The House of Favourite Newspapers

RIPOTI KAMILI: Vituo vya Masaji Dar Kugeuzwa Madanguro

KWA wasomaji wa gazeti la jana linalochapishwa na Kampuni ya Global Publishers la Ijumaa Wikienda, watakuwa wanaelewa nini ambacho tumeamua kukichimba na kukianika kwa manufaa ya taifa letu. Kwa wewe ambaye ndiyo kwanza unaanza kusoma makala haya iko hivi;

 

Kitengo cha Operesheni Fichua Maovu ‘OFM’ kwa muda mrefu kimekuwa kikifanya uchunguzi na sasa kimethibitisha uwepo wa utitiri wa vituo vingi vya masaji ‘Massage Parlor’ katika miji mbalimbali ikiwemo Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya na kwingineko!

 

Ukikatiza huko mitaani utakutana na mabango kibao yanayotangaza huduma hiyo huku mengi yakiambatana na picha zinazoonesha watu wakiwa wanapatiwa huduma hiyo katika mazingira yanayoshawishi ngono.

 

Yawezekana hata wewe msomaji ulishawahi kujiuliza swali hili, kwamba ni kweli Tanzania kuna uhitaji mkubwa wa vituo hivyo kiasi cha kuwa vingi kila sehemu? Na je, yanayofanyika ndani yake ni yapi? Ni masaji kama masaji tu au kuna biashara nyingine inaendelea?

 

Maswali hayo ndiyo yaliyowasukuma makamanda wa OFM kuzifungia kazi saluni hizo kwa kuanzia na zile zilizopo katika Jiji la Dar.

Katika hatua za awali za kuzungumza na wateja wanaokwenda kwenye vituo hivyo, wengi walikiri kwamba yanayotendeka huko yanatia kichefuchefu.

 

HEBU MSIKIE MTEJA HUYU

“Mimi nilikuwa na tabia ya kwenda kufanyiwa masaji baada ya kushauriwa na daktari kufuatia kusumbuliwa na maumivu ya viungo kila mara.

“Kuna masaji moja ipo pale Mikocheni. Kimsingi lile ni danguro maana ukiingia pale wale wasichana wanaohudumia wateja wanafanya kukugombania, halafu sasa majina wanayokuita ni baby… sweetheart, mume wangu. Sasa kama umeenda kwa ajili ya masaji tu, unadhani utaishia huduma hiyo tu? Mimi mazingira hayo yalinishinda, nikatafuta sehemu nyingine maana mle ni ngono tupu,” alisema kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Jacky.

Hakika hali inatisha sana! Yanayofanyika kwenye vituo hivyo ambavyo vingine vimesajiliwa na Serikali ni kinyume na maadili ya Kitanzania!

Tunasema ni kinyume na maadili kwa sababu baadhi ya vituo hivi badala ya kutoa huduma ya masaji, wanafanya ujanjaujanja wa kutoa huduma ya ngono na matokeo yake sasa, hivi vituo vimepewa jina la maduka ya ngono!

Kwa uchunguzi uliofanywa na OFM, vituo hivi vingi vimekuwa ni maduka ya ngono kwa sababu vitendo hivyo vinafanyika waziwazi. Ili kujua kwamba baadhi ya hivi vituo huduma ya ngono inatambulika na ofisi, wapo baadhi ambao waliwanasa na Polisi wakawa wanaeleza kuwa, wanafanya hivyo kwa sababu ya ugumu wa maisha.

“Mimi nimeajiriwa hapa lakini silipwi mshahara, nilichoambiwa ni kwamba, malipo yangu yatatokana na ujanja wangu na jinsi nitakavyokuwa naongea vizuri na wateja. Yaani akija mteja akataka huduma zaidi ya masaji, nimpatie na

pesa atakayotoa kutokana na tutakavyokubaliana, ni yangu.

“Ni kazi hatari sana lakini hatuna jinsi, tunafanya na tunapata pesa ambazo zinatusaidia kuendesha maisha yetu,” alisema binti mmoja aliyedai anaitwa Suzan ambaye alinaswa na OFM akitoa huduma ya ngono kwenye kituo kimoja kilichopo Sinza Palestina jijini Dar.

Kwa maelezo ya msichana huyo, vitendo vya ngono vinavyofanyika ndani ya baadhi ya vituo hivyo vya masaji, hata wamiliki wanajua. Wanaelewa michezo inavyofanyika na wao wananufaika kwa namna moja ama nyingine.

MSIKIE MMOJA WA WAMILIKI WA MASAJI

Katika kuchunguza zaidi, imebainika kwamba baadhi ya hawa wamiliki wa hizi masaji wanaharibiwa biashara na mabinti wanaowaajiri kufanya kazi hiyo.

“Unajua serikali na jamii kwa ujumla wanaweza kuona sisi tunaanzisha hizi biashara kwa lengo la kujipatia pesa kwa njia haramu. Siyo kweli na naomba niseme tu kwamba, hawa akina dada tunaowachukua kufanya kazi hii ndiyo wanaoleta masuala ya ngono.

“Unamwambia kabisa kwamba unatakiwa kufuata taratibu hizi, unamkataza kushawishika kufanya vitendo vya ngono lakini baadaye unakuja kusikia kanaswa akifanya mambo hayo.

“Hivi mimi hapo kama mmiliki, kosa langu linakuwa wapi? Leseni ya biashara hii ninayo, lakini biashara inachafuliwa na hawa wasichana wenye tamaa ya pesa. Baya zaidi wanapokuwa huko chumbani sisi hatupo, wanakuwa wenyewe, unadhani tunawezaje kuwadhibiti,” anahoji Kizungi James, mmiliki wa kituo cha masaji kilichopo Mbezi Beach jijini Dar. Makala haya yataendelea kwenye Gazeti la Risasi Jumatano kesho. Kumbuka hatupoi mpaka kieleweke.

 

Na Mwandishi Wetu

 

Comments are closed.