The House of Favourite Newspapers

MUME WA MJAMZITO ATEKWA USIKU! -VIDEO

Neema Sanga.

 

BADO pepo mchafu wa utekaji yupo kazini hivyo anahitaji kukemewa! Wakati mke wa Mwandishi wa Habari wa Kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communication, Azory Gwanda, Anna Pinoni akiteseka baada ya mumewe huyo kudaiwa kupotea tangu Novemba 21, mwaka jana, mwanamama Neema Sanga naye yupo kwenye hali mbaya kufuatia mumewe kudaiwa kutekwa usiku.

 

Neema ambaye ni mjamzito wa kujifungua muda wowote anayeishi Kibamba-Hospitali jijini Dar, hivi karibuni aliangua kilio mbele ya gazeti hili kuwa, anateseka na watoto wake wawili huku akiwa mjamzito baada ya mumewe huyo, Cilian Ndesamburo au Ndesa kutoonekana nyumbani tangu usiku wa Januari 16, mwaka huu.

 

Huku akisimulia kwa machungu, Neema alisema kuwa, siku hiyo walikuwa ndiyo wamehamia kwenye makazi yao mapya maeneo hayo ya Kibamba wakitokea Ubungo jijini Dar walikokuwa wakiishi awali.

 

Alisema kuwa, baada ya kushusha vitu kwenye ‘kenta’, hata kabla ya kuvipanga ndipo tukio hilo lilipojiri ambapo yeye (Neema) alikuwa amejipumzisha kwenye moja ya vyumba kutokana na uchovu wa kuhama na hali yake ya ujauzito.

Mke wa Azory Gwanda, Anna Pinoni.

SIMULIZI INATISHA

Alisimulia: “Wakati huo mume wangu alikuwa sehemu ya sebuleni. Mimi niliendelea kupumzika na hata nilipoamka, niliendelea na shughuli ya kuwahudumia wanangu wawili ambao nimejaliwa kuzaa na Ndesa, ukiachilia mbali niliye naye tumboni.

 

“Lakini ghafla nilishtuka kuona watu nisiowafahamu wanaingia ndani na kuanza kunihoji alipo mume wangu.

 

“Kiukweli nilichanganyikiwa kwa sababu sikujua nini kinaendelea. Niliwaambia kuwa mimi nilikuwa nimepumzika chumbani na yeye alikuwa sebuleni.

“Walinipiga sana, ilibidi nikimbilie kwa kiongozi wa serikali ya mtaa ambaye alipofika walimwambia kuwa ninamficha mume wangu, lakini nilimwelewesha mwenyekiti akanielewa.

Azory Gwanda.

 

“Baada ya mateso mengi huku wakipekua kila kona ya nyumba, niliwaona wakiwa wamebeba vitu kutoka chumbani kwetu hasa vile vilivyohusiana na ‘documents’ kisha walinikamata na kuniambia twende kituoni nikaeleze alipo mume wangu.

 

“Wakati ninapelekwa kituoni, nilipofikishwa barabarani ndipo nikagundua kuwa watu wale hawakuwa wachache bali walikuwa wamejaa kwenye gari lililokuwa limeegeshwa barabarani.

“Nilipakizwa kwenye gari, lakini sikumuona mume wangu, nilipofikishwa kwenye Kituo cha Polisi cha Mbezi- Kwayusuf, walinitelekeza na kuondoka na vitu vyangu.

 

ATUPWA NDANI

“Kweli, baada ya kuchukuliwa maelezo na kueleza namna tulivyofika pale nyumbani na mume wangu kutoweka kisha watu hao kunivamia na kuniambia niseme alipo mume wangu, bila kujali hali yangu ya ujauzito, nilitelekezwa hapo kituoni hadi asubuhi huku nikiliwa na mbu pamoja na hali niliyokuwa nayo (ujauzito mkubwa). Nilijua siku ile ndiyo kifo changu kilikuwa kimefika maana nilikuwa ninatetemeka mno.

 

“Ilipofika asubuhi alitokea mkuu wa kituo na kuuliza nilikuwa na shida gani na nikiwa katika hali ile.

“Yule mkuu wa kituo alinihurumia na kunitafutia wasamaria wema ambao walinisaidia kunirudisha nyumbani.

 

MAJANGA JUU YA MAJANGA

“Kufika nyumbani ndipo nilipokutana na majanga juu ya majanga. Kumbe wakati wale watu waliponivamia nyumbani walichukua kila kitu cha maana kule chumbani zikiwemo simu zangu mbili na ada za shule za watoto shilingi milioni moja na laki sita na picha zangu zote na mume wangu hivyo sina picha hata moja.

 

“Hapo ndipo nilipochanganyikiwa kabisa maana nilikuwa sina nyuma wala mbele. Nilikuwa sina hata senti tano ya kulisha watoto. Kiukweli nimepitia mateso makubwa sana. Hata nikikumbuka roho inauma mno (akitokwa machozi).

 

AMETEKWA NA WASIOJULIKANA

“Basi kuanzia hapo ndipo nikaanza kumtafuta mume wangu kila mahali huku nikiambiwa atakuwa ametekwa na hao watu wasiojulikana.

 

“Lakini kuna siku alinipigia simu, akaniuliza watoto wanaendeleaje, nikamwambia kabla ya yote aniambie sehemu alipo, akasema nisijali yupo salama, lakini anahofia kuwa atauawa na hao watu wasiojulikana.

“Baada ya hapo hakupatikana tena. Nimeshahangaika sana kumtafuta mume wangu, ninakumbuka kuna

siku nilizimia pale kituoni Mbezi-Kwayusuf, nilipozinduka, nilikuwa na hali mbaya sana. Kila mtu alikuwa akinionea huruma kama unavyoniona nilivyochoka hivi (akishika tumbo lake kubwa).

 

AMWANGUKIA IGP, JPM

“Kabla ya kuamua kutulia na kuacha nione Mungu akitenda kazi ya kumrejesha mume wangu, nilikwenda mara kadhaa kwa Mambosasa (Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa), yeye aliniambia analishughulikia suala langu, lakini bado naona yupo kimya.

 

“Ninachomuomba Mambosasa anisaidie nimpate Mungu wangu. Siyo Mambosasa tu, hata IGP Simon Sirro au Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’, ninawaomba chondechonde, nipo chini ya miguu yao wanisaidie.”

 

CHANZO NI NINI?

Gazeti hili lilipombana kujua nini chanzo cha kuamini kuwa mumewe huyo ametekwa, Neema ambaye ni mjasiriamali alifunguka: “Najua, mume wangu ni mtaalam wa IT (Information Technology) na mambo ya kompyuta kwa jumla.

 

“Ameshafanya kazi nyingi za kimtandao hivyo inawezekana watu hao wanajua ana ishu zao nyeti. Mimi ninahisi hivyo, lakini sina uhakika sana isipokuwa polisi ndiyo wanaweza kunisaidia.”

 

MAMBOSASA HEWANI

Baada ya kusikia simulizi ya Neema ambaye sasa unakwenda mwezi wa pili bila kumuona baba watoto wake na bila kujua alipo, gazeti hili lilimtafuta Kamanda Mambosasa na kumuuliza kama analifahamu sakata la Neema ambapo alikuwa na haya ya kusema:

 

“Hilo ni jambo zito na kila kanda ina kamanda wake wa polisi. Ni vizuri akaanzia kwa makamanda wa chini halafu suala lake litanifikia. Kama kweli alishafikisha malalamiko ofisini kwangu na akaahidiwa kuwa yanafanyiwa kazi, basi ni kweli yatakuwa yanafanyiwa kazi.”

 

HOFU YA UTEKWAJI

Hivi karibuni kumekuwa na hofu ya watu kutekwa tangu kupotea kwa aliyekuwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane, kutekwa kwa msanii Roma Mkatoliki na wenzake, kutoweka kwa Azory, mfanyabiashara maarufu wa Temeke, Francis Mohamed na wengineo.

 

Neema Sanga amejifungua usiku wa kuamia leo.

Stori: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko.

 

INATISHA! Mume wa Mjamzito Atekwa Usiku!

Comments are closed.