The House of Favourite Newspapers

MTOTO ALIA: MSINIACHE NIFE

MIMI nakufa.” Inasikika sauti ya mtoto akiugulia maumivu huku mwili wake ukiwa umekonda kupita maelezo; wanaomsaidia wanamfariji kwa kumuambia kuwa hutakufa na yeye anasikika akisema “Msiniache nife,” bila shaka hii ni habari ya kusikitisha ambayo Risasi Jumamosi limeipata.

 

Tusijidanganye ndugu, afya ni kila kitu kwa kweli; hakuna cha mali, usomi wala nini; ikitetereka, gia za maisha haziingii kabisa.

Ukimuona na kumsikia mtoto Rajabu Omary (20) Mkazi wa Isamilo jijini Mwanza anayeteseka na ugonjwa kwa mwaka wa nne sasa utakubaliana na ukweli kwamba; kosa vyote lakini afya uwe nayo. Mama mzazi wa Rajabu aitwaye Mariamu Juma aliliambia gazeti hili kuwa mwanaye alianza kudhoofu mwili kama mchezo; kwamba kuna wakati alikuwa akiamka anahisi uchovu na kulalamikia maumivu ya miguu, basi ndiyo ikawa safari iliyomfikisha mahali ambapo hawezi kusimama mwenyewe wala kukaa.

 

 

Kinachomsumbua mtoto huyo kwa mujibu wa ripoti za kitabibu alizozielezea mama yake ni ugonjwa wa kansa ya damu; aliupataje na kwa sababu gani? Haijulikani lakini ukweli unabaki kuwa mateso anayokutana nayo Rajabu usiombe yakukute. Mama yake anasimulia kuwa awali alipoona afya ya mwanaye inaendelea kuwa mbaya alimpeleka Hospitali ya Sekou Toure ambako alitibiwa bila kupona.

 

“Iliposhindikana hapo tukaenda hospitali ya jeshi ambapo nako walishindwa kuugundua ugonjwa jambo lililotulazimu kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyoko Mwanza kwa ajili ya vipimo zaidi. “Kutokana na ugonjwa, Rajabu amekatiza masomo akiwa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Mbugani, jambo ambalo linaniumiza sana,” alisema Mariamu.

 

Aliongeza kuwa, baada ya kufanyiwa vipimo katika hospitali hiyo ya Bugando ndipo alipogundulika kuwa na ugonjwa huo ambao hivi sasa unamtesa usiku na mchana. “Hivi unavyomuona hawezi kufanya chochote, ni mtu wa kulia maumivu muda wote, kuna wakati hatulali kwa ajili ya kumuuguza,” mama wa mtoto huyo anazungumza kwa huzuni.

Kutokana na hali ya mtoto huyo kuwasikitisha wengi, hivi karibuni Mtangazaji wa Kipindi cha Flora Nitetee, Flora Lauo  aliweka kwenye mtandao wake sehemu ya video ya mahojiano kati yake na mtoto huyo ambayo ilizidi kuwagusa wengi akiwemo msanii Nasibu Abdul ‘Diamond.’

 

Katika kuonesha kufungua njia na kuhamasisha wasamaria wema wamchangie fedha za matibabu Rajabu, Diamond alikabidhi mchango wake wa fedha (kiasi kinahifadhiwa) kwa mtoto huyo huku akiahidi kuendelea kufuatilia afya yake kwa ukaribu. Akimshukuru Diamond, mama wa mtoto huyo alisema: “Nashukuru kwa msaada, naomba wenye kuguswa na ugonjwa wa mwanangu wanisaidie ili nipate fedha ya kumuuguza.”

Kwa mtu yeyote anayeguswa na ugonjwa wa Rajabu anaweza kuwasiliana na wahusika kwa namba zifuatazo; 0753 773786.

DIAMOND ATUA SUMBAWANGA KWA NDEGE, MAPOKEZI YAKE BALAA! (VIDEO)

                  PART 1

 

                 PART 2

Comments are closed.