The House of Favourite Newspapers

MUME MBARONI KIFO CHA MKEWE!

NI shida! Mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Willibafosi William, mkazi wa Mbezi-Makabe, jijini Dar es Salaam amejikuta akitiwa mbaroni baada ya kifo cha utata cha mkewe, Carolina Sospeter William (40) kilichotokea hivi karibuni.

Awali, habari zilienea kwamba Carolina alifariki dunia kwa madai kuwa alikuwa akishushiwa sana kipigo na mumewe huyo hali iliyomsababishia kuwa na makovu mengi mwilini.

Akizungumza na Ijumaa Wikienda mama wa marehemu ambaye hakutaka kuandikwa jina lake gazetini, alidai kuwa mwanaye huyo aliteseka kwa muda mrefu ingawa alikuwa anamficha, lakini alihisi hilo kutokana na kudhoofika sana kiafya na makovu aliyokuwa nayo ambayo yalionesha yalitokana na kujeruhiwa kwa kitu chenye ncha kali.

“Carolina alinipigia simu mwezi wa nne mwaka huu, akaniambia anaumwa mkono, nikamuuliza mkono umefanyaje? Akasema huenda ameulalia vibaya nikamuuliza ameenda hospitali akadai amenunua dawa ya kuchua.

“Siku iliyofuata akaniambia mkono unazidi kuuma. Nikamshauri aende hospitali akaenda. Baada ya muda nilimpigia simu ili kutaka kujua majibu ya hospitali yalikuwaje, akaniambia mkono hauna tatizo lolote na kwa wakati huo majibu yote madaktari walikuwa wanampa mumewe.

“Mwanangu aliendelea kuugua mpaka siku moja mwanaye yaani mjukuu wangu alinipigia simu usiku akaniambia mama yake anaumwa sana, lakini pembeni nikawa nasikia sauti ya mwanangu analia, nikauliza kama naweza nikaongea naye, akasema hawezi hata kuongea.

“Baadaye ikabidi niwatume wadogo zangu waende kumuona, walipofika wanakanipigia simu wakaniambia, dada tumemkuta Carolina amekonda na anaumwa sana mkono, nilipoambiwa hivyo nikaamua kutoka Mwanza na kuja Dar kwa ajili ya kumuuguza mwanangu aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Mloganzila, nilipofika nilimkuta akiwa na hali mbaya tofauti na alivyokuwa akiniambia mumewe kwamba nisiwe na hofu mwanangu anaumwa kawaida tu.

“Nilikuta shingoni amevimba hawezi kula hata kupumua kwake kulikuwa kwa shida, baadaye ikabidi niwaombe madaktari wanipe majibu ya vipimo vya mwanangu, ambapo waliniambia watanipa kesho yake, tukaondoka tukamwacha mwanangu lakini kabla hatujafika nyumbani nikapigiwa simu kwamba Carolina hatupo naye tena duniani,” alisema mama huyo huku akitokwa na machozi

MAMA MDOGO WA MAREHEMU ANENA

Akizungumza kwa uchungu mama mdogo wa marehemu aliyejitmbulisha kwa jina moja la Chiristina alisema alipata taarifa siku chache zilizopita kuwa Carolina ni mgonjwa na alipelekwa Hospitali ya Bochi, Mbezi akiwa na hali mbaya ambapo alifikia chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

“Baada ya madaktari kuhangaika naye kwa muda mrefu wakampa rufaa aende Muhimbili kwa matibabu zaidi, lakini cha kushangaza baada ya kufika Muhimbili kesho yake kabla hata ya kupewa huduma, mume wake alimchukua na kumrudisha tena Bochi bila ridhaa ya madaktari.

“Lakini walipofika naye Bochi madaktari waligundua mgonjwa huyo walishampa rufaa ya kwenda Muhimbili, hivyo kumuamuru mume wa marehemu amrudishe huko, alimuondoa hospitalini hapo na kumpeleka katika Hospitali ya Mloganzila hadi umauti ulipomfika,” alisema.

TIMBWILI LAIBUKA

Kutokana na madai hayo kwamba Carolina alifariki dunia kutokana na kipigo cha mumewe kwani hata majirani walikuwa wakisikia na kushuhudia alivyokuwa anateseka, siku ya mazishi timbwili zito lilitokea na kusababisha Polisi kuingilia kati na kuuchukua mwili wa marehemu na kuondoka nao.

Mmoja wa ndugu wa mwanaume huyo ambaye ni mama mdogo aliyejitambulisha kwa jina la Justina Theones alisema siku waliyotarajia kuzika kesho yake, ilishindikana kwani Polisi walivamia msibani na kumchukua mume wa marehemu pamoja na mwili na kuondoka nao.

“Tulikuwa tumeshamaliza taratibu zote za mazishi lakini ghafla likaja gari la Polisi, Polisi wakashuka na kutupa pole mwisho wakasema wanamtaka baba mwenye nyumba (mume wa marehemu) wakamchukua, wakaingia moja kwa moja mpaka chumbani, wakabeba mwili wa marehemu na kuwaingiza kwenye difenda, mume alipouliza kwa nini anakamatwa wakamwambia aende ataenda kujua hukohuko kituoni, hivyo mpaka sasa ameshikiliwa kituo cha Polisi,” alisema mama mdogo huyo wa mwanaume.

Kwa mujibu wa mama mdogo wa marehemu, mwili wa Carolina ulifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na majibu yatatoka baada ya wiki moja, lakini mwili wa marehemu ulizikwa Jumamosi katika makaburi ya Msakuzi jijini Dar huku mume akiendelea kushikiliwa polisi.

STORI: Mwandishi Wetu, DAR

Comments are closed.