The House of Favourite Newspapers

Msichana wa Miaka 9 Mwenye Kipaji Kilichomvutia Rais Kenyatta

Sheila na picha ya rais Uhuru kenyatta

Sheila akiwa na picha ya Rais Kenyatta aliyoichora.

SHEILA SHELDON NI msichana mwenye  umri wa miaka tisa tu lakini uchoraji wake ni wa kiwango cha juu ukilinganishwa na watoto wa rika lake.

Yeye huchora picha ili kujifurahisha lakini cha kushangaza ni kwamba licha ya kuanza uchoraji akiwa na umri wa miaka sita hajapata mafunzo yoyote ya uchoraji na tayari ameanza kugonga vichwa vya habari baada ya kuchora picha ya Rais Uhuru Kenyatta na kusababisha aalikwe katika ikulu ya rais huyo wa Kenya.Sheilah na gavana wa Mombasa Hassan Joho akishikilia picha yake

Vile vile amewahi kuchora picha za Gavana wa Mombasa, Hassan Joho;  Gavana wa Kwale, Salim Mvurya na mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir. Kipaji cha uchoraji wake kwanza kiligunduliwa katika shule ya kimataifa ya Diani International School.

”Mimi hujihisi vyema ninapochora. Mara nyingine ninapokasirika huangalia kazi yangu na kufurahi,” anasema Sheila.

Mbali na uchoraji, msichana huyo ni mwanamitindo, mbunifu wa mitindo na mshairi.

Sheila akichora
Sheila akiwa kazini.

”Nilipata msukumo wa kufanya kazi hii kutoka kwa rais wa Marekan,i Donald Trump, kwa sababu yeye hupenda watu kufanya kazi na kujisaidia  Ninapochora mimi hufikiria sana familia yangu na vile tunavyoishi na lengo langu ni kuimarisha hali yetu ya maisha” anaendelea kusema.

Mamake Sheila ambaye ni afisa wa Magereza anasema kwamba wamepata ufanisi mkubwa kimaisha tangu kipaji cha Sheila kigunduliwe.

Anasema kwamba kipaji chake kinatoka kwa Mungu na kwamba anataka kuwa mchoraji mkubwa wa wanasesere katika kampuni ya Disney nchini Marekani.

Lakini Sheila anapima vipi masomo yake na uchoraji?  Tulipata fursa ya kuzungumza na mama’ke ambaye anasema kuwa kila mwanawe anaporudi nyumbani kutoka shule  hufanya kazi yake ya shule na baadaye kuanza kuchora.

”Sheila hawezi kukosa kuchora, na yeye huhakikisha kuwa anachora picha moja kwa siku kabla ya kulala, ” mama’ke Sheila ambaye ni ofisa wa Magereza anasema na kuongeza kwamba wamepata ufanisi mkubwa kimaisha tangu kipaji cha Sheila kigunduliwe.

”Tunashukuru kwamba tangu Rais Uhuru Kenyatta alipomjua Sheila kupitia mchoro wa picha yake aliochora,  maisha yetu yamebadilika. Mimi nimepandishwa cheo kazini na mume wangu akipatiwa kazi ya kudumu katika halmashauri ya bandari nchini Kenya,” anasema.

Tulimuuliza kuhusu hisia zake za kwanza alipogundua kwamba mwanawe ana kipaji  naye akajibu:

”Kwa kweli mimi huwa siamini, humuona mwanangu kama mtu aliyebadilika, sijui hizi fikra za kuchora zinatoka wapi kwa sababu hakuna mtu anayeweza kuchora katika familia yetu.  Baba’ke hawezi hata kuchora picha ya  mguu,” anasema akitabasamu na kucheka.

Shuleni,  mwalimu wake Sheila aitwaye Quinta Ndeche,  anasema kuwa ni mwanafunzi mwenye tabia tofauti ikilinganishwa na wanafunzi wenzake na ni mtu anayejituma.

Anasisitiza kuwa ni mwanafunzi mtulivu anayependa masomo yake na wakati wa kufanya kazi zake.

Kwa fahari, mwalimu Quinta anasema shule hiyo inajitahidi kukuza kipaji chake kupitia vikao mara kwa mara na mwalimu wa sanaa.

Comments are closed.