The House of Favourite Newspapers

Mtoto wa Mchungaji Apewa Kipigo Kanisani, Apasuliwa Kichwa

 

DUNIA inatisha! Katika hali ya kushangaza mtoto wa mchungaji wa Kanisa la Emmaus Bible Church Pentecost lililopo Mlandizi, Pwani, Kalebu Ipyana hivi karibuni alijikuta akijeruhiwa vibaya kwa kupewa kipigo kikali na kupasuliwa kichwa baada ya kuvamiwa kanisani.

 

Akizungumza kwa huzuni baba mzazi wa kijana huyo, Ipyana Mwanginda akiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa mwanaye, alisema tukio hilo lilitokea wiki iliyopita ndani ya kanisa lake lililopo Mtaa wa Polisi ya Zamani ambapo vijana wawili waliingia kanisani hapo mchana wakijifanya ni waumini ambapo waliingia kwa staili ya kuimba na kucheza.

 

Baada ya kuingia kanisani hapo kijana wake huyo alikuwa dukani akinunua maji ya kunywa na aliporudi ndani ya kanisa aliwakuta vijana hao wakifunga vyombo vya muziki na simu yake wakitaka kuondoka navyo na ndipo akaanza kupambana nao kwa kuwanyang’anya.

 

Purukushani zilizidi ndipo mchungaji huyo naye akasikia akiwa ofisini kwake na kutoka mbio ambapo aliwakuta vijana hao wawili wakimshambulia mwanaye kwa kipigo kikali hivyo naye akaanza kupambana nao na kufanikiwa kumdhibiti mmoja na kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Mlandizi.

 

“Tulipambana nao sana maana hakuna hata mtu aliyejitokeza kuja kutusaidia kwani watu wa mtaani hapo wanawaogopa sana vijana hao, mmoja alikimbia na mwingine nilimkamata na kumpeleka kituo cha polisi,” alisema mchungaji Ipyana.

 

MTOTO APASULIWA KICHWA

Licha ya kipigo cha nguvu walichompa mwanaye bado walimpasua kichwa kwa jiwe kubwa ambapo vipimo vilionesha kwamba damu ilivilia kwa ndani ya kichwa.

 

“Nilienda polisi Mlandizi na kupewa PF3 ambapo nilimkimbiza mwanangu Hospitali ya Mloganzira iliyopo Kibamba lakini akahamishiwa Muhimbili ambapo alifanyiwa upasuaji wa kutoa damu kwenye kichwa ili isiingie kwenye ubongo.

 

“Namshukuru sana Mungu kwa kuwa mwanangu anaendelea vizuri baada ya upasuaji maana alivyopigwa alizimia kama dakika kumi nikawa nimechanganyikiwa kwa kweli maana mwanangu ninaye mmoja tu wa kiume, mwingine ni wa kike,” alisema mchungaji huyo.

 

Kwa upande mwingine, mchungaji Ipyana aliiomba sheria ifuate mkondo wake kwani vitendo hivyo vya kihalifu siyo vizuri kwenye nyumba za ibada.

 

Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Kamanda wa Mkoa wa Pwani, ACP Jonathan Shanna na kumuuliza kuhusu tukio hilo ambapo alisema taarifa hazijamfikia ila atalifuatilia.

STORI: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko.

Comments are closed.