The House of Favourite Newspapers

Msoto Wa Mbowe Mwanzo Mwisho

0

KAULI mbiu ya kukumbukwa katika kesi iliyokuwa ikimkabili mwenyekiti wa chama cha upinzani Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ni “Mbowe Siyo Gaidi.”

 

Mbowe aliyekuwa akishtakiwa na wenzake waliokuwa wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mohamed Ling’wenya, Halfan Bwire na Adam Kasekwa, alikamatwa jijini Mwanza usiku wa kuamkia Julai 21, 2021, siku ambayo kulikuwa kufanyike kongamano la kudai katiba mpya lililokuwa limeandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).

 

Usiku huo, Mbowe alianzisha rasmi safari ya kupigania haki kutoka mikononi mwa polisi hadi kwenye Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo ilipelekewa tuhuma kuwa Mbowe na wenzake watatu walikuwa wakikabiliwa na kesi ya ugaidi.

 

Kesi hiyo namba 16/2021, kwenye Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imekuwa ikigusa hisia za wengi huku baadhi wakidai kuwa mashitaka hayo dhidi ya kiongozi huyo wa kisiasa “yalipikwa”.

 

Siku chache kabla ya kukamatwa kwake, Polisi jijini Mwanza ilitangaza kuzuia kufanyika kwa kongamano lao kwa sababu za kiusalama, lakini Mbowe alijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kutangaza kwamba kongamano hilo lipo palepale na litafanyika licha ya zuio la polisi.

 

“Kama polisi wanataka kutuzuia wajiandae kufanya hivyo wakiwa tayari kutukamata viongozi na wanachama wote kwa sababu sote hatutaondoka Mwanza hadi tufanye kongamano la katiba mpya,” alisisitiza Mbowe katika mkutano huo na wanahabari.

 

Wafuasi wengine zaidi ya 10 waliokamatwa pamoja na Mbowe jijini Mwanza waliachiliwa huru na jeshi la polisi, ambapo Mbowe aliendelea kushikiliwa kabla ya kuunganishwa na wanaodaiwa kuwa walinzi wake kwenye kesi ambayo leo Machi 4 mwaka huu, mwendesha mashitaka mkuu wa serikali (DPP), amesema hana nia ya kuendelea kumshitaki Mbowe na wenzake ambapo kwa msingi huo watuhumiwa hao wanatakiwa kuachiwa huru.

 

Katika kesi hiyo, Mbowe anadaiwa kula njama ya kutenda kosa la ugaidi kati ya Mei na Agosti, 2020 akiwa katika Hoteli ya Aishi mkoani Kilimanjaro.

Kosa la pili la Mbowe ni kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi kinyume cha sheria ya ugaidi, kosa alilodaiwa kulifanya kati ya tarehe hizo tajwa.

 

TUJIKUMBUSHE

Julai 21, 2021; Mbowe alikamatwa na kupelekwa “kusikojulikana” ambapo chama chake kiliwataka wafuasi wake kuingia mtaani kumtafuta baada ya juhudi za kumtafuta kukwama.

 

Baadaye, polisi walikuja kuthibitisha kukamatwa kwake na kwamba amesafirishwa kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam na kuunganishwa kwenye kesi ya ugaidi.

 

JULAI 26, 2021 Mbowe na wenzake walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka mawili ikiwemo la ugaidi.
Baada ya kusomewa maelezo, Mbowe hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka, kesi ikaahirishwa hadi Agosti 5, 2021.

 

Agosti 6, 2021, Mbowe alisomewa mashitaka; safari hii hayakuwa mawili tena bali yaliongezeka na kufikia sita; yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa kufanya vitendo hivyo.

Mashitaka mengine ni kukusanya fedha kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi kinyume cha sheria.

Kati ya mashtaka hayo sita, Mbowe alikabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi.

Agosti 9, 2022, Rais Samia Suluhu Hassan, licha ya kusema hawezi kuzungumzia zaidi kesi hiyo kwa kuwa iko Mahakamani, aliiambia BBC kuwa mashitaka dhidi ya kiongozi huyo wa Upinzani hayakuchochewa kwa sababu za kisiasa.

Septemba 03, 2021, kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ikitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambayo haikuwa na mamlaka ya kuisikiliza kisheria.

Septemba 6, 2021, Jaji Elinaza Luvanda alijitoa kusikiliza kesi hiyo kufuatia maombi ya Mbowe, kwa niaba ya washitakiwa wenzake kudai kuwa hawana imani na jaji huyo ambapo Jaji Mustapha Siyani alichukua nafasi ya Luvanda.

Oktoba 20, 2021, Jaji Mustapha Siyani kama ilivyokuwa kwa Luvanda naye alijitoa kusikiliza kesi hiyo kufuatia kuteuliwa kwake kuwa Jaji kiongozi. Jaji Joachim Tiganga akachukua nafasi yake.

Februari 13, 2022, ushahidi wa mashahidi 13 wa upande wa mashitaka kumaliza kutoa ushahidi wao na kilichokuwa kinachosubiriwa ni uamuzi wa mahakama hiyo kuamua kama Mbowe na wenzie wana kesi ya kujibu ama la.

Februari 18, 2022, Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilimkuta Mbowe pamoja na wenzake watatu wana kesi ya kujibu.

MBOWE ALIVYOTETEWA
Mbali na kuwepo kwa watetezi wengi walioshiniza kiongozi huyo aachiwe huru; Zitto Kabwe Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, katika kikao cha wadau wa siasa kilichofanyika Dodoma alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia namna ya kumnusuru kiongozi huyo wa chama cha upinzani.

Akijibu suala hilo Rais Samia alitaka mahakama ipewe uhuru katika kulimaliza shauri la Mbowe.
Licha ya ombi la Zitto kuzua zogo kwa baadhi ya wafuasi wa Mbowe waliotaka aachiwe bila masharti kutokana na kile walichodai “hana hatia”.

Makamu wenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia nchini Ubelgiji naye alimuomba rais huyo kuangalia namna ya kumsaidia Mbowe.

Juzi viongozi wa dini katika kikao chao na mkuu huyo wa nchi nao walimsihi rais Samia kutumia uwezo alionao kumsaidia Mbowe.

 

MBOWE HURU
Wakati shauku ya wingi ikiwa ni kuona namna ambavyo Mbowe na wenzake wataanza kujitetea leo mahakamani DPP alikuja na hoja iliyoibua shangwe kila kona kwamba hana haja ya kuendela na kesi iliyokuwa ikimkabili Mbowe na wenzake na hivyo kuwaachia huru.

Ingawa Mbowe na wenzake hawakuwepo mahakamani wakati wanaachiwa huru, shangwe iliibuka miongoni mwa wafuasi wake huku taarifa za tukio hilo zikienea kama moshi na kujadiliwa kwa mapana kwenye mitandao ya kijamii.

Richard Manyota

Leave A Reply