The House of Favourite Newspapers

MREMBO AFUNGA MTAA AKITAKA KUJIUA

NI timbwili! Mrembo aliyefahamika kwa jina moja la Shelua amefunga mtaa akitaka kujiua kwa kuparamia magari yaliyokuwa kwenye mwendokasi barabarani, Ijumaa Wikienda lilishuhudia. Tukio hilo lililojaza umati mkubwa na kusababisha foleni ndefu ya magari lilijiri wikiendi iliyopita, nje ya Ofisi za Manispaa ya Morogoro Mjini.

Chanzo cha balaa hilo ilielezwa kwamba Shelua aliyejaliwa shepu matata ambaye ni mkazi wa Chamwino mjini hapa ilisemekana anasumbuliwa na ugonjwa wa kuanguka (kifafa) baada ya kutumia pesa nyingi kwa matibabu bila mafanikio.

Ilisemekana kuwa, Shelua, akiwa kwenye hali kama hiyo aliamua kujiongeza na kwenda kuomba msaada kwa mkuu wa wilaya ambaye alimpatia kibali cha kuingia kwenye taasisi na watu binafsi kuomba msaada wa matibabu.Hivyo kwa muda mrefu Shelua alikuwa akitafuta kumuona mkurugenzi wa manispaa ili ampe msaada, lakini alikuwa akizuiwa na walinzi wa getini.

“Huyu dada, awali alifika ofisini kwetu hapa Star TV, akaomba msaada akidai ana kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya. “Kweli nilipokikagua kibali chake nilikuta kina saini ya mkuu wa wilaya huku kikionesha kwamba Shelua anasumbuliwa na ugonjwa wa kuanguka.

“Sisi tulimchangia tulichojaliwa na alipotoka hapa kwetu akaelekea manispaa. Nasikia alipofika getini, mmoja wa walinzi alionesha kumtaka kimapenzi. “Baada ya kukataa ombi, mlinzi alimzuia kuingia ndani ndipo mrembo huyo kwa hasira akaamua kufunga mtaa na kuparamia magari kwa mbele akitaka kujiua,” alisema Peter Laurence.

Akizungumza na Ijumaa Wikienda huku akiangua kilio, Shelua alisema: “Mimi siyo chizi kama watu wanavyodhani, nimefanya hivi kwa hasira, mimi ninaumwa, mkuu wa wilaya amenipa kibali cha kuomba msaada.

“Wiki iliyopita nilikuja hapa manispaa, mkurugenzi akaniambia nije Alhamisi au ljumaa. Nimekuja mlinzi ananitaka, eti nikampe penzi anipe elfu 20. “Baada ya kumkatalia ndipo akanizuia kuingia ndani. Kwa hasira nikaona bora nigongwe na magari ili nife kuliko kunyanyasika.

Wakati Shelua akijirusha barabarani ili agongwe, baadhi ya madereva wastaarabu walisimamisha magari na kumkwepa, lakini kuna dereva mmoja alimburuza umbali wa mita kadhaa kisha akambwaga na kutimka zake. Mwandishi wetu alitinga kwenye geti hilo la manispaa na kuwakuta walinzi wawili ambapo walipoulizwa kuhusiana na madai ya kumtongoza Shelua walisema:

“Kweli huyo binti alikuja na kibali chake kutoka kwa mkuu wa wilaya na hii si mara ya kwanza kuja. “Wiki iliyopita alikuja, tukamruhusu, kumbe huko ndani alikwenda kufanya fujo. Sisi kama walinzi tulisemwa sana na mabosi zetu kuwa kwa nini tulimruhusu huyo dada.

“Kuhusu kutongozwa, hakuna aliyemtongoza.”Hata hivyo, baadaye difenda la Polisi lilitinga ambapo askari walifanya kazi ya ziada kumkamata na kuondoka naye kumpeleka kituoni. Polisi walipoulizwa kosa lake walisema kuwa alichokuwa akikifanya ni kutaka kujiua, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Ijumaa Wikienda lilizungumza na Afisa Habari wa Manispaa ya Morogoro, Lilian Heneriko juu ya timbwili hilo ambapo alisema: “Siko ofisini kwa sasa na siwezi kuzungumzia kitu ambacho sikifahamu, nipe muda nifuatilie madai hayo, huenda ni kweli au siyo kweli, njoo ofisini Jumatatu (leo).”

STORI: Dunstan Shekidele, MOROGORO

Comments are closed.