The House of Favourite Newspapers

Msanii Bongo afia kwenye treni

KIFO hakina siku wala saa, popote kinaweza kukutokea! Hii imejidhihirisha kwa msanii maarufu wa vichekesho Bongo, Iddi Lusaka ‘Katuni’ ambaye amefikwa na umauti akiwa ndani ya treni akisafiri.

 

Akizungumza na Risasi Jumamosi, msanii mwenzake ambaye walikuwa wakiigiza michezo ya vichekesho hasa mikoani, Walii alisema kifo cha rafiki yake huyo kilitokea Jumanne iliyopita ambapo alizidiwa ghafla akiwa ndani ya treni na kufariki dunia.

 

Aliendelea kusema kuwa, Katuni alipata homa ya ghafla na kichwa kumuuma sana akiwa safarini kuelekea Kigoma kumsalimia mama yake, lakini walipofika mkoani Dodoma ndipo akafikwa na umauti.

 

“Wiki moja iliyopita Katuni ambaye ni msanii mwenzangu alikuwa anaumwa lakini akapata nafuu na kuwa sawa, ambapo alisema anaenda kumsalimia mama yake ambaye yuko nyumbani kwao Kigoma. Akapanda treni akiwa mzima lakini akazidiwa ghafla na kuaga dunia hukohuko ndani ya treni.

 

“Kifo cha Katuni kimenisikitisha sana kwani ameondoka bado hajatimiza ndoto zake kwa sababu alikuwa na ndoto nyingi za kufika mbali kwenye uigizaji, naumia maana alikuwa mtu wa karibu yaani kama ndugu ambaye tumefahamiana siku nyingi sana, sasa yeye kuondoka ghafla imenishtua sana, lakini ndiyo kazi ya Mungu, namuombea alale mahali pema peponi,” alisema Walii.

 

Walii alisema kuwa Katuni alizikwa Jumatano iliyopita mkoani Dodoma ambako ndugu zake baadhi waliamua hivyo kutokana na bajeti ya kuusafirisha mwili kwenda Kigoma kuwa ndogo kisha baadaye kuupeleka msiba Kigoma kwa ajili ya matanga.

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi Jumamosi

Comments are closed.