The House of Favourite Newspapers

Msanii wa Bongo Afanyiwa Ukatili India, Afariki

0
Msanii wa Kibongo, Neema Joseph (kulia) akiwa na walezi wake alipokuwa Bongo enzi za uhai wake.

STORI: Imelda Mtema na Mayasa Mariwata | Risasi Jumamosi | Habari

DAR ES SALAAM: Ukatili! Msanii wa Kibongo, Neema Joseph (31), anadaiwa kufanyiwa ukatili wa kutisha hadi kufariki dunia kisha maiti yake kurejeshwa nchini ikiwa na majeraha, hali ambayo imezua utata na maswali kwa ndugu, jamaa na marafiki zake.

Habari kutoka kwenye vyanzo zilieleza kuwa, msanii huyo alikuwa akiishi katika Mji wa New Delh, India na mwili wake ulisafirishwa na ndege ya mizigo hivyo kuwafanya ndugu zake kubaki na maswali mengi kwani waliukuta ukiwa na majeraha bila kusitiriwa.

Akionyesha majeraha yake mwilini.

DADA AMUELEZEA MAREHEMU

Akizungumzia tukio hilo kwa masikitiko kwenye msiba wa Neema uliwekwa nyumbani kwake, Mwananyamala B, Kinondoni jijini Dar, dada wa marehemu, Asha Sigareti, alianza kwa kuelezea historia ya Neema hadi alipojiingiza kwenye sanaa, kuitumikia na baadaye kukutwa na umauti. Asha alisema kuwa, mdogo wake alitoroshwa na mama mmoja kutoka kijijini kwao mkoani Singida miaka kadhaa iliyopita ambapo alikuwa darasa la tano kwa ahadi ya kumpeleka Dar kumsaidia kimaisha. “Walipofika Dar, mama huyo alikuwa hampi Neema malezi mazuri, akawa kama mtoto wa mtaani tu. “Baadaye kuna rafiki yake alimchukua na kwenda kuishi naye kwao. Wazazi wa rafiki yake huyo walimpenda sana Neema na kumchukulia kama mtoto wao.

APANGA CHUMBA ILALA

“Umri wa utu uzima uliposogea, Neema alipanga chumba maeneo ya Ilala, Dar na kubahatika kupata mtoto wa kiume aliyempa jina la Joshua. Baadaye alimpeleka mtoto huyo kwa baba yake (jina la baba halikupatikana),” alisema dada huyo. Akiendelea kuzungumza kwa uchungu, dada huyo wa marehemu alisema kuwa, kwa kuwa Neema alipenda kujishughulisha na sanaa, baadaye alijiunga na Kundi la Kanga Moko ‘Laki si Pesa’ ambalo lilikuwa likitoa burudani ya kunengua katika kumbi za starehe jijini Dar. “Walifanya shughuli mbalimbali za sanaa jijini Dar na hakika kwa watu wa kipindi kile, wanajua mambo waliyokuwa wanayafanya walipokuwa jukwaani,” alisema dada huyo na kuongeza kuwa Neema pia alikuwa mwimbaji wa Taarab anayeibukia.

AENDA INDIA

Dada huyo wa marehemu alisema kuwa, ilipofika mwaka 2014, Neema alipewa dili na rafiki zake la kwenda India kwa ajili ya kunengua na ndiyo ndugu hawakumuona tena hadi aliporejeshwa akiwa maiti. “Mwaka 2014 kuna rafiki zake walikuwa wanaenda India kufanya shughuli za sanaa (kunengua) kwani zinalipa, Neema naye alikuwa na tamaa ya maisha, akaenda na sisi akawa anatupigia simu kutujulisha maendeleo yake. “Maisha yaliendelea hivyo lakini baadaye akawa anatueleza kwamba yeye na baadhi ya wenzake kule wanakosana wenyewe kwa wenyewe na kujikuta akifanyiwa ukatili wa kupigwa na kumsababishia majeraha makubwa.

AWAPA TAARIFA HALI MBAYA

“Dakika ya mwisho tuliwasiliana na mwenzake mmoja, akatuambia kuwa Neema yu mahututi. Hatukuelewa nini kimemsibu hadi sasa, japo pia tumepewa taarifa nyingine, tunasikia baada ya kupigwa na wenzake aliumwa figo na alikuwa anakunywa dawa kisha anatumia pombe kali. “Mwili wake umeletwa nchini ukiwa na majeraha, sehemu ya kichwa imebonyea na cha kustaajabisha ameletwa na ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege la Ethiopia, tena tumepewa mwili ukiwa mtupu kama alivyozaliwa inauma sana mdogo wangu amekufa kikatili sana,” alisema Asha akilengwalengwa na machozi.

MAWASILIANO YA MWISHO

Alisema kuwa, mara ya mwisho kuwasiliana na mdogo wake ilikuwa Januari, mwaka huu ambapo alimwambia amwambie mama yao atarudi Mei (mwezi ujao), mwaka huu, jambo lililomuumiza zaidi kuona mwezi huo umekaribia lakini mdogo wake anarejeshwa akiwa maiti.

Alipotoka hospitali kwa matibabu akilewa.

NEEMA AZIKWA M’NYAMALA

Mrembo huyo ambaye ameacha mtoto mmoja alizikwa Aprili 22, mwaka huu katika Makaburi ya Mwananyamala, Dar huku familia yake ikiiomba serikali kufuatilia kwa kina kifo cha binti yao na kuwaelimisha mabinti wa Kitanzania wanaokwenda kutafuta maisha ughaibuni. Mmoja wa wanenguaji wa Kanga Moko aliyekuwa msibani hapo alithibitisha kufanya kazi ya unenguaji na uimbaji na Neema kwenye kundi hilo ambalo inasemekana kwa sasa limesambaratika. Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Nje Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk Augustine Mahiga ili kujua kama ana taarifa ya kifo cha Neema, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.

Leave A Reply