The House of Favourite Newspapers

Mtandao Wa Accelerate Afrika Wazinduliwa Rasmi Nchini Tanzania

0
Mratibu wa mtandao wa Accelerate Africa, Pendo Lema (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kwanza wa wafanyabiashara wadogo wanaonza kuwekeza na wale wa vikundi vya Wafanyabiashara wadogo na wa kati Jijini Dar es Salaam ambapo pia mtandao huo ulizinduliwa rasmi nchini Tanzania. Kulia ni Mratibu wa Mtandao huo Barani Africa, Gilbert Ewehmeh.

Accelerate Africa, mtandao unaohusiana na maswala ya    maendeleo na ukuaji wa kiuchumi na ambao unahusisha wataalamu waliobobea kwenye maswala ya kuibua, ufuatiliaji na ukuaji maswala ya kiuchumi Barani Afrika leo umezindua rasmi shughuli zake nchini Tanzania.

Uzinduzi huo unaifanya Tanzania kwa nchi ya tatu kufanya uzinduzi huo kati ya  mataifa 10 ambayo yanaunda mtandao huo.

Mtandao huo unawahusisha watendaji waliobobea kwenye mataifa yao na ambao utendaji wao umekuwa wa ufanisi mkubwa katika asasi za kiraia na pia wamepata mafanikio makubwa kama wafanyabiashara na wengine kama watendaji wazuri katika Serikali kwenye mataifa yao.

Mfaniko hayo ni pamoja na katika kuunda kizazi kipya cha viongozi katika maswala ya kiuchumi ambacho kitazingatia maswala ya ukuaji wa miundombinu, kilimo biashara, nishati na mabadiliko ya kidijitali katika kuelekea ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Uzinduzi huo ulienda sambamba na mkutano wa kwanza wa wafanyabiashara wadogo wanaonza kuwekeza na wale wa vikundi vya Wafanyabiashara wadogo na wa kati, ambao walikutana Jijini Dar es Salaam na kuwatanisha wqashiriki 100 kutoka sekta mbalimbali kwa ajili ya kubadilishana na kushauriana kuhusu maswala yanayohusiana shughuli za kifedha, uwekezaji na uanzishaji wa viwanda kuelekea ushiriki wao katika Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).

Akizindua mtandao huo, Mratibu wa Accelerate Africa kanda ya Afrika Gilbert Ewehmeh alisema, “Mfumo wetu huu unalenga kuunda biashara endelevu kwa nia ya kuimarisha sekta ya viwanda ili kuondoa umasikini na kuhakikisha uwapo wa uchumi endelevu”.

Alisema mtandao huo umejikita zaidi Barani Afrika kutokana na ukweli kuwa changamoto zinazohusiana na maswala ya kiuchumi barani humo hazitofautiani na kwamba ni wakati mwafaka kwa wanachama kutumia fursa zinazotokana na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika ambazo amesema nchi nyingi hazina ufahamu  kuhusiana na fursa hizo.

“Lazima tuanze na vikundi vya wafanyabiashara wadogo na wale wa wa kati kwani wengi wao bado hawana uelewa wa fursa nyingi za biashara zilizoko na ambazo wakizifahamu na kuzitumia watanufaika zaidi”, alisema.

Kwa upande wake Mratibu wa Accelerate Africa nchini Tanzania Pendo Lema, alisema hatua hiyo mpya itawasaidia wafanyabiashara wadogo na wa kati kuchangamkia fursa zilizoko kwa kupata uelewa wa kutosha kuhusiana na maendeleo ya kibiashara ulimwenguni.

“Accelerate Africa inatarajia kufanya mkutano mkubwa Juni, mwaka huu, ambapo nchi zote wanachama watalazimika kuchagua wawakilishi watatu kila mmoja; hapa nchini wawakilishi hao itabidi wapatikane kwa njia ya ushindani utakaoandaliwa na mamlaka husika”, alisema.

Aidha mtandao huo pia una mpango wa kuanzisha programu itakayojulikana kwa jina la ‘Operesheni ya mafunzo kwa wajasiriamali 100,000 kwa nchi zote 10 ambayo pamoja na mambo mengine italenga kuwapa washiriki kupata ufadhili wa kifedha, lengo kuu ni kuhakikisha kila nchi mwanachama inakuwa na wafadhili wa uhakika.

Nchi ambazo ni wanachama wa mtandao wa Accelerate Africa ni pamoja na Botswana, Cameroon, Malawi, Ghana, Rwanda, Afrika Kusini, Uganda, Kenya, Tanzania na Zimbabwe.

Mtandao huo tayari umezinduliwa rasmi katika nchi za Cameroon na Rwanda, ambapo kwa uzinduzi huo hapa nchini unaifanya Tanzania kuingia kwenye orodha ya mataifa ambayo yashafanya uzinduzi huo.

Leave A Reply