The House of Favourite Newspapers

Mshangao! Ni Mshangao!

0

Majaliwa kassim (2)Waziri Mkuu Mteule wa Tanzania, Kassim Majaliwa

Hilo ndiyo neno pekee unaloweza kulitumia kueleza uteuzi wa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, uliofanywa na Rais wa Awamu ya Tano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, jana, Novemba 19, 2015 kisha kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majaliwa alipitishwa kwa kura 258 kati ya 349 zilizopigwa ukiwa ni ushindi wa asilimia 73.5 ambapo waandishi wetu waliokuwa bungeni mjini Dodoma na Dar es Salaam, walikuwa makini kufuatilia kila kilichokuwa kinaendelea na hapa wanakuletea ripoti kamili:

Majaliwa kassim (1)Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai akiwaonesha wabunge bahasha yenye jina la Waziri Mkuu aliyeteuliwa na Rais Magufuli.

HAKUTARAJIWA NA WENGI

Jina la Majaliwa, halikuwa miongoni mwa majina ya wanasiasa kadhaa waliokuwa wakitajwa mara kwa mara, hasa kwenye vyombo vya habari kwamba wanaweza kutwaa nafasi hiyo.

Miongoni mwa wanasiasawaliokuwa wakipigiwa sana chapuo kwamba wanaweza kuvaa viatu vya uwaziri mkuu kutokana na utendaji wao wa kazi na majina ya majimbo wanayoyaongoza kwenye mabano, ni pamoja na Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), William Lukuvi (Ismani), January Makamba (Bumbuli), Prof. Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini), Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi) na wengine wengi.

Majaliwa kassim (5)Waziri Mkuu Mteule wa Tanzania, Kassim Majaliwa akipongezwa na wabunge baada kuteuliwa.

UPEPO WABADILIKA GHAFLA

Hata hivyo, siku moja kabla ya mchakato wa uteuzi wa waziri mkuu, upepo wa kisiasa ulibadilika baada ya majina mawili kuvuja kutoka vyanzo vya ndani vya serikali; Ramo Makani, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, alikuwa akipewa nafasi kubwa huku Majaliwa, akimfuatia kwa sifa za kuukwaa wadhifa huo nyeti serikalini.

Hata hivyo, mambo yaliendelea kuwa tofauti ambapo kwa mujibu wchanzo chetu cha ndani, jina la Makani lilikatwa kwa kigezo kwamba hakuwa na uwezo wa kuongoza baraza la mawaziri kwa sababu hakuwahi kuwa waziri hivyo kukosa uzoefu.

Bahati ya mtende ikamuangukia Majaliwa ambaye kabla ya jana kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, alikuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya WaziriMkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) akishughulika na upande wa elimu, nafasi aliyoitumikia kwa muda wa miaka mitano, tangu alipoteuliwa na Rais (mstaafu), Jakaya Mrisho Kikwete, mwaka 2010.

USIRI MKUBWA WATAWALA

Usiri mkubwa ulitawala katika mchakato wa kumtangaza waziri mkuu, ambapo tofauti na miaka mingine yote ambapo spika wa bunge ndiye hulifuata jina la waziri mkuu mteule kwa mheshimiwa rais, jana alimtuma Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila kufuatilia jina hilo kwa Mhe. Magufuli lakini ikashindikana.

Badala yake, tofauti kabisa na utaratibu wa miaka yote, Rais Magufuli alimtuma mlinzi wake wa karibukulipeleka jina hilo bungeni, akaingia akiwa na bahasha huku akisindikizwa na askari wa bunge na kwenda kumkabidhi Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Kingine kilichomshangaza spika ni kukuta ndani ya bahasha hiyo kuna bahasha nyingine mbili ambazo zote zilikuwa zimefungwa kwa gundi maalum ambapo alizifungua moja baada ya nyingine na hatimaye kukutana na jina la waziri mkuu.

Ajabu nyingine ni kwamba taarifa ya rais kwenda kwa spika, kuhusu kumteua Majaliwa ilikuwa imeandikwa kwa mkono na rais mwenyewe, tofauti na miaka yote ambayo huchapwa kwa mashine.

Baada ya yote, Spika Ndugai aliusoma ujumbe huo na alipolitaja jina la mbunge huyo wa Ruangwa, mshangao na mshtuko vilionekana Dhahiri miongoni mwa wabunge kwani ni jambo ambalo halikutarajiwa na wengi.

WENGINE WAONESHA WASIWASI WAO

Baada ya jina hilo kutajwa, baadhi ya wabunge walionesha dhahiri wasiwasi wao kama Majaliwa anaweza kumudu kushika wadhifa huo mkubwa serikalini, hasa ikizingatiwa kwamba hakuwahi kufikia ngazi ya uwazirikamili zaidi ya kukomea kwenye unaibu.

“Uwaziri mkuu siyo kazi lelemama, mheshimiwa hajawahi kuwa waziri kamili, anawezaje kuongoza baraza la mawaziri?” alinukuliwa mheshimiwa mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake. Hata hivyo, wasiwasi huo ulipingwa na baadhi ya waheshimiwa wengine waliomtolea mfano Mhe. Frederick Sumaye kwamba naye wakati anateuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo lakini akavunja rekodi ya kuwa waziri mkuu pekee aliyeshika wadhifa huo kwa kipindi chote cha miaka kumi.

NI WA PILI KUTOKA TAMISEMI

Ukiachilia mbali Majaliwa aliyetokea Tamisemi, waziri mkuu aliyemaliza muda wake, Mizengo Pinda naye alitokea kwenye wizara hiyohiyo, hivyo kufanya mpaka sasa wizara hiyo kutoa mawaziri wakuu wawili mfululizo, jambo ambalo halijawahi kutokea kwenye wizara nyingine yoyote.

RUANGWA CHEREKOCHEREKO

Mwandishi wetu aliyekuwa jimboni kwa Mhe. Majaliwa wakati jina lake likitangazwa kuwa waziri mkuu, anaeleza kwamba maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na kijiji alichozaliwa cha Mnacho, yalitawaliwa na cherekochereko ambapo wananchi wengi walikuwa wakiimba nyimbo za furaha na kumpongeza mbunge wao kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo kubwa serikalini.

KUBENEA, MBATIA WAPINGA KUMPIGIA MAKOFI MAJALIWA

Wakati wa shamrashamra za kumpongeza Majaliwa bungeni baada ya jina lake kutangazwa, tafrani kidogo iliibuka baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola kuwataja Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea na Mbunge wa Vunjo, James Mbatia kwamba aliwaona wakipiga makofi wakati jina la Majaliwa likitangazwa, jambo ambalo wawili hao walilipinga vikali na kusababisha mvutano ndani ya bunge wakimtaka afute kauli yake, jambo ambalo baadaye alilifanya baada ya spika kuingilia kati.

NI MCHAPAKAZI KAMA MAGUFULI

Watu waliowahi kufanya kazi na Majaliwa, wanamueleza waziri mkuu huyo mteule kwamba anaweza kuendana na kasi ya Rais Magufuli kwa sababu naye ni mchapakazi, asiyependa kukaa ofisini na kusubiri ripoti.

“Alipokuwa Tamisemi, alitembelea karibu nchi nzima kutafuta matatizo yaliyokuwa yanaikabili wizara yake, akawa anazungumza na walimu na watumishi wengine wa serikali na kusikiliza matatizo yao jambo ambalo hata Magufuli analo,” mtumishi mmoja wa wizara hiyo, alilitonya Uwazi Mizengwe kwa masharti ya kutotajwa jina lake.

WABUNGE WANAMZUNGUMZIAJE MAJALIWA

Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamemzungumzia kwa urefu Waziri Mkuu mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa ambapo walisema:

EZEKIEL MAIGE (MSALALA)

“Kwanza ni kijana ambaye kwa hakika ataendana sawa na falsafa ya Rais Dk. Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’. Lakini pia Majaliwa ni mchapakazi tena mfuatiliaji

wa mambo kwa vitendo, kwa hiyo ni chaguo sahihi.”

IBRAHIM RAZAZ (KIEMBESAMAKI)

“Majaliwa hana makundi, si mtu wa kupokea majungu, hivyo tutarajie utendaji usiokuwa na msukumo wa nguvu ya watu wachache.”

WILLIAM LUKUVI (ISMANI)

“Ni mtu msikivu, muadilifu, hana makundi lakini pia ni mtu wa bidii, ….nimpongeze Mhe. Rais kwa kutuchagulia mtu sahihi.”

MBONI MHITA (HANDENI VIJIJINI)

“Ni mzoefu katika utendaji, mkimya lakini mfuatiliaji wa mambo kwa vitendo na si kwa maneno mengi na makelele, pia ni muadilifu.”

MAGDALENA SAKAYA (KALIUA)

“Hana kashsfa, mimi namfahamu vyema kwa sababu alikuwa mkuu wangu wa wilaya kule Urambo, hata alipoacha nafasi hiyo na kwenda kugombea ubunge huko Ruangwa, nakumbuka wananchi wa wilaya ya Urambo walisikitika sana.”

PETER MSIGWA (IRINGA MJINI)

“Binafsi sijaridhika na uteuzi huu, kwanza kwa sasa kama nchi, tunahitaji waziri mkuu mtendaji na mwenye kufanya uamuzi kwa wepesi, sasa kwa haiba ya Majaliwa, sioni hali hiyo, mimi ni jamaa yangu kabisa, lakini sidhani kama anaweza kukikalia kiti hicho.”

DAVID SILINDE (MOMBA)

“Kwanza imekuwa tofauti kabisa na matarajio ya wengi, kwamba kila mtu alikuwa na hisia ya watu wengine maarufu sana wa siasa, lakini hali imekuwa nyingine, Mjaliwa si mtu wa kujikweza hata kwake anaishi maisha ya kawaida kabisa, ni mtulivu, naamini ni chaguo sahihi.”

KHAMIS KINGWALA (NZEGA VIJIJINI)

“Kusema kweli Majaliwa ni mtu mwenye hekima na busara za hali ya juu, nimefanya naye kazi kwa maeneo mengi, hata kwenye upande wa michezo amekuwa mwalimu wetu wa timu ya Bunge Sports Club; namjua.”

KANGI LUGOLA (MWIBARA)

“Hakutarajiwa, lakini ni mtu makini sana hususan kwa viongozi wazembe, mfano mzuri ni kule jimboni kwangu kuna shule moja walimu walifanyiwa mchezo wa kishirikiana, nilipompelekea shauri hilo, ni yeye ndiye alikuwa akinipigia simu na wakati mwingine usiku wa manane, akitaka kujua maendeleo ya walimu hao, kwa hiyo ni mtu mfuatiliaji.”

Leave A Reply