The House of Favourite Newspapers

Msanii Mkongwe wa Filamu Bi Hindu Afariki Dunia Baada ya Kuugua kwa Muda Mrefu

0
 Chuma Suleiman almaarufu Bi Hindu

MSANII wa filamu mkongwe na mtangazaji, Chuma Suleiman almaarufu Bi Hindu, amefariki dunia asubuhi hii, nyumbani kwake, Magomeni jijini Dar es Salaam.

 

Taarifa za kifo chake, zimetolewa asubuhi ya Julai 9, 2022 ambapo mjukuu wake, Badra Hanya amethibitisha taarifa za kifo cha bibi yake, ambaye ameaga dunia akiwa nyumbani kwake, Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.

 

Bi Hindu alianza kusumbuliwa na maradhi mwishoni mwa mwaka 2019 ambapo ilipofika Machi, 2022, Gazeti la Ijumaa Wikienda linalochapishwa na Kampuni ya Global Publishers, lilifanya mahojiano naye ambapo alinukuliwa akisema:

 

“Nilianza kuumwa muda kidogo. Kabla ya hali yangu kuwa mbaya, huko nyuma nilichukulia kawaida kwa sababu nilikuwa na goita shingoni. Ndugu zangu wakasema inaweza ikawa ndiyo inasababisha maumivu mwilini.

 

“Nilikwenda hospitalini, madaktari wakanipima na kuniambia mifupa yangu imesagika. Sehemu ya bega la mkono wangu wa kulia ndiyo inaniuma sana mpaka ninapoteza fahamu. Nimeshakwenda Muhimbili nikafanyiwa oparesheni ya kwanza, lakini haikusaidia.

 

“Ikabidi nifanyiwe oparesheni ya pili ambayo baada ya kukaa siku tatu, hali ilizidi kuwa mbaya na sasa hivi ndiyo siamki, naumwa na kupoteza fahamu kila wakati.”

 

Tangu wakati huo, Bi Hindu aliendelea kuteseka kwa maradhi kwa muda mrefu, wadau mbalimbali wakijitahidi kumsaidia kwa hali na mali mpaka hatimaye aliporejea kwa Muumba wake.

 

Enzi za uhai wake, Bi Hindu alikuwa miongoni mwa watu wachache walioanzisha kundi la sanaa la Kaole ambalo baadaye lilikuja kuwa hazina kubwa katika tasnia ya maigizo na filamu Bongo, likizalisha mastaa wengi wakiwemo Marehemu Steven Kanumba, Vincent Kigosi ‘Ray’, Blandina Chagula ‘Johari’, Elizabeth Michael ‘Lulu’ na mastaa wengine lukuki.

 

Taarifa zaidi kuhusu msiba wake zitaendelea kukujia.

 

 

Leave A Reply