The House of Favourite Newspapers

MPENZI WANGU SARAFINA-24

0

Ilikuwa ni kesi kubwa, Richard hakutaka kukubali, moyo wake ulikuwa na hasira kubwa kutokana na kile kilichokuwa kimetokea. Alikuwa akilalamika na muda wote aliwaambia madaktari kwamba ilikuwa ni lazima kufanya jambo baya ambalo lingebaki na kuwa historia mahali hapo.

Kila mtu aliona jinsi mwanaume huyo alivyokuwa akimaanisha, sura yake ilionyesha msimamo mkali juu ya kile alichokuwa akikizungumza, watu wote waliokuwa wakimsikia alivyokuwa akiongea, wakahisi kwamba mwanaume huyo angekwenda kuichoma moto hospitali hiyo.

Alisimama mbele ya mke wake, wote walikuwa wakilia. Bianca hakuamini kile kilichokuwa kimetokea, kilimuumiza mno, hakutegemea kumuona mtoto mmoja, aliambiwa kwamba alikuwa na watoto wawili na hata walivyokuwa wakichezacheza tumboni alihisi kabisa kulikuwa na watoto wawili.

Kujifungua kwake kulileta maumivu makubwa, alitegemea kwamba angepata furaha baada ya kupata mtoto lakini matokeo yake moyo wake ulikuwa na majonzi tele.

Manesi na madaktari waliohusika katika mchezo huo walikamatwa na kufikishwa polisi, kila mmoja alikuwa na hofu, walitamani kumrudishia mwanaume huyo mtoto wake lakini kitu cha ajabu kabisa, mtoto hakuonekana pale alipokuwa ameweka, kulikuwa na mtu aliyemfuata na kuondoka naye.

Hospitali hiyo ikaingia kwenye kashfa kubwa, watu wakazungumza mambo mengi kuhusu tukio lile lililokuwa limetokea. Tabia hiyo ya kuiba watoto ikawafanya watu wote kuikacha hospitali hiyo kwa kuona kwamba hata kama wao wangekwenda kujifungua hapo kulikuwa na uwezekano wa watoto wao kuibwa.

“Tena hii tabia imekuwa kubwa sana. Juzikati kuna mwanamke aliibiwa mtoto hivyohivyo katika hospitali hiyohiyo. Kumbe ndiyo mchezo wao,” alisema mwanamke mmoja, alikuwa akimwambia mwandishi wa habari.

“Tena ndugu mwandishi! Kuna dokta Zabroni, huyo ndiyo noma kwa kucheza michezo hiyo, anajenga majumba ya kifahari kwa kuwauza watoto wa wenzake,” alisema mwanamke mwingine, dokta Zabroni ndiye aliyesuka mipango yote.

Zilipita siku mbili wauguzi hao wakafikishwa mahakamani, wakakiri kuhusika kwa tukio hilo na hivyo kuhukumiwa kifungo cha miaka kumi na tano gerezani. Hilo halikumpa furaha Richard, alicheza mchezo mzima wa watu hao kufungwa gerezani kama kisasi kwa kile walichokuwa wamemfanyia.

Pamoja na hayo yaliyotokea, kuwafunga wauguzi hao, bado kulikuwa na swali moja tu kichwani mwake; mtoto wake alikuwa wapi?

****

Juma alibaki na mtoto chumbani kwake, kichwa chake hakikuwa sawa, alichanganyikiwa kwani kila alipomwangalia mtoto yule hakujua ni kitu gani alitakiwa kumfanyia.

Hakuwa na uji ndani ya chumban chake, hakuwa na kitu chochote kile zaidi ya maji na wali wa jana uliokuwa umebaki. Moyo wake ulikuwa na hofu, mtoto alikuwa akilia sana ishara iliyoonyesha kwamba alikuwa akisikia njaa kali.

Hakutaka kubaki ndani ya chumba hicho, alichokifanya ni kutoka na kwenda dukani ambapo akanunua maziwa na kurudi chumbani pale na kuanza kumnywesha mtoto yule ambaye akawa anakunywa huku akiachia tabasamu pana.

Moyo wake ukaridhika, akachukua simu yake na kumpigia Ibrahim kwa lengo la kwenda nyumbani na kumchukua mtoto huyo lakini hakuwa akipatikana.

Akawa na wasiwasi kwamba inawezekana Ibrahim alikwenda pale kumtelekeza mtoto yule na  kuondoka zake. Akaanza kumsubiri huku muda wote macho yakiwa kwa mtoto yule.

Maneno aliyoambiwa kwamba mtoto yule alikuwa ameibwa hayakuingia akilini mwake, hakuamini kama kungekuwa na hospitali ambayo ingethubutu kufanya kitu cha kijinga kama hicho, alichohisi ni kwamba Ibrahim aliamua kutumia uongo huo ili akubaliane naye na kukaa na mtoto huyo.

Alikaa mpaka baada ya saa kadhaa ndipo Ibrahim akarudi chumbani hapo na kuanza kuzungumza naye. Hakuonekana kuwa sawa, alikuwa amechanganyikiwa, hali aliyokuwa nayo mpenzi wake hospitalini ilimchanganya kupita kawaida.

Picha ya mpenzi wake alipokuwa kitandani ilipomjia kichwani mwake moyo wake ulimuuma kupita kawaida. Hakuamini kama kitendo cha kuwa na Malaika kingemfanya kuishi maisha ya machungu, yenye maumivu makali kama aliyokuwa akiishi.

Alimwambia Juma kilichokuwa kikiendelea hospitalini, Malaika hakuonyesha dalili zozote za kupona, kila alipokuwa akizungumza, ilionekana kabisa alikuwa akienda kufa japokuwa yeye mwenyewe alisema kwamba Mungu angemponya ugonjwa ule, kuumwa kwake kusingekuwa mwisho wa maisha yake.

“Kwa hiyo vipi kuhusu huyu mtoto?” aliuliza Juma.

“Sijajua! Ninataka akae hapa kidogo kabla ya kwenda kumwambia baba yake,” alisema Ibrahim huku akimchukua mtoto yule.

“Akae hapa?”

“Ndiyo! Kwa siku kama mbili hivi!”

Juma alikataa katakata kubaki na mtoto huyo. Alikuwa msumbufu, kwa saa kadhaa alizokuwa naye tu ilikuwa balaa, alikuwa akilia muda wote kiasi kwamba mpaka mwenyewe akaona kero.

Ibrahim hakuwa na jinsi, ilipofika usiku, akamchukua mtoto huyo na kwenda naye nyumbani kwake. Huko, akamnunulia maziwa, akamnunulia pempasi na kuanza kumuhudumia kwa kila kitu.

Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama mtoto mzuri kama alivyokuwa huyo alikuwa akiuzwa kwa mtu mwingine. Hakutaka kuona hilo likitokea na ndiyo maana aliamua kumchukua na kuondoka naye.

Usiku hakulala kwa raha, muda mwingi mtoto huyo alikuwa akiamka na kuanza kulia. Alichokuwa akikifanya Ibrahim ni kumpa maziwa pasipo kujua kama alikuwa akisikia njaa au kulikuwa na kitu kingine.

Ni kama alikesha, ilipofika asubuhi, akamuita mpangaji mwenzake, mama Issa na kumwambia kuhusu suala la kumuacha mtoto huyo kwake mpaka pale atakaporudi na kumchukua tena.

“Ni mtoto wa nani?”

“We acha tu!”

“Niambie ukweli kwanza!” alisema mama Issa.

“Ukweli ni kwamba kuna msichana nilizaa naye ndiyo kaja kumtelekeza kwangu,” alisema Ibrahim, hakutaka kumwambia ukweli kwani kama angethubutu kufanya hivyo basi stori zingeenea na hatimaye kuanza kutafutwa yeye.

Mama Issa alimwangalia Ibrahim, alimshangaa, angewezaje kutembea na msichana mwingine na wakati ndani alikuwa na Malaika. Moyo wake ulimuuma mno, aliyaamini maneno yote aliyoambiwa na Ibrahim, ila hakuwa na jinsi, kishingo upande akamchukua.

“Ila Malaika akirudi siyo unihusishe katika mambo yako,” alisema mama Issa.

“Wala usijali! Sitomwambia chochote kuhusu wewe.”

Akaondoka na kwenda hospitalini. Njiani alikuwa na mawazo tele, alitaka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Hakuacha kumuomba Mungu amponye msichana wake aliyekuwa hoi hospitalini.

Hakuchukua dakika nyingi akafika hospitalini hapo na moja kwa moja kuelekea katika chumba alichokuwemo Malaika. Kama alivyokuwa jana ndivyo alivyokuwa siku hiyo, alikuwa hoi na alionekana kama mfu kitandani pale.

Dripu za damu zilikuwa zikipishana tu, ilipotoka hii, ilitundikwa hii. Madaktari walikata tamaa, walijua kabisa kwamba msichana huyo alikuwa akienda kufa ndani ya siku chache zijazo lakini hawakutaka kumwambia Ibrahim kwa kujua kwamba angeumia sana.

Siku hiyo alizungumza naye kwa shida, msichana huyo alizidi kumwambia kwamba asiwe na hofu juu ya afya yake kwani aliamini kwamba Mungu wa Mbinguni angeweza kumponya ugonjwa aliokuwa akiumwa.

“Nitapona tu! Sitokufa mpenzi! Nitapona tu,” alisema Malaika huku akimwangalia mpenzi wake.

Ibrahim akaondoka hospitalini hapo, hakutaka kumwambia kitu chochote kuhusu mtoto aliyekuwa amemuiba hospitalini hapo. Alipofika nyumbani, akamchukua mtoto yule na kukaa naye chumbani kwake. Hayo ndiyo yakawa maisha yake ya kila siku, mpaka wiki inakatika bado alikuwa na mtoto huyo kitu kilichompa wakati mgumu.

“Ni lazima niwatafute wazazi wake, siwezi kuwa na huyu mtoto kila siku,” alisema Ibrahim, watu wa kwanza kabisa kuwasiliana nao walikuwa polisi, kile kituo ambacho Richard alikwenda kwa ajili ya kutoa taarifa.

Hakutaka kuchelewa, siku hiyohiyo akaondoka mpaka katika Kituo cha Polisi cha Osterbay, alipofika, akawaambia polisi kwamba alitaka kumfahamu mwanaume yule aliyekwenda pale wiki mbili zilizopita kuhusu kuibiwa mtoto hospitalini.

“Wewe wa nini?” aliuliza polisi mmoja.

“Ninataka kuzungumza naye!”
“Unaye mtoto?”
“Hapana! Ila ninataka kumsaidia!”
“Kumsaidiaje?”
“Mimi ni mganga wa kienyeji kutoka Sumbawanga. Nilisoma kwenye gazeti kuhusu tukio hilo. Ninataka nimfanyie dawa na ndani ya wiki moja tu atafanikiwa kumpata mtoto wake,” alidanganya Ibrahim, polisi wale wakamwangalia kijana huyo, kwa jinsi alivyokuwa akionekana, hata aliposema kwamba alikuwa mganga, hakukuwa na aliyebisha kwani hakuwa msafi sana, fukara ambaye alihitaji msaada.

“Mmh!”
“Mkuu! Najua unaweza ukawa huamini kabisa kuhusu uwezo wangu, ila unaweza kuniruhusu nikakufuata usiku twende sehemu ili uniamini. Ikifika asubuhi tu utakubaliana na mimi,” alisema Ibrahim huku akimwangalia polisi huyo.

“Unichukue mimi?”
“Ndiyo! Nikupeleke baharini uone mambo yanayotokea huko usiku,” alijibu Ibrahim.

“Wewe kijana acha masihara. Hebu kaa hapo niwasiliane naye,” alisema polisi huyo, Ibrahim akakaa kwenye benchi, polisi yule akapekua faili ambapo baada ya kuona jina la Richard, akampigia simu kwa lengo la kuzungumza naye kuhusu ‘mganga’ yule aliyefika kituoni hapo.

****

Moyo wa Richard uliuma, alihuzunika usiku na mchana, japokuwa kwa kutumia pesa zake aliwafunga wauguzi wale lakini hakuridhika hata kidogo. Kuwa na mtoto mmoja haikuwa mipango ya Mungu, yeye alipanga wawe na watoto wawili lakini kutokana na ukatili wa binadamu, wakajikuta wakiwa na mtoto mmoja.

Aliogopa hata kumwangalia mkewe, muda wote Bianca alikuwa mtu wa kulia na kuhuzunika, hakuwa na furaha hata kidogo na muda mwingi alikuwa akijifungia chumbani na mtoto wake akilia.

Siku zikaendelea kukatika, moyo wake uliendelea kuumia zaidi, kila siku alikuwa mtu wa mawazo na wakati mwingine hata kwenda kazini alishindwa kabisa kwani alihitaji kubaki nyumbani na kumfariji mke wake.

“Mtoto wetu hayupo mikononi mwetu, yupo sehemu anaishi! Kwa nini Mungu ameamua kutuadhibu namna hii?” aliuliza Bianca huku akilia.

“Usilie mke wangu! Kuna siku mtoto wetu atapatikana tu!” alisema Richard huku akimwangalia mke wake aliyembeba pacha wake mmoja.

“Ni wiki sasa imepita!”

“Haijalishi mke wangu, hata ukipita mwaka mzima, jua kuna siku mtoto wetu atakuwa mikononi mwetu,” alisema Richard, japokuwa alikuwa akizungumza kwa kujiamini lakini moyo wake haukuwa na imani hata kidogo.

Wakati akizungumza hayo na mkewe mara akasikia simu yake ikianza kuita. Akaitoa mfukoni mwake na kuiangalia. Namba ilikuwa ngeni, alitamani sana kuipokea lakini kwa kipindi hicho haukuwa muda sahihi wa kuipokea simu hiyo kwani alihitaji kuzungumza na mkewe.

Mpigaji hakukata, ilipokatika, akapiga tena na tena mpaka kuwa kero na hivyo Richard kuipokea na kuipeleka sikioni. Akasikia sauti nzito kutoka upande wa pili, alikuwa mwanaume ambaye alijitambulisha kama polisi na kumpa taarifa kwamba kuna mtu alitaka kuonana naye hapo.

“Nani?” aliuliza.

“Kijana mmoja! Amejitambulisha kwamba yeye ni mganga,” alijibu polisi huyo.

“Nimsaidie nini?”

“Kwamba anataka kuonana na wewe ili uweze kumpata mtoto wako,” alisema polisi, moyo wa Richard ukapiga paa.

“Ni mganga!”
“Ndiyo!”
“Sasa mimi na waganga wapi na wapi?”
“Naomba uje kumsikiliza!”
“Sawa nakuja!”

Richard akakata simu na kumwangalia mke wake. Alikuwa na hasira kali, hakuwaamini waganga na hakuona kama kwenye tatizo kubwa kama hilo mganga angeweza kumsaidia kwa lolote lile.

Akamwambia mke wake kuhusu simu ile iliyokuwa imepigwa, mkewe akamwambia kwamba aende huko kuonana na huyo mtu kwani siku zote binadamu hakutakiwa kukataa wito.

“Ila ni mganga!”

“Najua! Haimaanishi ukienda kumsikiliza tu basi atakuwa amekufanyia dawa. Nenda tu mume wangu,” alisema Bianca kwa sauti ya upole kabisa.

Kwa kuwa alisema mke wake, akachukua ufunguo wa gari na kuelekea huko. Hakuonekana kuwa na raha hata kidogo, moyo wake haukuwahi kumwamini mganga hata kidogo, alikwenda huko kwa ajili ya kumridhisha mke wake tu.

Alipofika, akateremka na kuelekea kaunta ambapo akamkuta Ibrahim ambapo baada ya kumuona Richard tu, akasimama kwa lengo la kuongea naye.

“Twende sehemu tukaongee!”

“Kwani hapa haiwezekani?”
“Ni muhimu sana! Twende tukaongee kaka,” alisema Ibrahim huku akimwangalia Richard.

Kwa jinsi alivyoonekana, Richard hakumwamini Ibrahim, alionekana kama mwizi, alimuogopa na kuona kwamba kama angeingia naye ndani ya gari angeweza kufanya tukio lolote baya.

Kila alipomwambia kijana huyo kwamba wazungumze sehemu yeye alitaka ndani ya gari tu. Polisi aliyekuwa akiwasikiliza yeye mwenyewe alishangaa, hakujua sababu ya kijana huyo kutaka sana kuzungumza na Richard ndani ya gari.

“Kwa nini ndani ya gari?” aliuliza Richard.

“Wewe twende! Nitakwambia kwa nini!”

Hakuwa na jinsi, akamchukua Ibrahim na kuelekea naye ndani ya gari. Walipofika, wakaanza kuangalia kana kwamba kila mtu alikuwa akimsikiliza mwenzake azungumze kitu chochote kile.

“Kuna nini?”
“Nina mtoto wako,” alisema Ibrahim huku akimwangalia Richard ambaye moyo wake ukapiga paaa.

“Unasemaje?”
“Ninahitaji kuzungumza zaidi na wewe juu ya jambo hili. Kuna mengi ya kukwambia ila kwa kifupi ni kwamba ninaye mtoto wako,” alisema Ibrahim na kumfanya Richard kuanza kutokwa na kijasho chembamba, hakuamini kile alichokuwa akiambiwa, alihisi kama alikuwa akidanganywa ila kila alipomwangalia Ibrahim, aliendelea kumwambia kwamba alikuwa na mtoto wake.

****

Richard alihisi mwili wake ukitetemeka, alihisi kabisa kijasho chembamba kikimtoka. Hakuamini kile alichoambiwa na Ibrahim, alimwangalia kijana huyo, alimwambia kweli kwamba alikuwa na mtoto wake na alitakiwa kuondoka naye na kwenda kumuona.

Richard hakutaka kupoteza muda, hapohapo akawasha gari na kuondoka mahali hapo, ilikuwa ghafla sana kiasi kwamba mpaka polisi wenyewe walishangaa. Alitamani kumpigia simu mke wake na kumwambia kilichokuwa kimetokea lakini wakati mwingine alisita kwa kuona kwamba inawezekana kijana huyo alikuwa akimdanganya.

Hakukuwa na siku ambayo aliendesha gari kwa tahadhali kama siku hiyo, hakutaka kupata tatizo lolote, hiyo ilikuwa nafasi yake ya kumuona mtoto wake, pacha ambaye kila siku alimnyima furaha, pacha ambaye kila siku alimfanya kulia kwa maumivu makali.

Safari ikaishia Magomeni nje ya nyumba moja ya kawaida ambayo kwa kuonekana ilikuwa imejengwa kwa ajili ya kupangishwa tu. Haraka sana akazima gari na kuteremka, alionekana kuwa na haraka hata zaidi ya Ibrahim aliyekuwa amemuita.

Akatangulia ndani, hakujua aingie chumba gani, alijifanya kuwa na haraka kupita kawaida, mwenyeji alikuwa nje, tayari yeye alikuwa ndani, akajikuta amesimama tu ukumbini.

“Yupo wapi?” alimuuliza Ibrahim.

“Subiri kwanza! Hebu njoo ndani,” alisema Ibrahim na kumchukua mwanaume huyo kumpeleka chumbani kwake.

Richard alipoingia tu, akahisi hali ya tofauti, chumba kilikuwa na harufu nzito, kilikuwa shaghalabaghala, kwa jinsi kilivyoonekana ilikuwa ni rahisi kusema kwamba mtu aliyekuwa akiishi humo alikuwa masikini ambaye aliishi chini ya dola moja kwa siku.

Richard akahisi machozi yakianza kujaa machoni mwake na ndani ya sekunde chache yakaanza kutiririka. Moyo wake uliumia, hakuamini kama mtoto wake alikuwa akiishi ndani ya chumba hicho kilichoonekana kutokuwa na hadhi ya kukaliwa na mtu yeyote yule.

“Mtoto wangu yupo wapi?’ aliuliza Richard, mwanaume alikuwa akitiririkwa machozi tu.

Kwanza kabla ya kumwambia mahali alipokuwa mtoto wake, akaanza kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea siku hiyo, tangu nesi mmoja alipompeleka mtoto wake nyuma ya ofisi ile kulipokuwa na pipa, alipomuona mwanaume akija kwa ajili ya kumchukua na yeye kumuwahi.

“Nashukuru sana! Mtoto wangu yupo wapi?” aliuliza Richard, hakutaka kusikia ilikuwaje mpaka mtoto wake alichukuliwa, alichokihitaji ni kujua mahali alipokuwa.

Ibrahim akatoka ndani ya chumba kile, akamfuata mama Issa ambaye akampa mtoto na kurudi naye chumbani. Richard alikuwa kwenye presha kubwa, mlango ulipofunguliwa, haraka sana akasimama na kuanza kumsogelea Ibrahim.

Alipomfikia, macho yake yakatua kwa mtoto wake, alikuwa amefanana na mtoto aliyekuwa nyumbani kwake, ilikuwa kazi nyepesi kugundua kwamba watoto hao walikuwa mapacha.

Machozi yake yakaongezeka, akamchukua mtoto huyo na kumkumbatia, moyo wake ukawa na furaha, furaha ambayo hakuwahi kuipata tangu siku alipozaliwa ndani ya dunia hii.

Alishindwa kuongea kitu chochote kile, kila alipotaka kuongea, alilia kwa kilio cha kwikwi, ilikuwa ni zaidi ya furaha, wakati mwingine kile kilichokuwa kikiendelea alihisi kwamba alikuwa katika njozi moja ya kusisimua ambapo baada ya dakika kadhaa angeamka na kujikuta akiwa kitandani.

Hakubaki ndani ya chumba hicho, akajikuta akitoka na kuanza kuondoka chumbani humo, alipofika nje, akaingia ndani ya gari lake na kuondoka pasipo kuzungumza lolote na Ibrahim ambaye alibaki akishangaa, ilikuwaje mtu amsaidie kwa kiasi hicho halafu aondoke pasipo hata kumshukuru.

“Tenda wema nenda zako,” alisema Richard, akakaa kitandani, kitu alichokikumbuka kichwani mwake ni msichana Malaika tu.

Hakutaka kuendelea kubaki chumbani humo, haraka sana akasimama na kuondoka, alikuwa na haraka, mpenzi wake ndiye alikuwa kila kitu maishani mwake. Hakuchukua muda mrefu akafika katika hospitali hiyo ambapo akaelekea katika wodi aliyolazwa mpenzi wake.

Hali haikubadilika, madaktari walikata tamaa, kila siku walipokuwa wakimwangalia msichana huyo walijua kabisa kwamba alikuwa akienda kufariki dunia kitandani hapo.

“Dokta! Nini kinaendelea?” aliuliza Ibrahim.

Siku hiyo daktari alibadilika, alionekana kuwa tofauti kabisa na kila alipomwangalia Malaika aliona kifo kikiwa mbele yake. Yeye na madaktari wengine walifanya kazi yao, walimpima Malaika na kugundua kwamba ule ugonjwa wa sickle cell aliokuwa akiumwa, ghafla ulibadilika na kuwa ‘terminal cancer’ ikiwa na maana kwamba ilikuwa ni kansa ambayo ni lazima imuue kitandani.

“Naomba nikwambie kitu kimoja,” alisema daktari huku akimwangalia Ibrahim.

“Kitu gani?” aliuliza Ibrahim.

Daktari huyo alimwambia kwamba mbali na ugonjwa wa sickle cell aliokuwa akiumwa mpenzi wake pia waligundua kwamba damu yake ilianza kushambuliwa na kansa na ndiyo sababu iliyomfanya kuteseka zaidi kitandani.

Hawakujua kansa hiyo ilianzaje, ilikuwa ghafla sana na mbaya zaidi ilivyokuwa imeanza kukomaa, haikuanza kikawaida, ilianza huku ikiwa na nguvu kubwa ya kuyapoteza maisha yake.

“Ni habari mbaya. Mwenzio amepata ugonjwa wa kansa ya damu, mbaya zaidi imekuwa terminal cancer,” alisema daktari huyo.

“Hiyo terminal ndiyo kitu gani hicho?”
“Ni kansa ambayo ni lazima afe, hawezi kupona kamwe. Mpenzi wako amebakiza miezi mitatu tu ya kuishi, baada ya hapo, atakufa, hatoweza kuishi tena,” alisema daktari huku akimwangalia Ibrahim.

“Unasemaje?”
“Mwenzio atakufa ndani ya miezi mitatu tu. Kansa hii imeharibu mfumo mzima wa damu mwilini mwake,” alisema daktari huyo.

“Yaani unamaanisha kwamba mbali na sickle cell pia ameanza kuumwa kansa?” aliuliza Ibrahim.

“Ndiyo! Tulishindwa kufahamu kabla juu ya kansa hiyo, ilijificha na ninahisi ni tatizo ambalo linawatokea watu wengi tu. Ila ukweli ni kwamba mwenzio ana terminal cancer, ni mbaya sana, huwa ikija inakuja na muda wa kuishi, wengine hupewa miaka miwili, wengine mitatu, wengine mwaka na wengine hata mwezi. Kwa hii aliyokuwa nayo mwenzio imebakiza miezi mitatu tu ya kuishi,” alisema daktari huyo.

“Miezi mitatu?”
“Ndiyo!”
“Dokta! Hebu niambie ukweli kwanza, sijasikia! Umesema Malaika amebakiza miezi mitatu?” aliuliza Ibrahim.

“Ndiyo!”
“Ya kuishi?”
“Ndiyo!”

Akasikia kitu kikali kikiuchoma moyo wake, hakuamini kile alichokisikia, akajikuta akisimama na kuanza kuelekea kule alipokuwa Malaika, alikuwa akitembea huku akipepesuka, alihisi kabisa mwili wake ukianza kuishiwa nguvu, alipofika huko, akasimama pembeni ya kitanda chake, moyo wake ulikuwa na maumivu makali, alimwangalia mpenzi wake pale kitandani alipokuwa, hakuamini kama alikuwa njiani kumpoteza mpenzi wake huyo ambaye kwake alikuwa kila kitu.

“Terminal cancer…hawezi kuishi zaidi ya miezi mitatu lazima atakufa,” aliisikia sauti ya daktari moyoni mwake.

Malaika alikuwa kimya, aliyafumba macho yake lakini baada ya kuhisi kwamba kulikuwa na mtu amesimama mbele yake, akayafumbua macho na kumwangalia mtu huyo, akatoa tabasamu pana kwani mtu aliyekuwa amesimama alikuwa Ibrahim, mwanaume aliyekuwa muhimu sana katika maisha yake.

“Ibrahim! Mungu atatenda maajabu!” alisema Malaika huku akimwangalia Ibrahim ambaye alikuwa kimya tu.

“Najua unahuzunika! Nimeambiwa kwamba nimepatwa na kansa na nitakufa ndani ya miezi mitatu. Ibrahim, huu ndiyo muujiza ambao nimekuwa nikikwambia, hii kansa ndiyo muujiza ambao Mungu aliniotesha kwamba nitakutana nao,” alisema malaika huku akimwangalia Ibrahim.

“Unaumwa kansa Malaika! Si sickle cell tena! Kwa nini Mungu anafanya yote haya?” aliuliza Ibrahim.

“Kwa sababu anataka kuniponya!”
“Kukuponya! Kukuponyaje?” aliuliza Ibrahim.

“Sijajua lakini nahisi hii ndiyo nafasi ya Mungu kujionyesha kwamba Yeye ni Mungu asiyeshindwa,” alisema Malaika kitandani pale ambapo alikuwa amekonda kupita kawaida.

Maneno yake yalikuwa hayohayo, alikuwa akijitia imani kila siku kwamba Mungu angekwenda kumponya. Aliendelea kubaki hospitalini hapo na baada ya wiki moja madaktari wakamwambia Ibrahim kwamba kiasi cha fedha alichokuwa akidaiwa kilikuwa kikubwa, asingeweza kulipia lakini wakamtaka kumchukua Malaika na kurudi naye nyumbani ili akamtibu hukohuko nyumbani.

Hakuwa na jinsi, akamchukua Malaika wake na kurudi naye nyumbani kwake ambapo akaanza kumpa matibabu hukohuko, akaanza kumnunulia dawa na kumuhudumia kwa kila kitu kama alivyokuwa akiambiwa.

Mwili wa Malaika ukazidi kukongoroka, akabaki mifupa mitupu, kansa ya damu ikaanza kumtesa, mwili ukapauka na wakati mwingine akaanza kutoka damu puani na masikioni, ngozi yake ikashindwa kupambana na ugonjwa huo, ikaanza kusinyaa, ikaanza kutoa vipele vilivyokuwa vikimuwasha usiku na mchana, alipoanza kuvikuna, vikatumbuka na kuanza kutengeneza vidonda mwilini mwake, vidonda vilivyokuwa vikimuuma na kumfanya kupiga kelele usiku.

“Ibrahim mpenzi! Ninakufa…” alisema Malaika huku akilia kitandani pale.

“Malaika! Kumbuka uliniambiaje! Kumbuka maneno uliyosema kwamba Mungu atakuponya. Mpenzi utapona, utapona, hautokufa! Nakwambia hautokufa,” alisema Ibrahim huku akimwangalia mpenzi wake huyo pale kitandani.

Kila siku ikawa mateso juu ya mateso, vidonda vile vilivyosababishwa na vipele viliendelea kumuuma zaidi, akawa mtu wa kulia, vikatoa damu na mwisho wa siku hali kubadilika na kutoa usaha kitu kilichosababisha harufu kali ndani ya chumba hicho.

“Mmh! Kuna panya ameoza au kuna maiti humu ndani?’ alisikika akiuliza mwanamke mmoja ndani ya nyumba hiyo.

Mwili wa Malaika ukazidi kutoa harufu kali ambayo iliwafanya wapangaji wengi kuanza kulalamika ndani ya nyumba hiyo kwamba iweje wakae na maiti ndani iliyokuwa imeoza na kunuka, wengi wakamtaka Ibrahim kwenda kumzika Malaika kwani tayari alikuwa amekufa na ndiyo maana mwili wake ulikuwa ukitoa harufu mbaya kama kitu kilichooza.

 

JE, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu hapahapa.

Leave A Reply