The House of Favourite Newspapers

 MUUZA PWEZA ANAVYOMZIDI KIPATO MFANYAKAZI WA BENKI-2

NIKIINGIA wiki ya pili ya safari ya makala haya napenda nianze kwa kuwashukuru wote walionijazia ‘nyama’ makala haya kwenye sehemu ya kwanza.

Kipekee nashukuru kaka yangu Fred Kaonga wa Chamazi, Dar kwa kufuatilia makala haya ambayo leo yanaingia wiki nyingine kwa kuangazia undani wa nini kinachangia vijana wengi kusema hawana kazi ilhali kazi zipo.

Tatizo kubwa linalochangia vijana wengi nyakati hizi kuthamini zaidi kazi za ofisini si jingine ni suala la malezi katika familia.

 

Kabla ya uhuru na ule uhuru wa mwanzoni hatukua na Watanzania wanaotukuza kazi za ofisini kuliko shughuli nyingine katika jamii kama kulima, kuchunga, uvuvi, useremala na uwashi.

Waliotuibia fikra za kupenda kulima na kufuga nyuki wanajulikana; ni wale waliotuletea elimu ya darasani inayotuandaa kufanya kazi ofisini kuliko kuendeleza shughuli nyingine walizofanya wazazi wetu.

Tulipopata uhuru mwaka 1961 kazi ilikuwa ndiyo msingi wa maisha, hatukuwa na vijana wanaozurura ovyo bila kufanya kazi.

 

Hapo ndipo sheria ya uzembe na uzururaji ilipotungwa; kuwadhibiti wanaosema hakuna kazi na kuishia kupiga soga kwenye michezo ya bao na dama inzi hizo.

Na kusema kweli mambo yalikwenda vyema, vijana walishindana kulima, kufuga, kuvua samaki, kujenga nyumba na kutunza familia bila kutindikiwa chakula.

Wanaokumbuka mwanzoni mwa miaka ya themanini Vijiji vya Vjamaa vilivyoanzishwa mwaka 1974 vingi vilijitoshereza kwa chakula na familia zilikuwa bora kimaisha.

Kilichochangia mafanikio hayo kilikuwa ni watu kupenda kufanya kazi bila kuchagua.

Lakini baadaye ulevi wa watu kupenda kazi za ofisini ulipowakolea watu mambo yakaharibika.

Heshima ikawaendea wafanyakazi maofini, mfano waalimu, matarishi, karani na wengineo, zamu ya wakulima kudharauliwa ikafika.

Majina mengimengi ya ovyo walipewa wakulima na wafugaji. Ukisikia: “We mshamba nini?” Ujue umedharaulika.

 

Vijana wengi wakaanza kukataa kudharaulika, wakawa hawapendi kazi za shambani, wakagoma kuvua samaki na wengi wakaanza harakati za kusoma ili waajiriwe serikalini.

Wanaposhindwa kusoma ili wasiitwe washamba wengi waliona bora waje mjini wawe wajanja hata kama hawafanyi kazi.

Taifa likaanza kuzama; wazururaji wakazaliwa kwa wingi na hapo neno la: Sina kazi ndipo lilipoanza kukua kwa sababu kazi za heshima zilishatambulika kuwa ni za maofisini tu!

 

“Soma mwanangu utukomboe. Nenda shule upate elimu uajiriwe. Usiposoma hutapata kazi,” yakawa ndiyo maneno ya kulelea watoto! Leo hii taifa linahangaishwa na shetani liliyemzaa na kumlea.

Taifa letu hivi sasa linao wasomi wengi ambao hawana ajira. Lina vijana chungu nzima wanaozurura mitaani bila kujishughulisha na chochote, wanaogopa kudharauliwa.

Kuuza pweza katika zama hizi za walevi wa kazi za ofisini ni aibu kubwa sana kwa vijana walio wengi.

Kwa kizazi hiki msichana mrembo tena msomi wa chuo kikuu aonekane anapika supu ya miguu ya ng’ombe maarufu kama makongoro, si kazi rahisi!

 

Vijana wengi wanaona ni bora washinde vijiweni wakibishana kuhusu timu za mpira za ulaya kuliko kwenda kubeba zege, kuuza mishikaki, kuchoma mihongo, kutembeza mitumba na hata kufanya usafi majumbani.

Wengi wanaamini kwamba hizo siyo kazi za kufanya.

Ukitafakari; wanazidharau kazi hizi kwa takwimu au ndiyo ulevi wa kupenda kazi za ofisini niliosema huko mwanzo?

 

Maana kazi ina faida gani nyingine kama siyo kukupatia kipato cha kukuwezesha kuishi?

Kama ni hivyo ni nani aliyewaambia kuwa kuuza chakula (mama ntilie) hakuna kipato, kawadanganya nani kuwa ukiuza pweza huwezi kupata fedha za kuendesha maisha yako vizuri hapa mjini?

Ndugu zangu, vijana wenzangu, rafiki na jamaa zangu tusidanganyike; muuza pweza tunayemdharau anaweza kumzidi kipato mfanyakazi wa benki na kuishi maisha mazuri na yenye kutimiza malengo.

Naomba tuseme kwa data! Wakati naandaa makala haya nilizunguka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar kuzungumza na wafanyabiashara ndogondogo ili kujua kama wanapata faida au la!

 

Nilichokibaini ni kwamba, wanaofanya biashara katika maeneo sahihi wanapata faida kubwa kuwashinda wafanyakazi wa ofizini.

Ninazo takwimu nyingi za kimapato za wachoma chips, wakaanga mihogo, wachoma mishikaki, wauza kahawa ambazo zinaonesha kwamba wanajikusanyia fedha nyingi kwa mwezi kuliko baadhi ya wafanyakazi wa maofisini.

Tuchambue hivi: Mshara wa mfanyakazi wa benki kwa makisio yangu kwa mwezi ni sh. 2,000,000 (milioni mbili) ambazo kwa namba, wengi wetu tunaziona ni nyingi.

Lakini mfanyakazi huyo akikatwa kodi ya serikali kwa kiwango cha asilimia 19, atakuwa amekatwa Sh. 482,000 kwa mwezi.

 

Akitoa mchago wa mfuko wa jamii atatakiwa akatwe Sh. 200,000.

Bima ya afya kwa mwezi ni Sh.60,000. Jumla ya makato yote hayo bila kumuwekea mengine madogomadogo kwa mwezi, mfanyakazi huyo atakatwa Sh. 742,100.

Ukichukua mshahara wake ukatoa na makato hayo bwana mkubwa huyo wa benki atajipatia Sh. 1,257,900 kwa mwezi.

 

MUUZA PWEZA niliyezungumza naye eneo la Sinza aliniambia kuwa alianza kuuza pweza kwa mtaji wa Sh. 10,000.

Anasema kwa sasa mtaji wake kwa siku ni Sh. 200,000. Ananunua pweza wa Sh. 180,000. Kuni na vifaa vingine Sh.5,000 kwa siku. Nauli na matumizi madogomadogo kayatengea bajeti ya Sh. 15,000.

Anasema kutokana na wateja kuongezeka mauzo ya vipande vya pweza kwa siku yamepanda, anatapa hadi Sh. 280, 000 kwa siku.

 

Anaeleza mchuzi wa pweza huuza hadi vikombe 70 – 80 kwa 300@, ambapo kimahesabu hujipatia takriban Sh. 21,000.

Ukiyajumlisha mauzo yake kwa siku kwa hesabu hiyo utakuta muuza pweza huyo anaondoka na Sh. 301,000.

Ukitoa gharama yake ya 200,000 fedha anazobaki nazo kwa siku ni Sh.101, 000 ambapo akifanya kazi siku 26 kwa mwezi akiacha siku moja anayopumzika huweza kujipatia kiasi cha shilingi 2,626,000 kwa mwezi. Ukilingasha muuza pweza na mfanyakazi wa benki kimapato utaelewa nilichosema.

Lakini pengine makala haya yamelenga nini? Yamelenga kuwahamasisha vijana, kuifungua jamii nzima kupenda kufanya kazi bila kuchagua. Kazi zote zinaheshima sawa, kikubwa kinachoangaliwa ni faida. ASANTE KWA KUWA NAMI!

 

Na Richard Manyota, Uwazi

Comments are closed.