The House of Favourite Newspapers

Mwaka Mpya, Kila Nchi Husherehekea kwa Muda Wake

how-to-celebrate-new-year-2017

Usiku wa leo, panapo majaaliwa tutauaga rasmi mwaka 2016 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017, lakini je, unajua kwamba wakati tutakapokuwa tunahesabu dakika kuelekea saa sita kamili za usiku, tayari kuna nchi nyingine kibao zitakuwa tayari zimeshauona mwaka kabla yetu?

Unajua pia kwamba kutakuwa na nchi nyingine kibao bado zinasubiri kuuona mwaka? Basi kwa taarifa yako, Mwaka Mpya, japo ni sikukuu moja lakini husherekewa kwa nyakati tofauti duniani kote.

Zipo nchi ambazo zitawahi sana kuuona mwaka na zipo nchi ambazo zitachelewa sana kuuona mwaka! Hiyo yote ni kwa sababu ya tofauti ya majira yanayosababishwa na mstari wa saa wa kimataifa (International Date Line).

Utafiti unaonesha kuwa, itachukua saa 26 na sita kwa nchi zote duniani kuuona mwaka mpya na nchi ya kwanza, Visiwa vya Samoa na Tonga, ndivyo vitakavyokuwa vya kwanza kuuona mwaka, ambapo wakati wao kwa saa za kwao ikitimia saa sita kamili za usiku, Bongo itakuwa ni saa saba za mchana, ya Jumamosi. Miji ya Kiribati, Nukualofa na Apia ndiyo itakayokuwa ya kwanza.

Nchi zitakazofuatia zitakuwa ni Urusi ambao watauona mwaka wakati Bongo ikiwa ni saa tisa alasiri, wakifuatiwa na Australia ambapo Miji ya Melbourne, Sydney, Canberra na Honiara, itauona mwaka saa kumi za jioni.

Japan na Korea Kusini zenyewe zitauona mwaka saa 12 jioni ya Jumamosi. China, Singapore na Ufilipino, wao watauona mwaka saa moja jioni ya Jumamosi. India na Sri Lanka wao watauona mwaka saa tatu na nusu, Pakistan na Afghanistan watauona mwaka saa nne.

Watakaouona mwaka saa tano za usiku, ni pamoja na Dubai (Falme za Kiarabu) na Iran.

Muda ambao Watanzania tutakuwa tukiuona mwaka mpya, tutauona sambamba na wakazi wa Moscow, Urusi, Iraq na Sudan sambamba na Misri, Ugiriki na Afrika Kusini ambao wao watauona mwaka muda mfupi baada ya sisi kuuona.

Watakaochelewa zaidi kuuona mwaka, ni Canada na Marekani ambapo baadhi ya majimbo yataanza kuuona mwaka Asubuhi ya Jumapili na kuendelea mpaka saa tano asubuhi ya Jumapili, wakati Visiwa vya Baker na Howland ambavyo vipo chini ya Ufaransa, ndivyo vitakavyokuwa vya mwisho kuuona mwaka, saa 9 alasiri, Jumapili.

Hayo ndiyo maajabu ya Mwaka Mpya!

Na Hashim Aziz/GPL

 

Comments are closed.