The House of Favourite Newspapers

Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili -2

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Nilioga, mwishowe nikatoka zangu lakini miguu ilikuwa ikitetemeka. Nilipofika chumbani nilikutana na jipya tena. Kitandani changu nilikitandika vizuri sana, shuka ilikaza vizuri sana lakini cha ajabu ni kwamba, nilikuta alama ya mtu kukaa na kuondoka bila kuweka vizuri shuka. Halafu juu ya stuli kulikuwa na chupa ya mafuta ya losheni ambayo mimi huyapaka ikiwa imefunguliwa. Ilionesha kwamba huyo aliyekaa kwenye kitanda alikuwa akijipaka mafuta hayo.

Wifi hakuwepo, mashemeji zangu hakuna mwenye tabia ya kuingia mle chumbani, sasa nani?

SASA ENDELEA…

Nilijiuliza sana mpaka ikafika mahali moyoni nikasema labda mama mkwe wangu aliingia kwa siri. Lakini aliingia ili afanye nini? Maana hakuna cha kumhusu.

Basi, niliendelea na mambo yangu mengine. Siku hiyo nilimkumbuka sana marehemu mume wangu. Kwani alikuwa ananipenda sana na aliipenda familia yote kwa ujumla. Hilo nalo lilichangia sana mimi kumkumbuka mume wangu.

Basi, maisha yaliendelea pale nyumbani nikiwa nakutana na viashiria mbalimbali vyenye maswali yasiyokuwa na majibu ya wazi.

Tukiwa tumebakiza siku tatu kabla ya siku ya kumaliza msiba ambapo kweli pombe za kienyeji zilishaanza kupikwa na ndugu waliashaanza kuwasili pale ukweni kwangu, nilipigiwa simu. Nikapokea:
“Haloo.”

Huyo aliyepiga aliposema haloo, nikashtuka sana. Sauti ilifanana sana na ya marehemu mume wangu. Nikatetemeka na kukata simu kisha nikaitupia kitandani na kuikodolea macho.

Wakati huo, siyo simu zote zilikuwa na uwezo wa kutuma au kupokewa meseji. Simu yangu haikuwa na uwezo huo. Mara ilipigwa tena na nikasikia sauti ikiniuliza moyoni ‘kwa nini usipokee ukamuuliza yeye ni nani?’

Nilipokea, akasema: “Samahani, naweza kuzungumza na Petro?”
Nilimuuliza yeye ni nani, akasema anaitwa Isdori. Nikamuuliza wa wapi? Akasema Kigoma. Yaani sauti ni ya mume wangu kabisa. Nilimwambia namba ile si ya Petro. Akaniomba samahani na kukata simu.

Nilimwita wifi yangu chumbani, nikamsimulia. Akashangaa sana, akaomba ile namba, akaipiga. Nilimwona akishtuka hivihivi kutokana na yeye alivyosikia ile sauti. Mwenzangu hakuvumilia, nikamsikia akiuliza:
“Wewe si kaka baba Kisu kweli?”

Sikujua huyo mtu alikuwa akijibu nini, lakini nilikuwa namsikia wifi akisema: “Kweli? Uko wapi kwani? Kigoma! Kigoma unafanya kazi au? Kazi gani? Ohoo! Haya basi sawa. Lakini kusema kweli sauti yako kama ya baba Kisu. Haya kwaheri.”

Alipokata simu wifi alinitumbulia macho huku machozi yakimchuruzika.
“Vipi wifi?” nilimuuliza.
“Mh! Wifi mbona ni sauti ya kaka kabisa! Mimi naanza kuingia shaka kuhusu kifo chake.”

Nilimtaka wifi kuondoa mawazo hayo kwamba huenda kifo cha kaka yake kina mambo mengine lakini yeye alikazania. Ikafika mahali moyoni nikasema siwezi kuendelea kumshawishi kwani mimi ndiye mke isije kusemwa kwamba nahusika bure.

Marehemu mume wangu alikufa kutokana na kuumwa ghafla, siku ya kwanza, ya pili akafariki dunia akiwa palelape kwao ambapo alikwenda kumjulia hali mama yake mzazi aliyekuwa akisumbuliwa na miguu.

Basi, siku ya kumaliza shughuli iliwadia. Watu, hasa ndugu walikusanyika nyumbani wakiwa wamejiandaa kwa tukio hilo maalum. Mimi kwa upande wangu alikuja mdogo wangu wa kike na mwanaye na baba mdogo.

Upande wa mume wangu kulikuwa na ndugu wengi sana. kama mia moja hivi kutoka sehemu mbalimbali. Wengine mjini, wengine vijijini.

Shughuli ilianza saa tano asubuhi ambapo mzee mmoja wa heshima ndiye aliyepewa jukumu la kusema na kuratibu mambo hatua kwa hatua.

Ilifika mahali sasa mimi nilitangaziwa utaratibu wa mila na desturi kwa kabila la mume wangu kwamba siku hiyo natakiwa ijulikane moja. Nikubali kurithiwa au nirudi kwetu na kuwa huru kuolewa na mwanaume mwingine.

Ndugu waliotakiwa kunirithi walikaa sehemu moja ambapo kiuhusiano, walikuwa ni kaka na wadogo wa marehemu. Lakini wengine ukaka au udogo ni wa kutoka kwa baba mkubwa au baba mdogo.

Niliambiwa utaratibu wote endapo nitataka kurithiwa na nani na nifanye nini. Lakini kama sitaki pia nilielekezwa cha kufanya.

Ngoma zilipigwa, wakaimba kikabila. Wengine wakawa wanacheza. Mzee mmoja akashukua kile chombo, kijomela na kwenda kuchota pombe, akasimama nayo, akanywa kidogo kisha kwa heshima na tahadhima alinifuata nilipokaa na ndugu zangu, akanikabidhi kijomela.

Mimi nilisimama, nikamfuata shemeji mkubwa, akanyoosha mikono ili kupokea, nikamkwepwesha, nikamfuata aliyefuatia, akanyoosha mikono, nikamkwepesha.
Niliwafanyia wote hivyo. Kila mmoja alinyoosha mikono huku akiachia tabasamu. Lakini kwa upande wa wale waliokuja na wake zao, wanawake hao hawakuonesha sura ya kunichangamkia.

Hilo hata wifi aliniambia kwa sababu walijua kama nitarithiwa kwa waume zao, mapenzi yangepungua kwao. Kwa hiyo wao kutoka moyoni, hakuna aliyependa mimi nichague mume kwenye ukoo ule.

Nilipoamini nimefika mpaka wa mwisho, nikamwona kijana mwingine anatokea akiwa anakimbia kama anayewahi. Nikaambiwa yule naye ni mwana ukoo anayetakiwa kukutana na zoezi hilo.

Nilimsubiri akae. Alikuwa akivuja jasho mwili mzima. Nikaambiwa sasa naweza kuendelea na utaratibu. Nikamsogelea, nikawa kama namnyooshea mikono ili kumpa kile kijomela, alipotaka kukipokea, nilishangaaa sana kuona sura yake kama ya marehemu mume wangu, yaani vilevile na aliachia tabasamu lilelile, nikashtuka.

Je, nini kiliendelea? Usikose kusoma wiki ijayo mkasa huu unaoitwa Mume Wangu Anaishi Mara ya Pili.

Comments are closed.