The House of Favourite Newspapers

MTOTO BEAUTY ALIYEIBIWA KISHA KUPATIKANA, WAZAZI WATOA FUNDISHO

DAR ES SALAAM: Tukio la mtoto Beauty Yohana wa Mbezi jijini Dar kuibwa katika mazingira ya kutatanisha akiwa kanisani kisha kupatikana mzima limetikisa ambapo wazazi wa mtoto huyo wametoa fundisho kwa wazazi wengine kuhusiana na utekaji wa watoto.

 

Wakizungumza na Risasi Jumamosi, wazazi hao, Yohana Isango na Lucy Mganga walisema, wanamshukuru Mungu kwa kumpata mtoto wao akiwa salama, lakini wameingiwa na hofu kubwa kutokana na maelezo ya binti aliyekamatwa na mtoto wao.

“Furaha tuliyonayo hailezeki, lakini tumejifunza kitu kikubwa sana na tungependa hata wazazi wengine wapate fundisho kupitia tukio hili. Huyu binti aliyekutwa na mtoto anasema ilikuwa akamtoe kafara kwa bibi yake sijui wapi huko, hii inatisha sana.

 

“Kwa hiyo wazazi wanatakiwa kuwa makini sana na watoto wao, kila wanapokuwa wawawekee ulinzi kuhakikisha wako salama. “Ninachokifanya sasa hivi ni kuhakikisha namuangalia kwa makini mwanangu, pia nahakikisha hatoki mbali na nyumbani, ndivyo wanavyotakiwa kufanya na wazazi wengine.

“Kingine ninachowashauri Watanzania ni kuwaweka watoto katika misingi ya imani na kuomba kwa Mungu awalinde, yaani tuwe tunawakabidhi mikononi mwa Mungu, maana tunaweza tukawalinda tukaweka mageti, tukaweka mbwa, lakini kumbe bado adui yupo, anaweza akatumia njia nyingine.

 

“Mimi mwanangu aliweza kufuatwa kanisani, hebu fikiria, kwa hiyo kikubwa tuwaombee watoto wetu ili Mungu azidi kuwaweka salama hata adui anapotokea awakinge,” alisema Lucy.

Naye baba wa mtoto huyo, Yohana Isango alisema anazidi kumshukuru Mungu kwa kumrejeshea binti yake akiwa salama huku akitoa pia wito kwa wazazi wengine. “Kikubwa ni shukrani kwa Mungu, lakini niwausie wazazi wenzangu kwamba, lililotupata linaweza kumpata mwingine, kikubwa tuwe makini katika kuwalinda watoto wetu,” alisema baba huyo na kuongeza:

 

”Ukianza kufuatilia jinsi mtoto wangu alivyopona, utajua ni Mungu ndiye kapenda mwanangu asitolewe kafara, kwa sababu yule binti alisema kwamba ili kafara ikamilike ni lazima huyo mtoto wanayemchukua anyolewe nywele kwanza, lakini kwa mwanangu hakufanikiwa kwa sababu kila saluni aliyokuwa anampeleka kunyoa alikuwa anakuta foleni na alishazunguka saluni kama mbili akakuta foleni, kwa hiyo ni jambo la kumshukuru Mungu sana.” 

STORI: Zaina Malogo na Memorise Richard, Risasi Jumamosi.

Comments are closed.