The House of Favourite Newspapers

Mume Amuua Mkewe kwa Jembe

Mume.

HALI ya sintofahamu imewakumba wananchi wa Kitongoji cha Magharibi na wananchi wa Kijiji cha Mwibagi katika Kata ya Kyanyari, wilayani Butiama mkoani Mara baada ya mkazi mmoja wa kitongoji hicho, Fungwa Busia (47) kudaiwa kumpiga kwa jembe mkewe aitwaye Roza Fungwa (46) pichani na kumuua na kisha kwenda kuuzika mwili wake kusikojulikana.

 

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo la aina yake wak­iwemo watoto wa mtuhumi­wa huyo walieleza kwamba, tukio hilo la kinyama lilitokea Aprili Mosi, mwaka huu, siku ya Sikukuu ya Pasaka majira ya saa 2.30 usiku, ambapo mtuhumiwa huyo inaseme­kana kuwa alianza kumpiga mkewe huyo kwa kutumia ubao kisha akachukua jembe, akaanza kumpiga mbele ya watoto wake na baada ya kipigo kikali, akapoteza fahamu.

Mke.

Walieleza kuwa, baada ya mama huyo kuanguka chini na kupoteza fahamu mbele ya watoto wake ambao wal­ianza kulia kwa machungu, mtuhumiwa huyo aliwaamuru waingie ndani ya nyumba wakalale hata bila kupata chakula cha usiku wali­chokuwa wakikitayarisha.

Baada ya kuingia ndani ya nyumba, watoto walifunga milango na kubana pembeni ndipo walipomuona baba yao huyo akichukua jembe na kumbeba mama yao begani ambaye alikuwa amelala chini na kuondoka naye kwenda kusikojulikana na kurudi nyumbani peke yake, usiku wa manane.

Aidha, walidai kwamba, mara baada ya tukio hilo, kesho yake ambayo ilikuwa Jumatatu ya Pasaka, majirani ambao walikuwa pembeni wakishuhudia ukatili huo aliokuwa akifanyiwa jirani yao, walikwenda kutoa taarifa kwenye ofisi ya kijiji, ambapo wananchi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwibagi, Moses Stefano walienda nyumbani kwa mtuhumiwa huyo na baada ya kuelezwa kinagaubaga juu ya tukio hilo, wananchi hao waliamua kumkamata mtuhu­miwa huyo na kumpeleka Kituo cha Polisi cha Kiabakari.

Baadaye walirudi kijijini na kupiga yowe na ndipo ilipo­tolewa amri na mwenyekiti kwamba wananchi waanze kumtafuta mwanamke huyo kila sehemu ili kujua mahali alipo, iwe milimani, mapangoni, vichakani na kwenye masham­ba lakini hata hivyo, hakukuwa na mafanikio yoyote.

 

Mashuhuda hao walidai kuwa huenda chanzo cha Fun­gwa kumfanyia unyama huo mkewe ni baada ya baba huyo kumtafutia mchumba mwenye umri wa miaka 60 mtoto wake wa kike mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa) kwa makubaliano ya mahari ya ng’ombe 6.

Baada ya mtoto huyo kukataa kuolewa katika ndoa hiyo ya utotoni na kutoroka nyumbani, huenda baba yake aliamini kuwa mkewe ndiye aliyemzuia binti yake asiolewe ili asipate mahari, hivyo kwa ha­sira ndio akaamua kumfanyia ukatili huo.

 

Hata hivyo, sakata hilo liligeuka kuwa kama mchezo wa kuigiza siku ya Alhamisi wakati polisi wilayani Butiama walipokwenda na mtuhumiwa huyo nyumbani kwake katika Kitongoji cha Magharibi, ambapo baada ya wananchi kuona tukio hilo, walialikana mamia kwa mamia wakiwa na mapanga na kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa huyo waki­amini kuwa polisi walikuwa wamempeleka hapo ili aka­waoneshe mahali alipomzi­ka mkewe.

Polisi kuona umati huo mkubwa wa wananchi ukiwa umezingira nyumbani hapo wakitaka polisi iwakabidhi mtuhumiwa huyo ili wamua­dhibu kwa lengo la kutaka awapeleke mahali alipozika mkewe, polisi iliwahadaa wananchi hao kuwa mtuhu­miwa huyo amewaeleza kuwa amemzika mkewe kwenye shamba lake la pamba lililopo umbali wa kilometa mbili kutoka nyumbani hapo.

 

Baada ya wananchi kuam­biwa hivyo na polisi walitimua mbio kuelekea kwenye shamba hilo kumtafuta mwanamke huyo anayeaminika kuwa ni amezikwa na kuwapa mwanya polisi hao kuondoka na mtuhu­miwa huyo salama.

Hata hivyo, wananchi hao walikosa kuona alipozikwa mwanakijiji mwenzao wakaa­mua kurejea nyumbani hapo wakiwa na hasira kali na baada ya kufika walipigwa butwaa kukuta polisi wameondoka na mtuhumiwa huyo.

Maofisa wa polisi wilayani Butiama wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kukiri kumshikilia Fungwa kwa mahojiano zaidi hata hivyo hawakuwa tayari kueleza kwa undani kwa madai kuwa wao siyo wasemaji wa polisi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, SACP Jafar Mohammed hakupatikana kufafanua tukio hilo, hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwibagi, Moses Stefano ame­kiri kutokea na kushughulikia tatizo hilo.

Stori: Gregory Nyankaira, Mara

Comments are closed.