The House of Favourite Newspapers

Mshindi wa Nyumba Kupokelewa Kifalme Dar

0
Mshindi wa Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, George Majaba  (kushoto).

SASA ni rasmi kwamba mshindi wa Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba Awamu ya Pili, George Majaba, atakabidhiwa mjengo wake wenye thamani ya mamilioni ya shilingi mwisho kabisa wa mwezi huu, jijini Dar es Salaam.

 

Mjengo huo uliojengwa Bunju B, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, una vyumba vitatu vya kulala, chumba cha kusomea, chumba cha chakula, sebule, jiko, choo na bafu na ambao, wakati Majaba atakapokabidhiwa, utakuwa tayari umeshaunganishwa na umeme ndani yake.

 

Lakini jambo moja la kufurahisha ni kwamba wakati George akiwasili Dar es Salaam tayari kwa shughuli hiyo, atapokewa kama mfalme, kwani maandamamo rasmi, yatakayoongozwa na pikipiki na magari, yameandaliwa.

 

“Tunataka kufanya kitu kidogo tofauti na cha kumtia faraja mshindi wetu, kwa maana hiyo tumeandaa mapokezi maalum, tumeandaa pikipiki na magari ambayo yatampokea Ubungo Terminal na kuja naye hadi ofisini kwetu (Zilizopo Sinza Mori, zamani Johannesburg Hotel).

 

“Pale kutakuwa na utambulisho rasmi wa mshindi wetu ikiwa ni pamoja na kufanya mahojiano na vyombo vya habari na kisha tutaanza safari ya kuelekea nyumbani kwake kwa ajili ya kumkabidhi nyumba yake,” alisema Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho.

 

“Tumeamua kumpa nyumba ikiwa kamili kabisa, atakachofanya yeye ni kuja na begi lake na kuanza maisha, hiyo yote ni kuonyesha jinsi gani Global Publishers imedhamiria kubadili maisha ya wasomaji wake, pamoja na thamani kubwa ya nyumba, lakini tumeona tumuongezee na nishati hii muhimu ili kumpunguzia jukumu la kuhangaika kuingiza umeme,” alisema Mrisho. Hii ni mara ya pili kwa Global Publishers, kampuni pekee ya uchapaji magazeti katika historia, kuwahi kutoa zawadi ya nyumba kwa wasomaji wake.

 

Katika Bahati Nasibu ya Kwanza ya Shinda Nyumba Awamu ya Kwanza, msomaji mkazi wa Iringa, Nelly Mwangosi aliibuka kidedea baada ya kuipata nyumba kama hiyo, iliyojengwa eneo la Salasala, ambayo pia iko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Nelly, ameipangisha nyumba hiyo kwa kile alichodai mihangaiko yake ya kila siku, ina ngome mkoani Iringa hivyo kwa sasa itamuwia vigumu kuweka makazi yake Dar, badala yake, ameipangisha na fedha anazopata, zinamsaidia kuwasomesha watoto wake wawili wanaosoma shule binafsi.

 

Kabla ya kupatikana kwa mshindi wa awamu hii ya pili, bahati nasibu hiyo ilifanya droo ndogo tano katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, ambako wasomaji zaidi ya 30 walijipatia zawadi kemkem, zikiwemo pikipiki, ving’amuzi, televisheni flat screen, simu za kisasa za mikononi, kofia na fulana.

Leave A Reply