akikimbia, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, hakumjua mtu aliyemuiba mtoto huyo, alitetemeka kwa hofu kubwa, akawafuata wenzake, akawaambia kila kitu kilichotokea kwamba mtoto hakuwepo.

Kila mmoja alichanganyikiwa, wengine wakahisi kwamba kama wanataniwa kwani kila wapokuwa wakifanya dili la kuiba watoto walikuwa wakipelekwa huko na hakukuwa na mtu aliyekuwa akiwachukua, sasa ilikuwaje huyo achukuliwe?

Hospitalini kulikuwa ni kizaazaa, kitendo cha kutumia bastola humo kiliwafanya polisi kumkamata na kumpeleka kituoni ambapo huko akaelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea.

Kwanza polisi hawakujua kama mtu huyo ndiye alikuwa yule Richard bilionea aliyekuwa akivuma kwa utajiri lakini baada ya kujielezea kidogo polisi wote wakaonyesha heshima kwani mtu aliyesimama mbele yao hakuwa wa mchezomchezo, mbaya zaidi mpaka namba ya rais alikuwa nayo kwenye simu yake.

Aliwaambia kila kitu kilichokuwa kimetokea kwamba mkewe alikuwa na ujauzito wa watoto mapacha na si mtoto mmoja kama ilivyojionyesha. Akatakiwa kupeleka ushahidi hilo halikuwa tatizo, kwa sababu karatasi ngumu za Ultra sound alikuwa nazo, akazipeleka na kuwaonyeshea, hakuishia hapo, mpaka madaktari ambao walimpima katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wakaripoti kituoni na kuthibitisha kwamba kweli Bianca alikuwa na mimba ya watoto mapacha.

“Kwanza manesi na madaktari wote waliokuwa ndani ya chumba kile wanatakiwa kufikishwa polisi,” alisema mkuu wa kituo.

Hilo likafanyika, haraka sana polisi wakaelekea hospitali na kuwakamata madaktari na manesi waliokuwa katika chumba cha leba na kuelekea polisi. Kila mmoja hakuona kama wangenusurika katika kesi hiyo, walikuwa wakimuomba Mungu kuwaokoa kwani Richard alikuwa tofauti na watu wengine kabisa.

“Nyie hamnijui! Mimi nawafunga jela maisha,” alisema Richard huku akiwaangalia wauguzi hao waliokuwa wakiingia ndani.

Wote wakafikishwa selo na kutakiwa kutulia huko. Kila mmoja alijuta kushiriki mchezo huo mchafu na maneno ya Richard aliyokuwa akisema kwamba angewafunga maisha yaliwatisha zaidi.

Huko wakaambiwa kwamba yule Richard bilionea waliyekuwa wakimsikia sana ndiye huyo, kila mmoja akashtuka, hofu waliyokuwa nayo ikaongezeka zaidi kitu kilichowafanya wote kuona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wao.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu hapahapa.

Leave A Reply